The House of Favourite Newspapers

MWANAHARAKATI KUWATAJA WANAOTUKANA SERIKALI MTANDAONI

Mwanaharakati mzalendo, Laurence Jumanne Mabawa.

MWANAHARAKATI mzalendo ambaye alipata kuwa gumzo mwaka jana kwenye vyombo vya habari mbalimbali nchini, Laurence Jumanne Mabawa, amesema atawataja wanaotumia mitandano ya kijamii kuwatukana viongozi.

 

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, mwanaharakati huyo awali aliyekuwa na kampeni ya ‘Magufuli Baki’ amesema kwamba ameamua kuja na kampeni nyingine aliyoipa jina la ‘Washa Data Tetea Taifa’ ili kuweza kuweka sawa matumizi ya kimtandao yanayoendelea kwa sasa nchini na kuwabainisha wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuchafua viongozi.

 

“Unajua kwa sasa watu wengi hasa vijana wanaitumia mitandao ya kijamii kama sehemu ya kumaliza hasira zao kwa kuwatukana viongozi wa kiserikali, kuitukana serikali pamoja na mienendo yake kwa sababu wanadai hawasikilizwi.
“Ndiyo maana wanaamua kutumia mitandao ya kijamii kutukana na kusema mambo yasiyofaa jambo ambalo si zuri kwa taifa kwa sababu madhara yake ni makubwa,” alisema.

 

Mwanaharakati Laurent aliendelea kueleza kwamba mfano halisi wa taifa ambalo vijana walitumia mitandao ya kijamii vibaya na baadaye ikawaletea matatizo ni Libya.

 

“Libya lilikuwa ni taifa ambalo wananchi wake walikuwa wanaishi kwa amani lakini baada ya machafuko ambayo kwa sehemu fulani yalichangiwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii taifa hilo limekuwa si sehemu nzuri tena kwa wananchi kukaa,” alisema.

 

Aidha mwanaharakati huyo alieleza kwamba ameamua kuja na kampeni hiyo ambayo itaanza hivi karibuni ili kuwakumbusha vijana hasa wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii ili waitumie vizuri kwa ajili ya manufaa ya taifa.

 

“Katika kampeni yangu nitawataja watu mbalimbali ambao wanaitumia mitandao ya kijamii vibaya, kwa kuwatukana viongozi wa kiserikali na nitashirikiana pia na wananchi mbalimba wazalendo ambao hawapo tayari kuona taifa linaangamia kisa, mitandao ya kijamii,” alisema Laurence.

 

Alipoulizwa na wanahabari kwamba katika kampeni zake anatumika kisiasa alikana juu ya hilo na kueleza wazi kwamba yupo kwa ajili ya kutetea taifa kwa sababu yeye ni mwanaharakati mzalendo.

Comments are closed.