The House of Favourite Newspapers

Nabii Suguye Afungukia Kanisa Kutumia Ushirikina Kuvuta Waumini

0
Mchungaji Kiongozi Nabii, Nicholaus Suguye wa Kanisa la The World of Reconciliation Ministries Ukonga jijini Dar Es Salaam akiwa katika Studio ya Global TV Online.

 

KATIKA mfululizo wa makala zetu za Live na Uwazi, wiki hii tunaye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la The World of Reconciliation Ministries (WRM) lililopo Ukonga wilayani Ilala jijini Dar, Nabii Nicolaus Suguye. Pamoja na mambo mengine, lakini katika mahojiano haya tutapata jibu la swali la wengi kuwa kwa nini Nabii Suguye anatoza fedha nyingi kwenye huduma yake ya maombezi? Ungana nasi; Uwazi: Nabii Suguye ni nani na ulianzaje kazi hii ya unabii? Nabii Suguye: Mimi ni mzaliwa wa Kibaha, Pwani lakini ni mkazi wa jijini Dar. Asili yangu ni mchanganyiko wa Kagera na Kusini mwa Tanzania.

 

Kabla ya kupata wito wa kuwahudumia watu nilikuwa mlinzi kwenye kampuni moja ya ulinzi hapahapa Dar. Siku moja nikiwa kazini, nilipata maono ya kumtumikia Mungu baada ya kutokewa na mwanga mkali na nikaona kiwiliwili kinakuja, ambacho sikuelewa ni cha kiumbe gani. Kiwiliwili kile kilipotua chini kikaanza kuniandikia maneno pale chini kuwa ninatakiwa kutii wito niliokuwa nao muda mrefu lakini nikawa sijautii. Mara baada ya kupata wito wa Mungu wa kuwahudumia watu bila kujali dini zao, niliamua kufuata maelekezo ya maono hayo na kuanzisha Kanisa la WRM ambalo kwa sasa lina zaidi ya waumini 5,000. Nilianzia ndani kwangu, tukiimba na mke wangu. Lakini tulipomaliza kuabudu, tulishangaa watu wanakuja na kusema tumesikia hapa kuna ibada ya watu wengi. Nikajua kuwa sauti zetu zilikuwa zikipaishwa na malaika.

Mhariri wa Gazeti la Ijumaa Wikienda, Sifael Paul (kulia) akifanya mahojiano na Nabii Suguye

 

Tuliwaambia ni sisi tu, nao wakashangaa. Hapo ndipo tukaanza kutafuta eneo la kuweka kanisa letu huku watu wakifurika kila kukicha wakihitaji huduma ya neno la Mungu na kuponywa katika magonjwa na shida zao mbalimbali. Sasa yapata zaidi miaka 20 tangu kuanza kwa huduma hii na sasa kanisa linajaa waumini. Wapo wanaoketi chini na wengine juu ghorofani na wote hawa wanakuja kutokana na uhakika wa kazi za Mungu tunazofanya. Uwazi: Kuna madai kuwa katika huduma yako ya uponyaji, unawalipisha watu fedha nyingi ili tu kukuona, je, madai haya yana ukweli? Nabii Suguye: Siwezi kukanusha hilo, ni kweli huwa tunalazimika kufanya hivyo kwa sababu ya gharama mbalimbali za uendeshaji wa huduma hii. Kuna fomu, wino, kalamu na wengine wanahitaji malazi, tuna nyumba maalum ya kulala kwa watu wenye kuhitaji huduma hii ambao wanatoka mikoani. Sisi hatulazi watu kanisani hivyo tunalazimika kuwatafutia huduma hiyo nje ya kanisa. Pia kuna wahudumu wanaonisaidia, hayo yote yanahitaji fedha ndiyo maana tunawaomba watu wanaohitaji maombi kulipa sadaka kiasi fulani. Hili la sadaka siyo agizo langu ni la Mungu mwenyewe na makanisa mengi duniani yanafanya hivyo.

 

Katika hili, watu watakubaliana na mimi kuwa katika kuwahudumia watu wa Mungu, ndiyo maana kuna makanisa yana hospitali na shule kwa sababu ya sadaka wanazotoa waumini wao. Na sisi ndiyo hivyohivyo, tuna shule ambayo tuliianzisha hata kabla sijawa mchungaji. Pia nina televisheni ya WRM ambayo kazi Suguye Nabii afungukia kanisa kutumia ushirikina kuvuta waumini
yake kubwa ni kutangaza neno la Mungu na hivi sasa nimekuwa nikipata mialiko hata kutoka nje ya nchi. Kwa hapa nyumbani nitafanya mkutano mkubwa wa kumuombea Rais John Magufuli na nchi yetu ili amani idumu kati ya Septemba 27 hadi Oktoba Mosi, mwaka huu katika Viwanja vya Hali ya Hewa, BananaUkonga (Dar) na watu wa dini zote ninawakaribisha. Uwazi: Watumishi wengi wanatumia nguvu za giza kuvuta waumini na kuwa nao wengi, je, hili likoje? Nabii Suguye: Mazingira ya Afrika yamewajenga watu wetu katika kuamini mambo hayo tangu wanazaliwa ambapo wapo wengine ambao akizaliwa tu hufungwa hirizi.

 

Kwa hiyo ukuaji wetu wote tumejengwa katika kuona kwamba nguvu za giza ndizo zenye uwezo kuliko Mungu aliyetuumba. Kwa hiyo kwa msingi huo, kila anayeonekana ana nguvu ya Mungu, anaonekana anatumia ushirikina kuvuta waumini kwa sababu ya msingi huo wa kuamini kwenye ushirikina. Lakini kwa upande wangu mimi situmii nguvu za giza kwa sababu chimbuko langu na kulelewa kwangu ni chini ya kanisa na kama siyo kuwa mtumishi kama nilivyo sasa, huko nyuma nilikuwa niwe padri. Maisha yangu yote nimelelewa kwenye misingi ya kumjua Mungu aliye hai. Sikuwahi kuona familia yangu ikihangaika na nguvu za giza pamoja na kwamba ni kweli zilikuwepo. Hivyo kwangu mimi siamini kama nguvu za giza zina

 

weza kuleta watu kanisani lakini naamini nguvu ya Yesu inaweza kufanya yote na kushinda nguvu nyingine yoyote kwa sababu yeye ndiye mwenye mvuto namba moja na mahali popote alipokuwepo Yesu alipokuwa angali nasi kabla ya kuteswa, kufa na kupaa kwenda kwa Baba alikuwa na mvuto wa aina yake.

 

Popote alipokuwa, maelfu ya watu walikusanyika na kukanyagana. Uwazi: Viongozi wengi wa makanisa ya kiroho wanaishi maisha ya kitajiri, lakini waumini wao wana maisha ya tabu sana na wakati mwingine hata sadaka wanaitafuta wiki nzima, kwa nini inakuwa hivyo? Nabii Suguye: Inategemea na mtumishi husika anaamini nini? Siyo wote ni matajiri, kuna watumishi wengine wa Mungu wanaishi maisha ya ufukara kabisa. Wapo wanaoishi maisha ya kati na wapo wa maisha ya juu au ya kifahari. Mimi ninaishi maisha ya kawaida kabisa.

 

Kuna wanaoamini kuwa ukiitwa kumtumikia Mungu utakuwa na maisha ya kawaida, lakini ukweli ni kwamba Mungu siyo wa kawaida. Unajua Mungu yupo mbinguni, lakini maandiko matakatifu yanatuambia kwamba kule mbinguni barabara zake zimepambwa kwa dhahabu na lulu safi, kiti cha Mungu cha enzi kimefunikwa na utukufu mkubwa wa kila aina ya madini. Kwa hiyo Mungu kama mfalme mwenyewe kwenye utawala wake, ana vitu vingi sana, tena vizuri na ana utajiri mwingi sana, kwa hiyo walio kwenye ufalme wake, lazima awafanikishe, lazima waishi vizuri. Kama mimi nitakuwa na maisha mabaya, sitakuwa na tofauti na mganga wa kienyeji.

Kwa Mungu, mtumishi wake kuishi maisha mazuri, mimi ninaona ni jambo la kawaida. Muumini kuishi maisha ya chini inategemea ni kwa namna gani anavyomwamini yule mtumishi anayemuhubiria. Kama unaniamini mimi juu ya mahubiri yangu, ni lazima na wewe ufanikiwe. Nisingependa kuwazungumzia watumishi wengine kwa sababu tunatofautiana katika kuingia kwenye bahari na kuvua samaki. Uwazi: Kuna baadhi ya waumini wanatangaza kufufua watu waliokufa, je, wewe unaweza kumfufua mtu aliyekufa? Nabii Suguye: Siyo mimi ninayefufua, Yesu Kristo ndiye anayefufua. Uwazi: Asante kwa mahojiano na tunashukuru kwa ushirikiano wako. Nabii Suguye: Nami ninashukuru, naomba niwakaribishe wote kwenye nyumba ya Mungu kuanzia Ijumaa na Jumamosi kwa ajili ya maombi kisha ibada kubwa ya Jumapili ili kushuhudia miujiza ya Mungu.

MAKALA: SIFAEL PAUL, DAR

Leave A Reply