The House of Favourite Newspapers

Mwanza watakiwa kutunza mazingira ili kulinda vyanzo vya maji.

0

WAKAZI pamoja na taasisi mbalimbali zinazoendesha shughuli zake za kimaendeleo kando ya Ziwa Victoria wametakiwa kutunza na kulinda chanzo hicho cha maji ili kuhakikisha linaendelea kuhudumia Taifa kupitia usambazaji wa Maji pamoja na kutoa samaki ambalo ni zao kuu la biashara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla.

 

Hayo yamebainishwa jana na Ofisa uhusiano kwa umma kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria Gerlad Itimbula wakati akitoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwa wanafunzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo kampasi ya Mwanza kufuatia maadhimisho ya siku ya Mazingira Dunia.

Alisema jukumu la kulinda chanzo hicho pamoja na vyanzo vingine vya maji ni la kila mtu hivyo uchafuzi wa aina yoyote unaweza kusababisha maji yake kutokuwa safi na salama sambamba na kuua viumbe waishio majini ambao kwa asilimia kubwa ni tegemeo katika uchumi wa Taifa.

“Ziwa hili linatakiwa kulindwa kwa kupanda miti, kudhibiti uchafuzi wa aina yoyote na hatua za kisheria uchukuliwa kwa wote ambao wanakiuka matakwa ya utunzaji na uhifadhi wa Ziwa Victoria,” alisema

Aidha aliongeza kuwa majukumu bodi hiyo ni kuhakikisha vyanzo vyote vinavyopeleka maji yake Ziwa Victoria vinalindwa na kuwa salama wakati wote ili kuwezesha shughuli za usambazaji maji kwa binadamu na viwanda yanakuwa salama.

Ofisa Mazingira Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria,Patrick Lucas alisema katika eneo la chanzo cha maji kuanzia Mita 60 hakuna shughuli zozote za kibinadamu bali zile tu za kulinda chanzo hicho kama upandaji miti kufuatia sheria na 11 ya mwaka 2019 sheria ya kulinda na kuhifadhi mazingira.

Ofisa Mazingira Wilaya ya Ilemela Phineas Marcon alisema kama Halmashauri wameweka sheria ndogondogo kwaajili ya utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji ambazo zimesaidia kudhibiti taka ngum,taka maji pamoja na taka yabisi na kufanya Halmashauri kuwa Safi na salama.

Adam Omoro ni Mwanafunzi wa chuo hicho ameahidi kutumia elimu ya utunzaji mazingira kuahakikisha anahifadhi mazingira yeye mwenyewe sambamba na kuhamasisha wengine kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji.

Leave A Reply