The House of Favourite Newspapers

Mwarabu Hachomoki Leo Taifa Michuano ya Kombe la Shirikisho

Kikosi cha timu ya Simba Sc.

LEO Jumatano, kikosi cha Simba kinachoiwakilisha Tanzania Bara katika Kombe la Shirikisho Afrika, kitakuwa na mchezo wa kwanza wa hatua kwanza dhidi ya Al Masry ya Misri.

 

Mchezo huo unatarajiwa ku­pigwa saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambapo kihistoria, Al Masry inakuwa ni timu ya tano kutoka Misri kumenyana na Simba katika michuano ya kimataifa, tangu ilipokutana na Haras El Ho­doud katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

 

Simba imefanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuwaondoa, Gendermarie ya Djibouti kwa jumla ya mabao 5-0 wakati Al Masry wakiwatoa Green Buffaloes kwa jumla ya mabao 5-2 huku timu hiyo ikiwa ni miongoni mwa timu zinazotoa upinzani mkubwa kwa vigogo wa Misri ikifundishwa na mshambuliaji wa zamani wa Zamalek, Hossam Hassan.

 

Rekodi zinaonyesha kuwa, Sim­ba inapokutana na timu za kutoka mataifa ya Kiarabu imekuwa ikifanya vizuri zaidi kwenye uwanja wa nyumbani ambao leo utawaka moto ambapo kwenye Kombe la Shirikisho kuanzia mwaka 1993 katika robo fainali ya michuano hiyo ilicheza na USM EL Harrach kutoka Algeria na katika mchezo wa kwanza Simba ilishinda mabao 3-0 wakati ziliporudiana Simba ilifungwa 2-0. Ikasonga mbele.

Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre

Mwaka 2010, Simba ilikutana tena na Haras El Hodoud katika raundi ya pili ya michuano hiyo ambapo katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar, Simba ilishinda kwa mabao 2-1, ziliporudiana huko Misri, Simba ilifungwa mabao 5-1. Ikatolewa.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre, alisema wamejipanga kuibuka na ushindi katika mchezo huo kwa kuwa amewaangalia wapinzani wao vizuri, wanapokuwa nyumbani kwao hucheza kwa jihadi kubwa.

 

“Maandalizi kuelekea mchezo wa kesho (leo), yamekamilika kwa asilimia mia kwa sababu tumefanya mazoezi ya kutosha na tumeangalia video za wapin­zani wetu na kujua namna walivyo kiuchezaji, hivyo kitu ambacho kwetu tumekipa kipaum­bele ni kuhakikisha tunapata matokeo ya ushindi ambao utatusaidia katika mchezo wa marudiano.

 

“Kitu kizuri nimecheza soka kabla ya kuwa mwalimu, hivyo naelewa tabia za timu za Kiarabu zilivyo na ikizingatiwa wapinzani wetu wakicheza kwao wanakuwa wakali kwa kucheza kwa jihadi kubwa kwa kutaka kufanya vizuri, sasa lazima kwetu tuitumie vizuri nafasi ya kucheza kwenye uwanja wa nyumbani kwa kupata ushindi mkubwa ili utusaidie mbele.”

 

Lechantre aliongeza kuwa hawezi kuweka wazi mfumo atakaoutumia kwa safu yake ya ushambuliaji lakini anaamini baada ya mazoezi ya mwisho ambayo yalifanyika jana jioni, kila kitu kitakwenda sawa kabla ya mchezo wenyewe.

 

“Nisingependa kusema nitafanya kitu gani katika safu yangu ya ushambuliaji kama nitatumia washambuliaji wawili au mmoja mbele, kwa sababu wote wapo tayari na hilo litabaki kuwa suala la benchi la ufundi kwa kuwa kikubwa tunataka ushindi wa nyumbani,” alisema kocha huyo.

Comments are closed.