The House of Favourite Newspapers

Mwakinyo, Bondia Mongo, Kayembe Moto Utawaka Leo

0

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo leo Agosti 14, 2020 amepania kupandisha rekodi yake katika pambano la kuwania ubingwa wa Super Welter dhidi ya bondia Mongo, Tshibangu Kayembe lililopangwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jioni hii.

 

Jana, mabondia hao walipima uzito na Mwakinyo alifikia kiwango cha kilo zinazotakiwa za uzani huo, huku Kayembe akizidi kilo na kulazimishwa kufanya mazoezi ili kufikia uzani kwa mujibu wa sheria.

Hali hiyo ilionekana kumpa shida Kayembe na hasa baada ya msimamizi wa upimaji huo, Emmanuel Mlundwa kusema kuwa endapo hatafikia kiwango cha kilo zinazohitajika anaweza kupoteza pambano kama akishinda.

 

Kayembe alikuwa na kilop 70.8, huku Mwakinyo akiwa na 68.8 na kutakiwa kutozidi kilo 69.7 kwa mujibu wa sheria.

Mlundwa alisema pambano linaweza kuwepo, lakini kama Mwakinyo atapigwa, basi Kayembe hatotambulika kuwa bingwa kutokana na kuzidi uzito.

Hali hiyo ilimfanya Kayembe kwenda gym kufanya mazoezi ili kufikia kiwango cha kilo ambacho kinatakiwa kwa mujibu wa taratibu.

Kwa upande wake, Mwakinyo alisema amejiandaa kuzichapa na Kayembe hata kama kilo zake zimezidi kwani amepania kupata matokeo mazuri na kuongeza alama katika viwango cha ngumi za kulipwa duniani, boxrec.

“Nimejiandaa kufanya vyema na si vinginevyo, nipo ardhi ya nyumbani na sitawaangusha Watanzania wenzangu. Nitamchapa hata kama amezidi kilo,” alisema Mwakinyo.

Kayembe hakuweza kuongea na waandishi wa habari kwani alipewa saa mbili za kupunguza uzito.

 

Pambano lingine ambalo linatarajia kuwa na upinzani ni kati ya bondia Baina Mazola na Haidary Mchanjo la uzito wa unyoya (Feather).

Mbali ya pambano hilo, Tonny Rashid atazichapa na bondia kutoka nchini Malawi, Yamikani Mkandawile litakalokuwa katika uzito wa Super Bantam.

 

Pia, aliyekuwa bondia nyota katika ngumi za ridhaa Selemani Kidunda atazichapa na Iddi Kaoneka katika pambano la uzito wa super middle. Kidunda kwa sasa amehamia ngumi za kulipwa.

Kidunda alisema kuwa baada ya kutamba katika ngumi za ridhaa, sasa ameamia katika ngumi za kulipwa kwa lengo la kuendeleza kipaji chake. “Sijawahi kupoteza pambano hapa nyumbani katika ngumi za ridhaa na hata baada ya kuhamia ngumi za kulipwa, hivyo Kaoneka ajiandae kwa kipigo,” alisema Kidunda

Leave A Reply