Mwanamke kukosa hamu na msisimko wa tendo la ndoa -2

WIKI iliyopita tulianza kuliangalia tatizo hili la mwanamke kukosa hamu na raha ya tendo la ndoa ambalo kitaalam huitwa low sex drive. Tatizo hili huwa halianzi ghafla. Huanza taratibu sana na huchukua miaka mingi hadi kuja kujitokeza.

Mwanamke huanza kupata hali hii anapoanza mahusiano ambapo tatizo hujitokeza mwanzoni tu mwa mahusiano hayo au pale mahusiano yanapokwisha au kuvunjika au mume kufariki dunia au kama amepata mabadiliko makubwa maishani ambayo yameathiri afya yake.

Wapo wanawake ambao huwa hawana hamu ya tendo, lakini wakianzwa, hupata hamu, kitaalam tunasema wana msisimko mdogo wa hisia za tendo la ndoa, hali ambayo kitaalam inaitwa hypoactive sexual desire disorder au HSDD.

MATATIZO YA MAHUSIANO

Tuliangalia matatizo kadha wa kadha yanayoweza kuchangia tatizo hili kama matatizo ya kisaikolojia. Ukaribu na mpenzi wako hudumisha hamu na hisia za tendo, wanawake wengi hupata tatizo hili la kupoteza hamu na msisimko wa tendo la ndoa kutokana na mahusiano kuvurugika, endapo hakuna mawasiliano mazuri na mpenzi wako, aidha yupo eneo ambalo upo au yupo mbali na wewe, lakini hakuna mawasiliano, kuachana kwa ugomvi, wakati mwingine mnaweza kuwa mnaishi pamoja, lakini migogoro na ugomvi haviishi na wakati mwingine mnapigana kabisa, kutokuwa na mawasiliano ya uhakika au kutokujua na kutofuatilia kwa mwenzi wako endapo wewe unahitaji tendo hilo na kwa jinsi gani au wakati gani, wanawake wengi wanataka wafuatiliwe hivyo na wapenzi wao na wanakuwa wagumu kuanzisha. Katika hili, la mwisho ni kutoaminiana, mwanamke haaminiki au hamuamini mumewe na kuna hisia endapo atashirikiana naye, basi anaweza kupata magonjwa ya viungo vya uzazi, magonjwa ya zinaa au muwasho ukeni na hata Ukimwi.

DALILI ZA UGONJWA

Kutokupenda kushiriki tendo la ndoa kipindi ambacho mwenzio anahitaji au mwenzio anataka kuongeza na wewe hupendi na kuanza sababu mbalimbali. Hali hii huwa haiharibu uhusiano yaani unakuwa unashiriki tu kwa kumridhisha mwenzio. Mwanamke mwenye tatizo hili pia hana hamu kabisa ya tendo kwa jinsi yoyote, hata kukumbatiwa na mumewe hapendi, hana hata mawazo au stori zozote za tendo.

UCHUNGUZI

Hufanyika katika kliniki maalum za madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama au Gynecologist au wengi huwaita Gaino. Daktari atakufanyia uchunguzi kuangalia hali zisizo za kawaida au pelvic examination, uchunguzi wa kuta za uke na sehemu nyingine zitafanyika. Wanawake wengi walio katika umri wa kuzaa kuanzia miaka 20 hadi 45 hupatwa na tatizo hili la kupoteza hamu na raha ya tendo kutokana na kusinyaa, ukavu, kutokuwa na majimaji ya kulainisha uke na hali hii wakati mwingine huhisi maumivu wakati anapoingiliwa. Vipimo mbalimbali vya damu vitafanyika kuangalia mfumo wa homoni, magonjwa ya mwili. Historia ya ugonjwa itafahamika kwa undani na baada ya uchunguzi wa kina ni tiba.

MATIBABU

Kwanza ni kubadilisha mtindo wa maisha na kurekebisha matatizo yaliyo juu ya uwezo wako. Matibabu ya dawa yatatolewa baada ya kuthibitisha tatizo. Pamoja na dawa mbalimbali ziwe za kunywa, kupaka au sindano, basi kama mwanamke hana tatizo kubwa ila tatizo ni ukavu wa uke na maumivu na kutofurahia tendo au kukosa msisimko, basi daktari atakupatia dawa maalum ya kupaka ukeni ambayo ina kazi ya kuboresha kuta za uke, kurudisha hali ya maji maji ukeni, kukuletea msisimko wa tendo na kuondoa maumivu. Dawa hii hupakwa ukeni kwa kiasi kidogo mara kwa mara na kukurudisha katika hali ya kawaida, ina homoni za kike. Inaweza kutumika na wanawake hadi umri wa miaka 55. Zaidi muone daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama katika hospitali au kliniki.

-MWISHO-


Loading...

Toa comment