The House of Favourite Newspapers

MWAKIFWAMBA MBARONI KWA GARI LA WIZI

RAIS wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba Ijumaa iliyopita amepatwa na msala baada ya kunaswa akiwa na gari aina ya Mercedes Benz 350 SDL linalodaiwa kuwa ni mali ya Dokta Fabian Mbunda.

 

Chanzo chetu cha kuaminika ambacho kimeomba jina lake lisiandikwe gazetini kimedai kuwa, Dokta Mbunda ambaye anafanya kazi ya urubani huko Marekani ndiye mmiliki halali wa gari hilo lakini katika mazingira ya kutatanisha limetua mikononi mwa Mwakifwamba na kumfanya ajikute matatani.

 

“Lile gari ni la dokta na mara nyingi akiwa Tanzania analitumia, akiondoka anamuachia jamaa mmoja anaitwa Shabani, akija siku nyingine analichukua, analitumia.

 

“Hivi karibuni wakati dokta anajiandaa kuja Tanzania, akampigia simu Shabani na kumpa taarifa za ujio wake. Cha ajabu alipotua na kuanza kumpigia simu Shabani hakuwa akipokea na hata alipotumiwa SMS hakujibu.

 

“Machale yakamcheza, wapambe wakamtonya kuwa mshikaji aliyemuachia gari lake alikuwa ameliuza kwa Mwakifwamba. Hapo ndipo Dokta Mbunda alipoanza kumsaka. Alipoona juhudi za kumpata zinagoma aliamua kwenda kuripoti katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay na kumfungulia jalada la kesi lenye namba OB/RB/3022/2019 WIZI WA KUAMINIWA.

Baada ya kufungua kesi hiyo inadaiwa Shabani aliendelea kutoonekana lakini gari hilo lilionekana mitaani akitesa nalo Mwakifwamba hivyo ikabidi polisi walikamate. Chanzo kinadai kuwa, gari hilo likiwa mikononi mwa Mwakifwamba lilikamatwa maeneo ya Msasani Dar na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay ambapo staa huyo alihojiwa na kuachiwa lakini gari likaendelea kubaki kituoni hapo.

 

Kufuatia habari hiyo kutua kwenye meza ya Gazeti la Amani, mwandishi wetu alimtafuta Dokta Mbunda ambapo alipopatikana alisema: “Nikiwa nchini Marekani mara nyingi nilikuwa nikimuachia gari yangu Shabani ambaye tulikuwa family friend.

 

“Nikashangaa wakati nikiwa huko nilimpigia simu na kumwambia nataka kurudi nchini ambapo baada ya kumpa taarifa hiyo alianza kunikatia mawasiliano. “Kitendo cha kuanza kunikatia mawasiliano ghafla kilianza kunishtua, iweje mtu niliyempa mali yangu anitunzie aanze kunikatia mawasiliano.

 

“Basi siku ya kurudi nchini ilipofika nilirudi na kumfuata alipokuwa akiishi, nikaambiwa ameshahama. Niliendelea kumsaka bila mafanikio lakini nilipata taarifa kuwa gari langu linaonekana mitaani akilitumia Mwakifwamba, nikaenda polisi kuripoti na baadaye tukalikamata.

Baada ya kuzungumza na Dokta Mbando mwandishi wetu alimtafuta Mwakifwamba ambapo alipoulizwa juu ya madai ya kunaswa na gari la wizi naye alianza kuuliza maswali: “Hivi wewe unaona mimi naweza kuiba gari?”

 

Alipoeleweshwa kuwa yeye si mtuhumiwa wa wizi wa gari hilo isipokuwa gari hilo lina RB ya wizi wa kuaminiwa ndipo aliposema: “Lile gari mimi nimelinunua lakini ukitaka kujua undani njoo polisi Oysterbay.”

 

Aidha, mwandishi wetu alifanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Mussa Taibu ili kupata ufafanuzi wa sakata hilo ambapo alisema bado halijafika mezani mwake. Alipotaarifiwa kuwa tukio hilo lipo na kutajiwa RB alisema atalifuatilia kisha kutoa taarifa rasmi.

BABA DIAMOND – “Naumwa, DIAMOND Anipe KOLABO, Sijui KUIMBA”

Comments are closed.