The House of Favourite Newspapers

Mwanza; Majambazi Yaua Mdada Muuza Magazeti

0

MWANZA; Majambazi wanaosadikiwa kuwa watatu, wamevamia na kumuua mfanyabiashara kwa njia ya mtandao wa simu na aliyekuwa muuza magazeti mkoani hapa, Naomi Lewis (35).
Tukio hilo la kusikitisha lilijiri usiku wa Aprili Mosi, mwaka huu majira ya saa tatu usiku katika Mtaa wa Temeke, Nyakato wilayani Nyamagana mkoani hapa baada Naomi kuvamiwa na majambazi hayo wakati akitoka kazini karibu na nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara wenzake waliokuwa wakifanya naye kazi katika eneo la Mwanza Hoteli, Naomi aliondoka katika eneo la kazi majira ya saa moja usiku kuelekea nyumbani kwake kama ilivyo kawaida lakini siku hiyo hakukua na tatizo lolote kazini.
“Ilipofika majira ya saa nne usiku tulianza kupokea simu kutoka kwa watu zikisema Naomi ameuawa na majambazi, wengi tulidhani utani kwa kuwa tarehe moja mwezi huu huwa ni siku ya wajinga duniani hivyo hatukuwa na wasiwasi sana kuhusu jambo hilo.

“Simu zilivyozidi ilibidi tumpigie (Naomi) lakini simu yake iliita bila kupokelewa, wasiwasi ulituingia na uhakika tulikuja kuupata kesho yake (Jumamosi) baada ya kufika eneo la kazi.

Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia Amani kuwa Naomi alishuka kwenye daladala katika Kituo cha Nyakato Sokoni akitokea mjini (kazini) na kuchukua pikipiki ili impeleke nyumbani kwake Mtaa wa Temeke, walipofika karibu na kwake alishuka kwenye ile bodaboda na kuchukua mkoba kwa lengo la kumlipa fedha yule bodaboda aliyejulikana kwa jina la Maduhu John (28) lakini kabla hajatoa fedha kumlipa, majambazi wapatao watatu walimkaba na kufyatua risasi moja hewani kwa lengo la kutawanya watu.

“Ilichukua muda kama wa dakika tatu hivi ndipo risasi ya pili ilisikika ambayo ilimuua Naomi na majambazi hao kukimbia kusikojulikana,” alisema mmoja wa mashuhuda.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema kuwa walipokea taarifa za tukio hilo na kufika kwenye tukio lakini uchunguzi bado unaendelea ili kubaini watu ama kikundi kinachojihusisha na ujambazi huo ili kuwakamata na kuwachukulia hatu za kisheria.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema tangu alipokabidhiwa ofisi hiyo kumekuwa na ongezeko la majambazi kutumia silaha hivyo atahakikisha ulinzi unaimarishwa kila sehemu ili wananchi wafanye kazi zao bila kuwa na wasiwasi wowote.

Matukio ya ujambazi kwa mwaka huu katika Mkoa wa Mwanza yanazidi kuongezeka, tukio la kwanza lilitokea Mtaa wa Chake ni Chake ambapo majambazi walivamia maduka mawili ya wafanyabiashara na kumuua fundi viatu kisha kujeruhi watu watatu, tukio lingine lilitokea Nyegezi ambapo majambazi walivamia duka la huduma ya pesa na kujeruhi watu wawili na lingine llitokea Bukarika ambapo watu wawili waliuawa. Matukio yote hayo yametokea ndani ya mwaka huu na jeshi la polisi bado halijafanikiwa kukamata jambazi hata mmoja.

Leave A Reply