The House of Favourite Newspapers

Mwakyembe Kuhusu Yanga: Manji Asithubutu Kuichezea Serikali

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amemweleza wazi Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji, kuwa aache kuichezea Serikali, kama bado ana mapenzi na klabu hiyo achukue fomu kugombea nafasi, huku akiwaonya wale wote wanaopinga uchaguzi wa klabu hiyo waache mara moja.

 

Kauli ya Mwakyembe imekuja baada ya Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini Yanga, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, kutangaza juzi kuwa Manji ataendelea na kazi yake kama Mwenyekiti mwakani pindi afya yake itakapoimarika.

 

Mwakyembe aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, ambapo alieleza kama Yanga wanampenda Manji basi wamshawishi achukue fomu na kama wanaona inafaa sana basi wamchukulie.

 

Alisema Manji aliandika barua Mei 20, 2017, tena kwa Kiingereza kujiuzulu na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, alichukua nafasi kuwa Mwenyekiti wa Yanga na kuiongoza klabu hiyo.

 

“Tusicheze hii ni Serikali, achukue fomu agombee au wamchukulie, tulipata tabu sana pale Manji alipojiweka pembeni kwani Yanga ilitakiwa kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa lakini ilikuwa haina fedha.

 

“Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wadau ambao si viongozi walijitutumua kuchangia chochote, lakini hakuna hata senti tano iliyotoka kwa Mwenyekiti huyo wanayemlilia leo, tumechoka kuwabeba, umefika wakati Yanga ichague viongozi wake na tuione ikisimama kwa miguu yake, hilo ndilo lengo la Serikali, tumeichoka kuwa ombaomba.

 

“Kama kuna wana Yanga wanaona wataugua bila kuwapo Manji, basi wanaweza kumshawishi achukue fomu agombee lakini si kupitia njia ya mkato, kwanza wachague viongozi ambao wana uchungu na timu hiyo,” alisema.

 

Alisema kama Manji anataka kugombea lazima afuate sheria za uchaguzi, kwani pamoja na vyombo vya sheria kumhoji tangu Juni hadi Oktoba, mwaka huu, kuhusu kurudi kwake bado alikataa akisema hawezi kurudi Yanga.

 

“Hatuwezi kuwa na sheria mbili za uchaguzi moja ya Yanga na nyingine ya klabu nyingine, utaratibu wa klabu yoyote ni kwamba pale inapotokea kuna mapengo ya uongozi wanatakiwa kufanya uchaguzi na ufanyike kidemokrasia,” alisema.

 

Mbali na Manji, viongozi wengine wa Yanga waliojiuzulu ni Makamu Mwenyekiti, Sanga na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Hashim Abdallah, Salum Mkemi na Omar Said.

Wakati Mwakyembe akiyasema hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mchungahela, amesema uchaguzi huo upo pale pale ikiwemo ya kujaza nafasi ya Manji.

 

“Sisi uchaguzi unaendelea kama kawaida, hata nafasi ya Manji pia watu wanachukua fomu kama tulivyoelekezwa na Serikali.

“Kama Manji wanamtaka aendelee kuongoza basi waje wamchukulie fomu au aje achukue fomu, sisi tunafuata taratibu,” alisema.

 

Mchungahela aliweka wazi wanachama wote ambao wamekuwa vinara wa fujo na kuyumbisha zoezi hilo, habari zao zimeshafika kwenye kamati ya maadili akiwemo Mkuchika na muda wowote kuanzia sasa wataitwa na kuhojiwa.

Kwa upande wake, Rais wa TFF, Wallace Karia, amesisitiza iwe isiwe lazima klabu ya Yanga ifanye uchaguzi, kama walivyoelekezwa na Serikali kupitia Baraza la Michezo Tanzania (BMT).

 

“Sina la kusema lakini niwaambie neno moja, uchaguzi lazima ufanyike kutokana na agizo la Waziri Mwakyembe, hakuna kitakachozuia watambue wasitambue sisi haituhusu,” alisema Karia.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Januari 13, ukisimamiwa na TFF ambao utajikita kwenye kutafuta mwenyekiti, makamu wake pamoja na wajumbe wanne.

RAYVANNY Alivyotinga BASATA leo kuwekwa Kikaangoni!

Comments are closed.