The House of Favourite Newspapers

Mwanza; Denti sekondari Auawa Kilabuni

0

Mashaka Baltazar, AMANI

MWANZA: Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Thaqaafa iliyopo Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Amos Kitala (26) ameuawa kikatili kwa kukatwa shingo kwa kipande cha chupa kwenye ugomvi kati yake na watu wawili aliokuwa akigombana nao, Amani lina habari yote.

SIKU YA TUKIO
Tukio hilo la kinyama lilitokea Machi 19, mwaka huu, majira ya saa 10:00 jioni wakati mwanafunzi huyo  aliyekuwa akisoma kidato cha sita katika shule hiyo akiwa kwenye kilabu hicho kinachouza pombe mbalimbali za kienyeji.

UGOMVI HAUJULIKANI
Kwa mujibu wa mashuhuda, siku ya tukio, marehemu Kitala akiwa kilabuni hapo ulizuka ugomvi kati yake na watu wawili waliotajwa kwa majina ya Ramadhan Sima (27) na Omar Philip ambapo inadaiwa kuwa, katika mpambano wao marehemu aliwazidi nguvu hivyo kuonekana anapata ushindi.
“Kwanza ugomvi wenyewe wala haujulikani kisa nini. Lakini kutokana na kuzidiwa nguvu na Kitala kwenye ugomvi huo, Sima na Philip waliamua kuchukua moja ya chupa za pombe za kilabuni hapo wakaivunja kisha kumkata nayo shingoni kwa kutumia kipande chake hivyo kusababisha marehemu atokwe na damu nyingi kabla ya kukata roho papo hapo.
“Kwa kweli yule kijana mwanafunzi amekufa kifo kibaya sana. Hii dunia yetu kwa sasa haina huruma wala haina kuvumiliana,” alisema shuhuda mmoja.

KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kueleza kwamba, watuhumiwa Omar na Ramadhan  wanashikiliwa na jeshi hilo wakihusishwa na mauaji hayo.
Kamanda Kamugisha alisema kuwa, baada ya upelelezi kukamilika, watuhumiwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria huku akiwataka wananchi kutii sheria bila shuruti kwani serikali ya awamu ya tano iko macho sana.

Leave A Reply