The House of Favourite Newspapers

Mzee Dalali Awashukia Mabosi Simba

0

KUKOSA matokeo mazuri kwa timu ya Simba kumemuibua mwenyekiti wa zamani wa timu hiyo, Mzee Hassan Dalali ambapo amewashukia viongozi wa timu hiyo akitaka majibu ya chanzo cha hali hiyo.

Dalali ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo yeye pamoja na wazee wenzake wanatarajia kukutana kesho Jumapili kwa ajili ya kutafakari hali hiyo inayowaandama timu yao.

Mzee Dalali alisema kwenye kikao hicho wameagiza na kuwataka viongozi wote wa juu wa Simba akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez kuwepo kutoa majibu.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mzee Dalali alisema haiwezekani timu yao ikose matokeo kwenye mechi tatu jambo ambalo wao wanahisi kutakuwa na shida mahali na wenye kujua hayo ni viongozi hao.

“Tunataka watuambie pindi tutapokutana nao kesho kwa nini timu ikose matokeo kwenye mechi tatu mfululizo jambo ambalo siyo kawaida yetu. Waje watuambie shida ipo wapi.

“Tumewaambia lazima mwenyekiti wa bodi na C.E.O wawepo. Wao ndiyo wenye majibu sahihi ya haya maswali ambayo sisi wazee wa Simba tunataka kuyajua kutoka kwao,” alisema.

Simba haijapata matokeo kwenye mechi zao tatu za Ligi Kuu Bara wakichapwa 1-0 na Mbeya City na Kagera Sugar huku wakienda suluhu na Mtibwa Sugar.

Na Issa Liponda

Leave A Reply