The House of Favourite Newspapers

Mzee Yusuf Awa Mhadhiri wa Kitaifa

mzee-yussuf-sheikhDAR ES SALAAM: Aliyekuwa staa mkubwa wa muziki wa Taarab Bongo, Mzee Yusuf ambaye kwa sasa amemrudia Mungu wake na kuwa alhaji, amefunguka kuwa bado watu hawaamini kama kweli ameachana na muziki wa kidunia hivyo wamekuwa wakimwalika kwenye misikiti mbalimbali ndani ya Dar na mikoani hivyo kuwa mhadhiri wa kitaifa (kwa mujibu wa Kamusi Sanifu, mhadhiri ni mtu anayetoa mhadhara, au mwalimu katika chuo cha elimu ya juu hususan chuo kikuu).

Akizungumza na Uwazi baada ya kuulizwa juu ya taarifa kwamba anafanya ziara kwenye misikiti mbalimbali na kutoa mawaidha (kufanya mihadhara) ya kumtangaza Mungu kwa nguvu zote, Mzee Yusuf alifunguka kuwa siyo kweli kwamba amepanga ziara ya misikitini bali huwa anaalikwa kwa ajili ya kutoa mawaidha ya Kiislamu.

“Siyo kwamba nimepanga ziara bali kila ninapoingia kwenye misikiti mbalimbali kuswali, watu wamekuwa wakinitaka nitoe neno kwa waumini hivyo nasimama, natoa mawaidha maana ndiyo upande niliochagua kwa sasa wa kumtumikia Mungu wangu.

“Nimekuwa nikipata mialiko kutoka kwa mashehe mbalimbali wa mikoani, ninakwenda kutoa neno maana watu wengi hawaamini kama kweli nimeachana na muziki hivyo ninasafiri sana na nikifika huko ndiyo wengine wanaamini na kuthibitisha.

“Kwa sasa nimeamua kusoma dini kiundani ili nijue nini Mungu anataka na nini hataki, siyo kusoma Quran bali nasoma dini niijue vizuri ,” alisema Mzee Yusuf, hata hivyo, watu mbalimbali wanasema familia yake iko mguu sawa kujiandaa kufuata nyayo zake.

Mwaka jana, Mzee Yusuf alitangaza kuachana na muziki wa taarab kisha akaenda kuhiji Macca, jambo liliibua mshtuko wa mashabiki wake lukuki wa bendi yake ya Jahazi.

Comments are closed.