Mwandishi Mwandamizi wa Global Publishers Haruni Sanchawa afariki dunia

sanchawa (2)

Haruni Sanchawa enzi za uhai wake.

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Global Publishers LTD, wachapishaji wa magazeti ya Ijumaa, Uwazi, Risasi, Amani, Ijumaa Wikienda na Championi, leo imepata pigo kubwa la kufiwa na mfanyakazi wake mahiri, Haruni Sanchawa aliyefikwa na umauti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar.

Sanchawa aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya tumbo, amefariki dunia leo saa 8 mchana ikiwa ni saa chache tangu alipohamishiwa katika hospitali hiyo baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Amana alipokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.

sanchawa (3)

Haruni Sanchawa akifanya mahojiano na Athuman Hamisi ambaye alikuwa Mpiga Picha wa magazeti ya Serikali ya Tanzania Standard Newspapers.

Sanchawa ambaye alikuwa mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi kupitia Gazeti la Uwazi, alikuwa akiishi nyumbani kwake Gongo la Mboto, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mjomba wa marehemu, taratibu zote za mazishi zitaanza kufanyika nyumbani kwake Kitunda, Dar ambapo taarifa za awali zinaeleza kuwa mwili wa marehemu utasafirishwa Ijumaa kuelekea Mugumu, Serengeti mkoani Mara kwa mazishi.

sanchawa (1)

Marehemu Sanchawa akikabidhi msaada enzi za uhai wake.

Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya Global Publishers LTD, Mkurugenzi Mtendaji, Eric Shigongo amesema, kampuni imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Sanchawa na kwamba pengo lake halitazibika.

“Alikuwa kijana mchapakazi. Amefanya makubwa sana katika habari za uchunguzi kupitia gazeti letu la Uwazi. Sisi kama kampuni tunawapa pole familia na pia tunamuombea kwa Mungu apumzike kwa amani. Kwaheri Sanchawa, tutakukumbuka daima,” alisema Shigongo.

Marehemu Sanchawa ameacha mjane na watoto wawili. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina!


Loading...

Toa comment