The House of Favourite Newspapers

Namna ya Kukabiliana na Tatizo la Kutopevusha Mayai!

0

AFYA DK. CHALE

MWANAMKE kutopevusha mayai kitaalamu huitwa Ovulatory Dysfunction . Ni hali ambayo si ya kawaida inayoweza kumtokea mwanamke yeyote aliye katika umri wa kuzaa. Mwanamke mwenye tatizo hili anaweza kupata upevushaji isivyo kawaida. Mfano mwezi mmoja au miwili mwanamke asipate, akaja kupata mwezi unaofuata au akawa anarukaruka miezi.

Wakati mwingine anakaa mwezi mzima bila kupata. Mwanamke huyu pia hata mzunguko wake wa hedhi siyo wa kawaida, unavurugikavurugika na miezi mingine hapati au anaweza kufunga hedhi hata miezi miwili au zaidi pasipo kuwa na ujauzito. Katika hali ya kawaida ya mwanamke anapata ute wa uzazi ndiyo unaoashiria Ovulation.

Ute huu hutokea vipindi vya katikati ya mzunguko. Ute wa uzazi upo wa aina tatu, kwanza ni ute mwepesi,  halafu ute wa kuvutika na mwisho ni ute mzito. Ute wa uzazi ndiyo unaoashiria yai limetoka na linasubiri kurutubishwa. Utokaji wa ute huu wingi wake unatofautiana kati ya mwanamke na mwanamke, wengine hupata mwingi na wengine kidogo kiasi kwamba hauonekani.

CHANZO CHA TATIZO

Mwanamke mwenye tatizo hili kwa muda mrefu daima huwa sugu na hata umri wake unakuwa umekwenda, wengi wenye tatizo hili sugu huwa na umri kati ya miaka 35 hadi 45 na wanakuwa na historia ya kutafuta mtoto kwa muda mrefu. 

Chanzo kikuu cha tatizo hili linaweza kuwa ni uwepo wa vivimbe katika vifuko vya mayai au Polycystic Ovarian Syndrome, matatizo katika mfumo wa homoni uitwao Hyperprolactinemia, matatizo katika mfumo wa kichwa yaitwayo Hypothalamic Dysfunction ambapo mwanamke pia hupata tatizo la kupoteza siku zake za hedhi pasipo kuwa mjamzito na tatizo la kupoteza kabisa uwezo wa upevushaji.

Wanawake wenye tatizo la kutopata Ovulation au upevushaji wanaweza kupata damu ya hedhi kama kawaida kila mwezi au wanaweza kupoteza
kabisa kupata damu ya hedhi hata zaidi ya miezi mitatu. Kwa hiyo siyo kila mwanamke anayepata damu ya hedhi ana uwezo wa kupata ujauzito ingawa wengi wenye tatizo hili hupoteza siku zao au siku za hedhi zinavurugika, hazieleweki na hazina mpangilio maalumu.

DALILI ZA TATIZO

Mwanamke mwenye tatizo la kutopevusha mayai kwanza kabisa hapati ujauzito  na analalamikia tatizo hilo, anakuwa katika harakati za kutafuta mtoto kwa zaidi ya mwaka, wakati mwingine anakuwa na historia ya kuwa na mtoto au alishapata ujauzito ukatoka au hana kabisa historia.

Wapo wengine wana historia ya kutumia dawa za kuzuia mimba kwa muda mrefu, walishawahi kupata magonjwa ya viungo vya uzazi kama kutokwa na uchafu ukeni na muwasho, maumivu ya chini ya tumbo kwa muda mrefu na historia ya kupoteza hali ya kujisikia vizuri wakati wa tendo la ndoa.

Kama tulivyoona hapo awali, tatizo la kutopevusha mayai hutokea zaidi kwa wanawake ambao hawapati siku zao za hedhi pasipo kuwa wajawazito. Dalili nyingine ni mwanamke kuumwa matiti mara kwa mara na wakati mwingine yanatoa maji, maumivu chini ya tumbo mara kwa mara na kuhisi tumbo linajaa gesi na hali ya kukosa raha au akili kutokaa sawa.

UCHUNGUZI

Mtu wa kwanza katika hili ni mwanamke mwenyewe baada ya kugundua dalili hizo tulizozieleza na amekuwa akitafuta mtoto kwa muda mrefu. Unashauriwa umuone daktari wa masuala ya uzazi kwa uchunguzi wa kina ambapo utapewa maelekezo ya kujichunguza mwenyewe nyumbani kwa kujipima joto la mwili na vipimo vya mkojo. Vipimo vya damu vitafanyika katika maabara.

Kipimo cha joto la mwili hupimwa asubuhi ambapo kipima joto utakiweka kinywani kwa dakika tatu na kama upevushaji upo, basi joto la mwili litaongezeka kwa nyuzi 0.5 zaidi ya lile la kawaida, hii utapima kila siku kuanzia unapomaliza hedhi hadi unapoanza tena.

Kipimo kingine utakachojipima mwenyewe ni mkojo kwa kipimo kiitwacho Ovulation Prediction kitu ambacho hupima homoni ya LH inayoashiria yai limetokea, kama kipimo hiki kikiwa hakionyeshi maana yake hujapata Ovulation. Vipimo
vingine ni Ultrasound , itatumika kuona endapo kuna maambukizo katika viungo vya uzazi, itasaidia kuhesabu mayai na ujazo wa vifuko vya mayai. Vipimo vya damu vitatumika kuangalia viwango vya homoni.

MATIBABU NA USHAURI Tiba itatolewa baada ya uchunguzi wa kina. Tiba nyingine ni baada ya uchunguzi wa kina, kutibu vyanzo vya matatizo. Hivyo tiba inaweza kuwa ni dawa au upasuaji.

SIMU: +255713350084

Tazama Daktari Mwenye Uwezo wa Ajabu wa Kupandikiza Mishipa ya Damu Kwenye Moyo kwa Dakika 5

Leave A Reply