The House of Favourite Newspapers

Mzee wa Baraza la Mahakama Akwamisha Kesi Ya Mke wa Bilionea Msuya

0
Kesi ya mauaji  inayomkabili mke wa aliyekuwa mfanyabiashara marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella imeshindwa kuendelea baada ya mzee wa baraza kushindwa kufika mahakamani kwa madai ya kuwa mgonjwa.
Katika kesi ya msingi washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 103/2018 wakidaiwa kumuua kwa kukusudia Aneth Msuya, dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya Mei 25, 2016 maeneo ya Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilipangwa kuendelea leo Jumatano Februari 23, 2022 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Edwin Kakolaki ambapo shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka alitarajiwa kuanza kutoa ushahidi wake.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Erick Tesha akisaidiana na Gloria Mwenda alidai kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa
Hata hivyo Jaji Kakolaki amesema kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa lakini mzee mmoja wa baraza ni mgonjwa, amepata tatizo la kiafya usiku na ameshindwa kufika Mahakamani.
“Sheria inatutaka tunaposikiliza shauri kama hili tusiendelee kama mzee wa baraza  mmoja wapo hayupo, inatulazimu kuahirisha shauri hili hadi hapo atakapopata nafuu,” amesema Jaji Kakolaki.
Baada ya maelezo hayo upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala na Nehemia Nkoko walidai hawana pingamizi.
Jaji Kakolaki ameahirisha Kesi hiyo hadi 1/3/2022 mwaka huu.
Leave A Reply