The House of Favourite Newspapers

Nabi aja na mbadala wa Mayele

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amemuangalia mshambuliaji wake Fiston Mayele akipaniwa na kutolewa macho na mabeki wa timu pinzani, haraka amechukua maamuzi magumu ya kumuingiza kikosini Chico Ushindi.

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Mayele kutamka kuwa anapaniwa na mabeki wa timu pinzani huku wakimuangalia yeye pekee baada ya kugundua ni mchezaji hatari katika timu.

Awali kocha huyo alikuwa akimuanzisha benchi Chico katika michezo ya Ligi Kuu Bara na kumuingiza kipindi cha pili akipewa dakika chache baada ya kukosa mechi fitinesi ambayo tayari ameiongeza mazoezini.

Mmoja wa viongozi wa Benchi la Ufundi la Yanga, ameliambia Championi Jumamosi kuwa ili wawavuruge mabeki wa timu pinzani, Nabi ameona ni vyema akamuanzisha Chico katika kikosi chake cha kwanza kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao katika mechi.

Kiongozi huyo alisema kuwa Nabi katika kikosi chake anataka wawepo wachezaji hatari wa kuogopwa na mabeki wa timu pinzani kama ilivyo kwa Mayele.

“Kocha anataka kuwa na washambuliaji wenye uwezo wa kufunga na kutengeneza mabao ambao pia ni hatari kwa mabeki wa timu pinzani.

“Nabi anaamini kuwa kama Chico akianza katika kikosi chake cha kwanza, basi namba ya mabeki wa kumkaba Mayele itapungua tofauti na ilivyokuwa hivi sasa katika timu akimtumia Moloko kama winga wa kulia.

“Alichopanga kocha ni viungo wawili wa pembeni wacheze Chico na Saido (Saidi Ntibanzonkiza) huku namba 10 akiwa Fei Toto (Feisal Salum) na 9 awe Mayele, wachezaji wote hao wana uwezo wa kufunga na kutengenezeana mabao,” alisema kiongozi huyo.

Nabi hivi karibuni alimzungumzia Chico na kusema kuwa: “Wachezaji wangu wote wana nafasi za kucheza na Chico nimeshindwa kumtumia katika kikosi cha kwanza kutokana na kutokuwa na mechi fitinesi.

“Nashukuru hivi sasa yupo fiti kabisa, tayari kwa ajili ya kupambana ndani ya uwanja baada ya kumuongezea mechi fitinesi iliyopotea baada ya kukaa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na majeraha.”

Musa Mateja na Wilbert Molandi

Leave A Reply