The House of Favourite Newspapers

Nacte yatoa taratibu za uendeshaji wa mafunzo ya ufundi nchini

0

Kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Dkt.Adolf  Rutayuga akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari hawapo (pichani) wakati alipokuwa akiongea nao makao makuu ya ofisi hizo yaliyopo Mikocheni  jijini Dar es Salaam, kuhusiana na  maamuzi mbalimbali yaliyofanywa  na baraza hilo katika kuratibu uendeshaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi nchini. Kushoto ni Mkurugenzi wa Ukaguzi na ufuatiliaji wa Ubora wa Mafunzo wa (NACTE) Agnes Ponera na Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa  Baraza hilo ,Alex Nkondola. 
Kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Dkt.Adolf  Rutayuga akiandika pointi muhimu wakati wa  maswali alipokuwa akiulizwa na waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa mkutano uliohusu maamuzi mbalimbali yaliyofanywa  na  baraza hilo katika kuratibu uendeshaji wa mafunzo ya ufundi nchini. Kushoto ni Mgurugenzi wa Ukaguzi na ufuatiliaji wa Ubora wa Mafunzo wa (NACTE) Agnes Ponera na Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa  Baraza hilo ,Alex Nkondola.
Kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Dkt.Adolf  Rutayuga(katikati)akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari hawapo (pichani) wakati alipokuwa akiongea nao katika  makao makuu ya ofisi hizo Mikocheni  jijini Dar es Salaam, kuhusiana na  maamuzi mbalimbali yaliyofanywa  na baraza hilo katika kuratibu uendeshaji wa mafunzo ya ufundi nchini. Kushoto ni Mgurugenzi wa Ukaguzi na ufuatiliaji wa Ubora wa Mafunzo wa (NACTE) Agnes Ponera na Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa  Baraza hilo ,Alex Nkondola(kulia) 
Kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Dkt.Adolf  Rutayuga (Kulia)akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari , wakati alipokuwa akiongea nao makao makuu ya ofisi hizo Mikocheni  jijini Dar es Salaam, kuhusiana na  maamuzi mbalimbali yaliyofanywa  baraza hilo katika kuratibu uendeshaji wa mafunzo ya ufundi nchini. Kushoto ni Mgurugenzi wa Ukaguzi na ufuatiliaji wa Ubora wa Mafunzo wa (NACTE) Agnes Ponera na Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa Baraza hilo ,Alex Nkondola(kulia) Baadhi ya wakurugenzi wa  Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) wakimsikilza kwa makini Kaimu katibu mtendaji wa Baraza hilo, Dr.Adolf  Rutayunga wakati alipokuwa akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari hawapo ( pichani) jijini Dar es Salaam, juu ya maamuzi mbalimbali yaliyofanywa na  baraza hilo katika kuratibu uendeshaji mafunzo ya ufundi nchini.
Mmoja wa waandishi wa habari kutoka kituo cha TV1 Gervas Charles akiuliza swali  wakati wa mkutano wao na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi uliofanyika jijini Dar es Salaam,Uliohusu  maamuzi mbalimbali yaliyofanywa na  baraza hilo katika kuratibu uendeshaji wa mafunzo ya ufundi nchini. 
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza  Kaimu Katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Dkt.Adolf  Rutayuga wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam,juu ya maamuzi mbalimbali yaliyofanywa na  baraza hilo katika kuratibu uendeshaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi nchini. 
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) leo limetoa taarifa ya maamuzi mbalimbali ambayo limefanya kuhusiana na taratibu za uendeshaji wa mafunzo ya ufundi nchini.
Akiongea na waandishi wa habari Kaimu katibu Mtendaji wa baraza hilo Dkt. Adolf Rutayuga alisema wamebainisha mambo mbalimbali yanayohusiana na uendeshaji wa elimu ya ufundi nchini na masuala mbalimbali ya uboreshaji wa elimu hii na masuala ambayo yamebainishwa katika taarifa hiyo ni taratibu za usajili wa Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Ufundi,
Ithibati ya Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Ufundi,mitaala iliyoidhinishwa kutumika katika kutoa elimu ya mafunzo ya ufundi,Utambuzi wa idara zinazotoa kozi mpya,usajili wa walimu, Kuongezwa kwa Muda wa Usajili wa Wanafunzi Wanaomba Kujiunga katika Vyuo na Taasisi za Ufundi katika Mwaka wa Masomo 2015/2016 na Kufungua Vyuo na Taasisi za Elimu ya Ufundi 2015/2016.

Maamuzi ambayo yamefanyika yanafafanuliwa zaidi kama ifuatavyo:

1. Usajili wa Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Ufundi
Kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Na. 9 ya mwaka 1997) na Kanuni za Usajili Na. 13 za mwaka 2001, vyuo na taasisi za serikali na zisizo za serikali zinazotoa elimu na mafunzo ya ufundi zinatakiwa kusajiliwa ili ziweze kuendesha mafunzo. Usajili unalenga kuhakikisha kuwa chuo au taasisi ya elimu na mafunzo ya ufundi imeanzishwa kisheria na ina uwezo, nyenzo na rasilimali za kutosha kuwezesha kutoa mafunzo yenye ubora.

Baraza katika kikao chake cha 57 liliidhinisha usajili wa kudumu kwa vyuo na taasisi zipatazo 143 na usajili wa muda kwa vyuo na taasisi 102 na kufanya hadi sasa kufikisha idadi ya vyuo vilivyosajiliwa na Baraza kuwa 567 (Jedwali Na. 1). Baraza linapenda kuukumbusha umma wa Tanzania kusoma katika vyuo na taasisi ambazo zimesajiliwa ambazo zimetimiza masharti na vigezo vya utoaji elimu ili kupata elimu bora. Baraza pia linawataka wale wanaoendesha vyuo kiholela bila usajili kuacha tabia hiyo mara moja na kuchukua hatua kufuata taratibu za kusajili vyuo/ taasisi hizo kwa mujibu wa sheria.

2.Ithibati ya Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Ufundi
Baraza pia lina mamlaka ya kutoa ithibati kwa taasisi na vyuo kwa mujibu wa sheria ya Baraza na Kanuni za Ithibati za mwaka 2001. Ithibati hutolewa kwa vyuo vyenye usajili wa kudumu na kutimiza vigezo vya ithibati. Ithibati inahusisha masuala mbalimbali ikiwemo uongozi na utawala wa chuo/taasisi, mpango wa kudhibiti na kusimamia ubora wa mafunzo pamoja na tathmini ya utendaji wa chuo. Katika ithibati Baraza huangalia pia uwezo wa taasisi/chuo wa kuendesha programu za mafunzo kwa viwango vya ubora unaokubalika kimataifa na kimataifa.

Hivyo basi katika kikao chake cha 57 Baraza lilitoa ithibati kwa vyuo na taasisi 27 na kufanya vyuo na taasisi zenye ithibati kufikia 124 (Jedwali Na. 2). Baraza linapenda kutumia nafasi hii kuvitaka vyuo vyenye Usajili wa kudumu kukamilisha vigezo vya ithibati ili kuweza kufikia ngazi ya ithibati ambayo ni ya juu katika utoaji wa mafunzo katika vyuo vya ufundi.

3. Mitaala Iliyoidhinishwa Kutumika Katika Kutoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Mojawapo ya masharti ya usajili na ithibati ni chuo au taasisi ya elimu na mafunzo ya ufundi kuwa na mitaala iliyoidhinishwa na Baraza. Baraza huratibu uandaaji wa mitaala inayozingatia umahiri kulingana na mahitaji ya soko la ajira na muundo wa tuzo (NTA) ambao unatoa taarifa sahihi juu ya madhumuni na matarajio ya elimu na mafunzo. Kwa vyuo na taasisi zisizo na uwezo wa kuandaa mitaala yake, Baraza limechukua hatua ya kuandaa baadhi ya mitaala ya kitaifa kwa mujibu wa kifungu Na.11 cha Sheria ya NACTE.

Baraza katika kikao chake cha 57 kiliidhinisha mitaala 169 inayozingatia umahiri kutumika katika ufundishaji wa taaluma mbalimbali zitolewazo vyuo na taasisi za ufundi nchini na kufanya jumla ya mitaala ambayo tayari imeidhinishwa kutumika katika vyuo na taasisi za ufundi kufikia 512 (Jedwali Na. 3). Baraza lingependa kuwaomba wananchi kutokusoma katika kozi yoyote itolewayo na chuo au taasisi ya ufundi ambayo haina mtaala ulioidhinishwa na Baraza.

4. Utambuzi wa Idara Zinatoa Kozi Mpya

Baraza pia lina mamlaka ya kuidhinisha Kozi yoyote mpya ambayo chuo/taasisi inataka kutoa ili kuhakikisha kuwa idara itakayotoa mafunzo hayo imefikia vigezo vya utoaji elimu bora kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Baraza za Ithibati na Utambuzi wa Idara za 2001.

Katika kikao cha 57 Baraza lilitoa idhini kwa idara 91 kutoka vyuo na taasisi mbalimbali kutoa kuanzisha kozi mpya 62 (Jedwali Na. 4). Tunawaomba wananchi wanaotaka kupata elimu kusoma katika kozi ambazo zimepitishwa na Baraza ili waweze kupata elimu bora na kutambulika kitaifa na kimataifa.
5. Usajili wa Walimu

Baraza pia linatoa usajili kwa walimu wanaofundisha katika vyuo na taasisi za elimu ya ufundi ili kuhakikisha kuwa vyuo na taasisi za elimu ya ufundi zinakuwa na walimu wenye sifa stahiki na wenye uwezo wa kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

Katika kikao cha Baraza cha 57 walimu 748 walisajiliwa na kufikisha idadi ya walimu 3325 waliosajiliwa wanaofundisha katika vyuo na taasisi za elimu ya ufundi. Baraza linapenda kuwakumbusha viongozi wa vyuo na taasisi za elimu ya ufundi kuhakikisha kuwa walimu wanaofundisha katika vyuo/taasisi za elimu ya ufundi wana sifa stahiki na waliosajiliwa na Baraza.

6. Kuongezwa kwa Muda wa Usajili wa Wanafunzi Wanaomba Kujiunga katika Vyuo na Taasisi za Ufundi katika Mwaka wa Masomo 2015/2016

Baraza linapenda kuutaarifu umma kuwa muda wa kufanya udahili kwa wanafunzi wanaoomba kujiunga na mafunzo kwa njia ya kielectronic kupitia mfumo wa udahili wa pamoja (CAS) umeongezwa mpaka tarehe 16/10/2015 kwa wanafunzi wenye stashahada wanaotaka kujiunga katika ngazi ya shahada katika elimu ya juu na wale wanaotaka kujiunga katika ngazi za astashahada na stashahada katika kozi za afya. Hivyo Baraza linawaomba wale ambao hawajaomba na wana nia ya kujiunga na mafunzo katika mwaka huu wa masomo watumie nafasi hii kutuma maombi yao sasa.

7.Kufungua Vyuo na Taasisi za Elimu ya Ufundi 2015/2016
Baraza linapenda kuwataarifu viongozi na wamiliki wa vyuo na taasisi za elimu ya ufundi kufungua vyuo na taasisi zao mwezi Novemba 2015 ili kuruhusu wanafunzi kupata fursa nzuri ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika tarehe 25/10/2015. Aidha, kwa vyuo na taasisi ambazo zilishafunguliwa na kuanza masomo, watatakiwa kufunga wiki mbili katika kipindi cha uchaguzi ili kutoa nafasi kwa kila mwanafunzi kushiriki katika uchaguzi na kupiga kura katika eneo alilojiandikisha.

 

Leave A Reply