The House of Favourite Newspapers

Mwili wa Mtangazaji Kibonde Kuzikwa Kesho

Aliyekuwa mtangazaji mahiri wa Kituo cha Redio cha Clouds FM, Ephraim Kibonde enzi za uhai wake.

 

MWILI wa aliyekuwa mtangazaji mahiri wa Kituo cha Redio cha Clouds FM, Ephraim Kibonde unatarajiwa kuzikwa kesho Jumamosi jijini hapa baada ya kufariki jana mkoani Mwanza.

 

Kibonde alifikwa na umauti katika Hospitali ya Bugando ambapo alikuwa akipatiwa matibabu baada ya kukumbwa na ugonjwa wa ghafla wakati akiwa Bukoba katika msiba wa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds, Ruge Mutahaba.

Akizungumzia msiba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media, Joseph Kusaga alisema: “Leo (jana) Clouds tumepata pigo lingine kubwa kwa kumpoteza mtangazaji wetu mahiri, Ephraim Kibonde, saa 12 na nusu leo (jana) ndiyo muda ambao mwenzetu Kibonde alipoteza maisha, nilipigiwa simu asubuhi na kufahamishwa kuwa Kibonde hatuko naye tena.

 

“Matatizo yalianza tukiwa kwenye msiba wa mkurugenzi mwenzangu, Ruge Mutahaba, Bukoba ambapo Kibonde alipatwa na tatizo ambalo lilikuwa la ghafla ikabidi kumpeleka katika Hospitali ya Bukoba kwa matibabu tukisaidiana na dokta Isaac (Maro).

 

“Baada ya hapo ikaonekana kuna umuhimu wa kumpeleka haraka sana Mwanza ili aweze kutibiwa zaidi, tuliondoka Bukoba saa mbili na nusu asubuhi kuelekea Mwanza na kupokelewa katika Hospitali ya Uhuru pamoja na Dokta Derick na Dokta Isaac wakahangaika kumuweka sawa hali yake.

 

“Baada ya hapo aliendelea vizuri na mimi jioni ya jana nikaongea na Dokta Derick ambaye alinihakikishia kwamba yuko vizuri tu. “Lakini bahati mbaya nasikia usiku wakati wakijitayarisha sasa kurudi Dar es Salaam, hali yake
ilibadilika na kupoteza maisha saa 12 na nusu asubuhi katika Hospitali ya Bugando.

 

“Tunaurudisha mwili wa marehemu siku ya leo (jana) usiku saa nne, tutampokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kisha tutamhifadhi katika Hospitali ya Lugalo leo (jana) usiku.

 

“Kesho (leo) taratibu za mazishi na maombelezo zitafanyika nyumbani kwake Mbezi na siku ya Jumamosi tutamuaga rasmi na tutamzika siku hiyo, Mungu muweke mahali pema Epharim Kibonde,” alisema Kusaga.

Comments are closed.