The House of Favourite Newspapers

Mwalimu bora duniani kutoka Kenya akutana na Trump

 

BROTHER TABICHI ni mtawa wa Shirika la Kikatoliki la Mtakatifu Fransisco wa Capuchini na alishinda tuzo ya mwalimu bora duniani mnamo Machi 2019.

Mwalimu huyo anafundisha  sayansi katika Shule ya Sekondari ya Keriko katika kaunti ya Nakuru, kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Picha ya Tabichi akikutana na Rais wa Marekani, Donald Trump,  iliyowekwa na ofisa wa mawasiliano kutoka Ikulu ya Marekani, kwenye Twitter, imesema  Tabichi alitoa asilimia 80 ya mshahara wake kwa mwezi kuwasaida masikini nchini mwake, Kenya.

“Uwajibikaji wake na kazi yake ngumu na imani kwa wanafunzi, umeifanya shule anayofundisha kuibuka kidedea baada ya kushindana na shule zingine bora nchini katika mashindano ya kitaifa ya sayansi. Peter, unatutia moyo sisi sote! Asante kwa uwajibikaji wako kwa wanafunzi wako,” alisema Stephanie Grisham ofisa wa Ikulu ya Marekani.

Tabichi anatarajiwa kutoa maombi kabla ya kuanza kwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York baadaye leo. Anatarjiwa pia kuzungumzia kidogo kuhusu namna alivyofanikiwa kufika alipofika katika taaluma ya ualimu.

Tabichi amenukuliwa akisema kwamba: “Hii ni heshima kubwa kwa watawa wa St Franciscan. Inaonyesha kuwa Umoja wa Mataifa unatutambua kutokana na kwamba ina jukumu kuu katika kuendeleza utu.”

Katika tuzo hiyo iliyotolewa katika shindano lililoandaliwa na Wakfu wa Varkey, Brother Peter, aliwapiku washiriki wengine 10,000 waliochaguliwa kutoka nchi 179.
Brother Peter anasema kuna “changamoto ya ukosefu wa vifaa ” katika shule yake ukiwemo uhaba wa vitabu na waalimu.

Madarasa yenye uwezo wa kuwa na wanafunzi kati ya 35 hadi 40 hulazimika kuwa na wanafunzi 70 na 80, jambo analosema linamaanisha kuwa darasa linakuwa na wanafunzi wengi kupita kiasi, na ni tatizo kwa walimu.

Ukosefu wa Intaneti ya kuaminika unamlazimisha kusafiri hadi kwenye cyber-cafe kwa ajili ya kupakua maelezo ya masomo yake ya sayansi. Na wanafunzi wengi hutembea zaidi ya maili nne kwenye barabara mbovu hadi kufika shuleni. Lakini Brother Peter anasema ameazimia kuwapatia fursa ya kusoma na kufikia ndoto zao.

Comments are closed.