The House of Favourite Newspapers

Naibu Waziri Aipongeza Dcb Kwa Kuwainua Wajasiriamali

0
Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis ( wa pili kushoto) akikabidhi cheti cha shukurani kwa Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Biashara ya DCB, Zacharia Kapama katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoandaliwa na Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam hiyo ni kwa kutambua udhamini wa DCB kwa kufanikisha hafla hiyo jijini humo jana. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng`wilabuzu Ludigija, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Dar es Salaam, Tabu Shaibu na Rais Mstaafu wa Vicoba Tanzania, Devotha Likokola.

 

Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Bi. Mwanaidi Ali Khamis  ameipongeza Benki ya DCB kwa jitihada inazoonyesha katika kutoa elimu ya biashara na kifedha kwa wanawake wajasiliamali jambo litakalowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Naibu waziri aliyasema hayo katika hafla ya Siku ya Wanawake iliyoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa udhamini mkuu wa DCB  jijini humo jana huku akiitaka  benki hiyo kutochoka katika kutoa elimu juu ya uendeshaji mzuri wa biashara pamoja na masuala ya masoko.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Dar es Salaam, Tabu Shaibu ( kushoto ) akipokea fomu ya kufungua akaunti katika Benki ya Biashara ya DCB kutoka kwa Mkuu wa Kitengo Serikali za Mitaa wa benki hiyo, Francisca Mushi wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

 

“Hafla kama hizi ni muhimu kwa wajasiriamali kwani zinawasaidia kubadilishana uzoefu mlionao katika kufanya biashara, kujenga mtandao wa kibiashara, kubadilishana ujuzi katika masuala ya kiubunifu na pia kujadili fursa mbalimbali za kibiashara zilizopo katika maeneo tofauti.

 

“Ninayo Imani kubwa na wajasiriamali wetu kwa jitihada zinazofanywa na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hamuwezi kutuangusha, wanawake mnapaswa kujiamini ili pia kusaidia juhudi za Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutoa fursa mbalimbali kwa wanawake zikiwemo fursa za uongozi”, akasema.

Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Biashara ya DCB, Zacharia Kapama akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kudhaminiwa na benki hiyo.

 

“Rais wetu ni msikivu, anajali, mtetezi wetu, mpenda haki, muadilifu na mwenye maono ya mbali, tushikamane naye tuungane naye mkono kwa yote anayofanya kwani anahangaika sana ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo”, alisema naibu waziri.

 

Pamoja na hayo akatoa rai kwa wanawake hao kurejesha mikopo wanayopewa na halmashauri kwa wakati ili iweze kuwasaidia wananchi wengine ili kwa pamoja kujikwamua kiuchumi.

… Mwanaidi Ali Khamis ( wa pili kulia ), akisindikizwa na viongozi mbalimbali waliokuwa katika hafla hiyo.

 

“Safari ya kuelekea uchumi wa viwanda ni ya pamoja, kwa kutegemea mfuko wa halmashauri ya jiji pekee hatuwezi kufikia malengo, tukishirikiana kwa pamoja na wadau wa maendeleo tutapiga hatua kubwa”, alisema.

 

Akizungumza katikla hafla hiyo, Mkurugenzi wa Biashara wa DCB, Zacharia Kapama alisema kwa kutambua umuhimu wa sekta ya wajasiriamali walio katika makundi ya vijana wanawake  benki hiyo imetoa mikopo ya Zaidi ya shs bilioni 500 kwa kipindi cha miaka 20.

 

“Kwa Zaidi ya miaka 20 sasa tokea benki yetu imeanzishwa tumekuwa mstari wa mbele katika kusaidia wanawake, vijana na makundi maalumu kupitia halmashauri zote za Dar es Salaam.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Biashara ya DCB pamoja na wanawake wajasiriamali wakiselebuka wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoandaliwa na Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam na kudhaminiwa na DCB.

 

“Kwa kipindi chote cha miaka 20 ya uendeshaji, jukumu mama la benki yetu limeendelea kuwa ni kutoa huduma bora za kifedha huku ikijikita katika kutengeneza miradi ya kupunguza umasikini na kuendeleza jamii”, alisema.

 

Aidha alisema sambamba na hayo DCB kupitia asasi yake ya DCB Foundation ambayo lengo lake kuu ni kuwajengea uwezo wananchi hususan wajasiriamali na kuwapa mitaji kwa ajili ya kujiinua kiuchumi, imeanza kutoa mafunzo kwenye makundi mbalimbali yenye lengo la kutoa elimu ya jinsi ya kuanzisha, kukuza na kuendeleza biashara.

Mwanaidi Ali Khamis ( wa pili kushoto) akimkabidhi zawadi ya shukrani kutoka Benki ya Biashara ya DCB na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng`wilabuzu Ludigija wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuza Ludigija alisema kupitia uwezeshaji unaofanywa na Jiji la Dar es Salaam hana shaka wataenda kupata wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa kutokea katika makundi ya wajasiriamali wanawake.

 

“Kupitia maadhimisho haya tuhakikishe pia tunapeana elimu na kukumbushana jinsi ya kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, ni kwa jinsi hiyo tunaweza kufanikisha jitihada zetu za kujiinua kiuchumi”, alisema mkuu huyo wa wilaya.

Leave A Reply