The House of Favourite Newspapers

Mzungu Simba ampiga changa la macho Julio

0

Na Mohammed Mdose

SIMBA leo inacheza na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga, lakini kocha wake Dylan Kerr amesema kikosi chake kitatumia mfumo mpya ambao haijawahi kuutumia ili kuwazuga wapinzani.

Kerr raia wa Uingereza aliliambia Championi Jumamosi kuwa, ni lazima abadili mfumo kwani anakutana na Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye amewahi kuifundisha Simba.

“Tunacheza na kocha anayeifahamu Simba vizuri, sasa ni lazima nibadili mfumo na nitatumia mpya kabisa ambao hatujawahi kuutumia ili tuweze kushinda.

“Tukitumia mfumo wa siku zote itakuwa sawa na bure kwani kocha wao (Julio) anaujua na tunaweza kupata wakati mgumu kushinda, sasa nimeamua tuweke mabadiliko kidogo,” alisema Kerr ambaye timu yake ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 23.

Kerr alisema mara zote kocha anakuwa na wakati mgumu anapokutana na timu ambayo kocha wake alishawahi kuifundisha timu hiyo, kwani ni lazima atulize akili na kusuka mipango mipya.

Alisema kuwa kwakuwa kwa sasa timu yake inachohitaji ni ushindi tu na siyo kinginecho hivyo atatumia mfumo ambao utamfanya apate ushindi katika mchezo huo ambao wengi wanauona ni mgumu kwake.

“Najua Julio atawaelekeza wachezaji wake jinsi ya kutuzuia lakini nitautumia mfumo ambao hata siku moja hatujawahi kuutumia kwenye mechi yoyote ya ligi kuu, hapo lazima wapinzani wafeli,” alisema Kerr.

Leave A Reply