The House of Favourite Newspapers

Mwanafunzi Anayedaiwa Kuanika Tatizo la Maji UDOM Akamatwa

0

MWANAFUNZI wa mwaka wa pili anayesomea Shahada ya Sayansi ya Asili (Natural Science) katika Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Mugaya Tungu,  amekamatwa Januari 21, 2020,  akiwa ndani ya bweni la wanafunzi chuoni hapo.

 

Inadaiwa  alikamatwa bila kuambiwa kosa lake ni lipi na kwa nini alikamatwa na kisha kupelekwa Kituo cha Polisi Chimwaga, Dodoma.

 

Lakini pia inaelezwa kuwa, rafiki yake wa karibu (jina lake limehifadhiwa) naye alifuatwa ili akamatwe usiku ila alishtuka mapema na hakulala chumbani kwake, hivyo polisi  hawakumpata.

 

Kwa mujibu wa  taarifa zilizopo,  wanafunzi wa UDOM wana changamoto ya kupata maji, hali inayowasababishia kupanga foleni muda mrefu na pengine kuchelewa masomo. Tungu anadaiwa kupiga picha za wenzake wakiwa wamepanga foleni muda mrefu na kwa wingi.

Jana, Januari 22, 2020, wenzake wanadai walifika kituo husika  cha polisi lakini hawakufanikiwa kumuona na kuambiwa kuwa Tungu alipewa dhamana ya polisi na walipohoji endapo kuna mtu amemdhamini waliambiwa hayo hayawahusu.

 

Hata hivyo, wanafunzi wenzake wamejaribu kupiga simu zake lakini hazipatikani na mwanafunzi huyo hajaonekana bwenini mpaka sasa hivyo bado haijulikani alipo.

 

Leave A Reply