The House of Favourite Newspapers

NANDY APINDUA MEZA MDOGOMDOGO

FEBRUARI 9, 2017 bado itaendelea kubaki kama kumbukumbu katika kichwa cha mwanadada mrembo anayetikisa Bongo Flevani, Faustina Charles Mfinanga anayetumia majina ya Nandy au The African Princess anapokuwa stejini. Hiyo ndiyo siku iliyofungua rasmi safari yake ya muziki baada ya kuwa mshindi wa pili katika mashindano ya kuimba ya Tecno Own the Stage yaliyofanyika nchini Nigeria na kujizolea kitita cha zaidi ya shilingi milioni 35 za Kibongo.  Baada ya kuianzisha safari hiyo ni kama gari lililowekwa mafuta full tank kwani amekuwa akifanya poa na kutingisha tasnia ya muziki Afrika Mashariki kiasi cha kubatizwa majina mengi kama vile Sauti ya Asali na The African Princess. Leo hii Nandy yule aliyezaliwa 1992 kule Moshi mkoani Kilimanjaro, aliyekuwa akipiga shoo na B Band chini ya Banana Zorro miaka ya 2010 si yule tena.

Kuna utofauti mkubwa wa Nandy yule aliyekuwa Jumba la Kuibua Vipaji Tanzania (THT) kipindi hicho akiwa na ngoma ya kawaida sana ya Bye (My Ex). Over Ze Weekend limekuandalia baadhi tu ya vitu ambavyo vimemfanya Nandy kuwa juu na wa tofauti ambapo wasanii wengi wa kike wameshindwa kupitia nyayo hizo hivyo kupanga foleni nyuma yake.

KUMILIKI STUDIO

Ni moja ya mafanikio makubwa kwa Nandy ambapo asilimia kubwa ya nyimbo zake anazipikia katika studio yake aliyoiita African Princess. Bidada huyu anasema lengo hasa la kumiliki studio nyumbani kwake ni kurahisisha muziki wake.

“Siyo kama studio za watu wanakaa foleni nje, hapana hii kwa ajili yangu na wale nitakaokuwa ninawashikirikisha kwenye nyimbo zangu. Lakini pia kwa hapo baadaye tutaangalia utaratibu wa wasanii wengine,” anasema Nandy. Studio hiyo kwa sasa inasimamiwa na Prodyuza Kimambo.

ALBAM

Hadi sasa Nandy anamiliki albam moja inayokwenda kwa jina la African Princess ikiwa na nyimbo 13 ambazo miongoni mwake ni One Day, Wasikudanganye, Kivuruge, Subalkheri, Njiwa, Aibu, Ninogeshe na Nagusagusa. Albam hii aliizindua rasmi usiku wa Novemba 9, 2018 na kuwa msanii wa pili wa kike kuzindua albam akiwa nyuma ya Vanessa Mdee ‘Vee-Money’ ambaye aliizindua albam yake ya Money Mondays.

MFANYA-BIASHARA

Kitu kingine kinachomfanya kuendelea kuwa juu ni kutokana na kujihusisha katika biashara ambapo kwa sasa anamiliki kampuni ya kutengeneza nguo ya Nandi African Prints na Nandy Beauty Products ambayo ameingia ubia na kampuni ya vipodozi ya Grace akiingiza matolea mawili ya Nandy Beauty Soap na Nandy Petroleum Jelly.

TUZO

Nandy anashikilia tuzo kadhaa ambazo ni Marantha na Dear za nchini Kenya kupitia Cover aliyofanya kwenye wimbo wa Injili wa msanii Angel Benard wa Nikumbushe Wema Wako. Tuzo nyingine kubwa ni ya AFRIMMA ambayo aliipata mwaka 2017 katika kipe-ngele cha Msanii Bora wa Kike Afrika Mash-ariki.

TAMT-HILIA YUMO

Licha ya kutikisa kote huko, Nandy bado ameonesha kipaji chake katika uigizaji ambapo kwa sasa anashiriki Tamthiliya ya Huba inayorushwa na Maisha Magic Bongo kupitia King’amuzi cha Dstv.

TAMASHA

Ameonesha ukomavu kwenye gemu ndani ya muda mfupi baada ya kuandaa tamasha lake mwenyewe aliloliita Nandy Festival ambalo lilifanyika Sikukuu ya Idd Mosi ndani ya Uwanja wa Mpira wa Nelson Mandela uliopo Sumbawanga.

Katika usiku huo, Nandy alikuwa msanii wa kike aliyeshindana na wasanii wengine waliokuwa wakifanya shoo za viwanjani ambao ni Diamond Platnumz aliyefanya Uwanja wa Mpira wa Kahama na Harmonize aliyefanya Uwanja wa Mpira wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. Huyo ndiye Nandy ambaye anapindua meza mdogomdogo akiwapangua wakongwe wa kike mmoja baada ya mwingine!

Comments are closed.