The House of Favourite Newspapers

Nandy Afunga Mwaka Kibabe

0

MALKIA wa Bongo Fleva Afrika Mashariki na Kati, Faustina Charles almaarufu Nandy amefunga mwaka 2021 kibabe kwa mafanikio makubwa.


Hii ni baada ya kufanikiwa
kufikisha jumla ya streams (wasikilizaji) milioni 30 kwenye mtandao mmoja pekee wa
Boomplay.


Hii ni sehemu ya mafanikio
makubwa kwa Nandy au The African Princess kuwa miongoni mwa wasanii wachache ambao wamefanikiwa kufikisha idadi hiyo ya streams au wamezidi zaidi ya hapo.


Nandy ni miongoni mwa
wanamuziki wakubwa waliofanya vizuri akitwaa Tuzo ya Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki 2021 huku akiwa ni miongoni mwa wasanii wachache wa kike wenye ushawishi na mashabiki wengi kwenye soko la muziki Afrika Mashariki kwa jumla.

 

Ni msanii ambaye amekuzwa kwenye misingi ya kimuziki tangu akiwa binti mdogo, wakati huo akiimba kwaya kwenye makanisa ambayo alikuwa akihudhuria ibada mbalimbali.

 

Amepitia katika Nyumba ya Vipaji ya Tanzania House of Talents (THT) ambapo alijifunza mambo mengi kuhusu muziki, jambo ambalo limemfanya kuwa Nandy huyu wa sasa ambaye kila jukwaa amekuwa akisikika.


Nandy alianza kusikika mwaka
2016 baada ya kuibuka mshindi wa pili katika shindano la kuimba lililoandaliwa na Tecno na mwaka huohuo aliachia wimbo wake wa Nagusagusa uliomtambulisha vyema.


Mwaka 2017 aliachia Wimbo
wa One Day ambao ulimpa nafasi ya kushinda Tuzo za AFRIMMA kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki. Pia amewahi kutamba na nyimbo kama Kivuruge, Ninogeshe, Hallelujah, Acha Lizame, Leo Leo, Nimekuzoea na nyingine nyingi.

Hadi sasa, Nandy amefanikiwa kuachia albam moja ya The African Princess huku akiachia EP mbili za Taste
EP na Wanibariki.
Idadi ya nyimbo zote hizo ndiyo inakamilisha jumla ya streams milioni 30 katika app
ya Boomplay. Usiku wa kuamkia
Desemba 13, 2021, Nandy alifanikiwa kushinda Tuzo za Afrimma katika kipengele cha Msanii Bora Afrika Mashariki.


Endelea kusikiliza ngoma yake
inayotamba kwa sasa ‘Party’ ambayo amemshirikisha Billnass

Leave A Reply