The House of Favourite Newspapers

Mwalimu Adaiwa Kuua Mtoto wa Jirani

0

MAMA mmoja mkazi wa jijini Mwanza ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Islamic Nyasaka, Fatuma Rashadu amepata msala mzito.

 

Fatuma anadaiwa kumuua mtoto wa jirani yake mwenye umri wa miaka mitano aliyejulikana kwa jina la Farid baada ya kumchapa kwa fimbo akiwa shule, kisa kikiwa ni kumvua nguo mtoto wake wa kike na kumlalia.

 

Akizungumza kwa uchungu mno, mama wa mtoto huyo anasema kuwa, aliamka asubuhi kisha akamuandaa mtoto wake na kumpeleka Shule ya Angelina anayosoma siku zote na kurudi nyumbani, kumbe huko nyuma, mwalimu huyo alimpeleka mtoto wake huyo kisha kumuomba mwalimu amuitie mtoto Farid.

 

“Mwalimu aliniambia alivyofika pale shuleni, mama Maisala ambaye ni mwalimu wa shule ya Sekondari ya Islamic Nyasaka alimuomba mwalimu mtoto wangu alivyotoka, akaanza kumchapa sijui na nini kisha akazimia na kuanza kumwagia maji ndipo mwalimu akatoka na kumwambia inabidi ampeleke hospitalini,” anasema mama huyo.

 

Mama huyo anaendelea kuzungumza kuwa, alipokea simu kutoka kwa mwalimu na kumuuliza mtoto wako ana tatizo la kuzimia maana amezimia shuleni ndipo mama huyo akapatwa na mshtuko mkubwa.

 

“Baada ya mama Maisala kuona mwanangu amezimia, walimu wakamwambia ampeleke hospitali ambapo alimpeleka Hospitali ya Kiloleni na baada ya muda niliona dada wa kazi wa yule mama analeta viatu vya mwanangu na kusema yupo hospitalini Kiloleni Juu.

 

“Hapohapo nikapokea simu ya mama huyo akiniambia naitwa na daktari hospitalini hapo,” anasema mama huyo.

Anaendelea kusema kuwa, baada ya kwenda hospitali hapo aliingia mpaka kwa daktari na kuambiwa mtoto wake amefariki dunia.

 

Wakati akitoka hospitalini hapo akilia ndipo mwalimu huyo akachukua boda na kuondoka mpaka nyumbani kwake ambapo majirani walizingira nyumba yake.

 

“Unajua alipokuja yule dada wa kazi aliyeleta viatu vya mwanangu alisema kuwa, alimuelezea yule bosi wake kuwa wakati anakwenda kumchukua mtoto shuleni alimkuta marehemu amevua nguo, amemlaza chini amemlalia mwanaye kwa juu ndipo alipokwenda kumueleza yule bosi wake na kuamua kwenda kumuadhibu shuleni hadi akamuua mwanangu,” anasema mama huyo.

 

Gazeti hili lilizungumza na mtangazaji Flora Lauo ambaye alisaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kuweza kuzungumza naye ambapo alisema kuwa hakumpiga mtoto huyo fimbo nyingi zaidi ya mbili kwani hiyo tabia anaifanya siyo chini ya mara moja.

 

“Mimi nilimpiga kama kumfundisha tu na kama mzazi na sikumfanya chochote kingine maana hana hata jeraha kwa sababu mimi ni mzazi pia, ninapaswa kumfundisha na sikuwa ninakimbia bali nilikuwa nimekuja nyumbani mara moja kuchukua pesa,” anasema mtuhumiwa huyo kabla ya Polisi kumtia mbaroni.

 STORI: IMELDA MTEMA, MWANZA

Leave A Reply