Nabi Atoa Masharti Mazito Usajili Yanga

KOCHA mkuu wa kikosi cha Yanga, Nasreddine Nabi ameuambia uongozi wa timu hiyo kuwa, hataki kuona wakirudia makosa waliyofanya misimu miwili iliyopita kwenye dirisha la usajili kwa kusajili wa nyota wengi wapya na kuacha idadi kubwa ya wachezaji.

 

Kwa misimu miwili iliyopita, Yanga imekuwa na kawaida ya kusajili nyota wengi wapya, huku pia ikitangaza kuachana na kundi kubwa la wachezaji ambapo kwa msimu uliopita pekee waliachana na wachezaji 14.

 

Yanga ambao wanakamatia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, wamedhamiria kuhakikisha wanarudisha utawala wao katika michuano mbalimbali watakayoshiriki msimu ujao, utawala ambao kwa sasa unaonekana kuchukuliwa na wapinzani wao wa jadi, Simba.Akizungumzia mipango yao ya usajili Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema:

 

“Kocha mkuu wa kikosi chetu, Nasreddine Nabi amesema anafurahishwa na ubora wa kikosi tulichonacho, na kuhusiana na maboresho kupitia usajili wa wachezaji wapya, kocha ameutaka uongozi kufanya usajili wa wachezaji watano au sita kwa ajili ya kuongeza nguvu.

Kocha Nabi hataki kuona tunaondoa wachezaji wengi kwa mara moja kama ambavyo ilitokea kwa misimu miwili iliyopita, hivyo tunatarajia kuachana na baadhi ya wachezaji wakiwemo wanaomaliza mikataba yao, ili kutoa nafasi ya nyota wapya ambao watatangazwa.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi,Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Yanga na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wa Yanga, Injinia Hersi Said kuhusu mipango ya usajili alisema: “Sisi kama GSM tumetenga dau kubwa la usajili wa nyota wapya, tunataka kutengeneza timu bora si tu kwa mashindano ya ndani, bali timu itakayofanya vizuri na kuweka rekodi kimataifa.”


Toa comment