The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Jini Alivyonipenda na Kunipeleka Ujinini! – 2

0

ILIPOISHIA ALHAMISI:

Nikahisi labda palitokea wizi.  Wazo kwamba kuliingia wezi lilinifanya niyazungushe macho yangu pale sebuleni.  Lakini niliona kila kitu kilikuwa sawa.  TV ilikuwepo, sabuufa ilikuwepo pamoja na vitu vingine ambavyo kama kuliingia mwizi lazima angevichukua.

Nilijiambia hakukuingia wezi, aliyeingia alikuwa muuaji.  Nikasimama na kutoa simu yangu.  Nikawapigia polisi.

Haukupita muda mrefu polisi wakafika.  Wao pia walipomuona Farida walishtuka.

“Nini kimetokea?” polisi mmoja akaniuliza.

Nikamweleza kwamba yule alikuwa mdogo wangu tumbo moja na mimi.  Nikaendelea kuwaeleza jinsi nilivyotumiwa ile meseji na nilivyofika pale nyumbani na kukuta amechomwa kisu.

SASA ENDELEA…

“Mpaka sasa sijajua amepatwa na nini.”

“Umegundua kuna wizi wowote uliotokea?”

“Sidhani.  Naona kila kitu kipo. Huu si wizi, huu ni uuaji!”

Polisi wakaanza kuukagua mwili wa marehemu.

“Anaitwa nani?” polisi aliyekuwa akiniuliza maswali aliendelea kuniuliza.

“Anaitwa Farida Ibrahim Msangi.”

“Anaishi na nani?”

“”Anaishi peke yake.”

“Umesema alikutumia meseji asubuhi hii?”

“Ndiyo.  Meseji yenyewe hii hapa.”

Niliifungua ile meseji kwenye simu yangu na kumpa simu yule polisi.

“Halafu nadhani hii meseji hakuiandika yeye.  Iliandikwa na huyo mtu aliyemuua.  Alitaka nije nione kama mdogo wangu ameuawa.  Inaonekana kama alikuwa na kisasi na sisi.”

“Kwa nini unadhania hivyo?” polisi huyo akaniuliza.

Ni kwa sababu kama ingeandikwa na Farida asingeandika jina langu, angeandika kaka na ndivyo alivyoniita siku zote.

Polisi huyo akatingisha kichwa kunikubalia.

“Simu ya huyu msichana iko wapi?” akaniuliza.

Nikazungusha macho yangu kwenye ile sebule na kuiona simu ya Farida ikiwa kwenye kochi.

“Ile pale, nikamwambia yule polisi huku nikiifuata.

Wakati nataka kuichukua, polisi huyo akaniambia:

“Usiiguse!”

Niaiacha.

Polisi huyo akatia kitambaa kutoka mfukoni mwake akakiweka mkononi kisha akaishika ile simu kwa kutumia kitambaa hicho.

Hapohapo nikagundua sababu ya kuiambia nisiiguse.  Bila shaka aliona endapo nitaigusa nitaharibu alama za vidole zilizokuwa kwenye simu hiyo ambazo zilikuwa muhimu kwa uchunguzi wao.

Baadaye polisi wawili waliondoka.  Baada ya nusu saa hivi walirudi wakiwa na kifaa cha kuchukulia alama za vidole pamoja na kamera.

Waliupiga picha mwili wa marehemu kisha wakaanza kutafuta alama za vidole kwenye mpini wa kile kisu, kwenye simu, kwenye kitasa cha mlango wa mbele na cha mlango wa chumbani kwa marehemu.

Alama zangu pia zilichukuliwa pamoja na alama za vidole za marehemu mwenyewe.

Baada ya hapo mwili wa marehemu ulichukuliwa na kupelekwa hospitali.  Mimi nilipelekwa kituo cha polisi ambako niliandikisha maelezo yangu.

Polisi waliniuliza kama kulikuwa na mtu yeyote niliyokuwa nikimshuku kumuua mdogo wangu, nikawaambia sikuwa na mtu yeyote niliyekuwa nikimshuku.

Hili tukio linaashiria kwamba lazima kulikuwa na tatizo kati ya marehemu na huyo mtu aliyeandaa mauaji hayo.

“Tatizo lazima litakuwepo.  Hili suala linahitaji uchunguzi.”

“Marehemu hakuwahi kukueleza kama aliwahi kugombana na mtu hivi karibuni?”

Hakuwahi kunieleza.”

“Basi tuache tuendelee na uchunguzi wetu na utakapopata fununu yoyote juu ya chanzo cha mauaji haya usisite kuja kutuambia.”

“Sawa.”

Nilipotoka kituo cha polisi nilirudi nyumbani kwangu na kuanza kuwapigia simu ndugu, jamaa na marafiki kuwajulisha kuhusu kuuawa kwa Farida.

Msiba wa Farida ulifanyika katika nyumba niliyokuwa nikiishi mimi.

Mazishi yake yalifanyika siku ya pili baada ya ile siku aliyouawa.

Tukio lile lilinitia huzuni na majonzi mengi.  Ndugu yangu wa pekee niliyezaliwa naye alikuwa ni Farida.  Kifo chake kilinihakikishia kuwa sasa nilikuwa nimebaki peke yangu.

Lakini siku zikapita.  Mara kwa mara nilikuwa ninakwenda kituo cha polisi kuulizia kuhusu uchunguzi wa mauaji ya mdogo wangu.  Jibu nililolipata liliuwa “Bado tunaendelea na uchunguzi”.

Ikapita miezi mitatu.  Kulikuwa na siku Mishi alikwenda kwao Arusha kuwasalimia ndugu zake.  Aliniambia kuwa atakuwa huko kwa wiki moja.

Kuondoka kwake kuliniachia upweke kwa vile nilishazoea kuwa naye.  Nikawa napotezea muda wangu mwingi kwa rafiki yangu aliyeitwa Martin aliyekuwa akiishi Raskazoni.

Siku nyingine Martin alikuwa akinirudisha usiku na gari lake aina ya Toyota RAV 4 na kuna siku nyingine nilikuwa nikimwazima gari hilo kwa ajili ya shughuli zangu binafsi.

Siku moja nilialikwa kwenye harusi ya rafiki yangu mmoja aliyekuwa akiishi wilayani Mkinga.

Nikaenda kuazima gari kwa rafiki yangu Martin ili niweze kuhudhuria harusi hiyo.

Niliondoka Tanga saa nne asubuhi nikafika Mkinga saa tano na nusu.  Ndoa ilifungwa saa saba mchana.  Baada ya  kufungwa kwa ndoa hiyo sherehe ziliendelea hadi usiku.

Je, nini kiliendelea.  Usikose kusoma hapahapa.

Na Faki A. Faki

Leave A Reply