The House of Favourite Newspapers

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini Aagiza Miradi Ikamilike Kabla ya Desemba 2023

0

ATAKA WAKANDARASI KUHAKIKISHA UBORA NA WELEDI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Wilaya za Nachingwea, Nanyumbu, Masasi na Tandahimba kukamilisha miradi yao ifikapo Desemba 31, mwaka huu.
Pia amewaelekeza kuhakikisha ubora, weledi na kukamilika kwa wakati miradi yote wanayoisimamia ili wananchi wapate huduma kwa muda uliopangwa.
“Nishati ni kila kitu, usalama, uchumi, siasa, afya na maeneo mengi, hivyo, jukumu la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni kuhakikisha kuwa wanawapatia wananchi umeme ili waweze kutimiza malengo yao,” amesema Balozi Kingu.
Amesema hayo katika kikao chake na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya nishati vijijini katika Mkoa wa Mtwara ambapo amewataka watendaji wa REA na TANESCO kuwafuatilia kwa karibu kuhakikisha kuwa lengo la kuvifikia vijini vyote ifikapo Juni 30, 2024 linafikiwa.
Wakandarasi hao , NAMIS Corporate na Central Electrical International Co, wametakiwa kuongeza nguvukazi na upatikanaji wa vifaa kwa wakati
ili ifikapo Novemba 30, 2023 vijiji vyote walivyopangiwa kimkataba viwe vinawaka umeme.
Amewaagiza kutumia vifaa vinavyozalishwa  na kupatikana katika viwanda vya ndani ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuagiza nje vile tu ambavyo havipatikani nchini.
Ametaka kikao cha tathmini kifanyike Desemba Mosi mwaka huu  na wakandarasi hao na kuona kama wako katika muda uliopangwa na endapo
kuna changamoto waone namna bora ya kuzitatua kwa pamoja.
Pia amewataka Wakandarasi kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa kazi zao kila wiki ili kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa miradi hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amempongeza Balozi Kingu kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais Samia katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi na kuongeza kuwa anaamini kwa sifa yake ya uchapakazi, REA itaendelea kupata matokeo chanya zaidi.
Kanali Ahmed amesema anatamani kuona wananchi wote wa vijijini wanafikiwa na umeme kama ilivyodhamiriwa na Serikali ili waweze kuboresha maisha yao na kwamba hana shaka kuhusu kutimia kwa jambo hilo ikiwa wote wanaohusika watashirikiana.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Mtwara, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu alisema hadi sasa, vijiji 384 kati ya 785 vimekwishafikishiwa huduma ya umeme na kwamba kazi inaendelea ili kukamilisha vijiji vyote.
Mhandisi Olotu ambaye ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, amesema Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (R3-R2) ambao ni mojawapo ya miradi inayoendelea kutekelezwa mkoani humo unalenga kufikisha umeme katika vijiji vyote 401 na kwamba Wakandarasi wanaendelea na kazi hiyo.
Aidha, ametaja miradi mingine inayoendelea kutekelezwa mkoani humo kuwa ni pamoja nan a Mradi wa Vijiji Miji, Mradi wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo ya madini, maeneo ya kilimo, vituo vya afya na pampu za maji pamoja na Mradi wa Ujazilizi.
“Hadi kufikia Novemba 15 mwaka huu, REA imewasha umeme katika vijiji 193 kati ya 401 ambavyo vilikuwa havina umeme kwa Mkoa wa Mtwara wakati Mradi wa R3-R2 unaanza kutekelezwa Julai, 2021.”
Mhandisi Olotu ameongeza kuwa, vijiji 208 vilivyobakia vitafikishiwa umeme kabla ya Juni 2024.

 

Leave A Reply