The House of Favourite Newspapers

Nas B Akiri Kuporomoka Kisa Menejimenti!

Nas BAMINA ni msichana mrembo anayeishi Temeke Mikoroshini, kuhusu maisha yake ni msumari na nyundo, wazazi wote masikini, walijiganga ganga ili aende shuleni, wakazichangachanga wakakubali hata madeni…

 

Wengi mtakuwa mnakumbuka hii mistari kutoka kwenye ngoma iitwayo Ng’ombe wa Masikini ya mwanamuziki Nas B aliomshirikisha 20 Parcent.

Wimbo huu ulikuwa ni miongoni mwa nyimbo zilizofanya vizuri mwishoni mwa miaka ya 2000 na kumtambulisha vyema kijana huyu Nas B, mtoto wa Magomeni, kwenye ulimwengu wa Muziki wa Bongo Fleva.Nyimbo nyingine ambazo alizowahi kutamba nazo ni pamoja na Dua la Kuku, Analia Shida na nyingine nyingi.

 

Hata hivyo baada ya kutikisa kipindi kile, kwa sasa Nas amepotea. Mara kadhaa amejaribu kurudi lakini hafiki pale ambapo anahitaji kufika au alipokuwa. Nini sababu inayomfanya asitusue zaidi? Anafanya nini kwa sasa? Vipi kuhusu ndoto zake zaidi za kimuziki? Msikilize kwenye makala haya;

Risasi: Nas habari za kitambo?

Nas: Poa tu.

Risasi: Umepotea sana mzee.

Nas: Nipo ninakomaa.

Risasi: Mara ya mwisho kama sikosei uliibuka na wimbo uitwao Mbigili, baada ya hapo umeme ukakatika tena, tatizo nini?

Nas: Changamoto tu za muziki, kama unavyofahamu muziki kwa sasa una mambo mengi. Ili uweze kufanikiwa kimuziki kwa sasa ni lazima pia uwe na menejimenti iliyosimama. Kama huna menejimenti ina maana hata hatua zako zitakuwa za kusuasua kwenye muziki.

Risasi: Lakini kuna kipindi ulipoibuka ulisema kwamba una menejimenti?

Nas: Ni kweli nilikuwa

ninamenejimenti, lakini kuna mambo ambayo hayakwenda sawa kwenye menejimenti yangu. Kwa hiyo nikatofautiana nayo na ndiyo sababu hasa iliyonifikisha hapa nilipo kimuziki kwa sasa.

Risasi: Pole sana. Kwa hiyo kwa sasa unajishughulisha na nini zaidi?

Nas: Ni muziki huuhuu. Lakini katika hatua nyingine. Kwa sasa mbali na kuimba mimi ni prodyuza, ninamiliki studio yangu inayoitwa Pamoja Records. Kwa hiyo muda mwingi ninakuwa kwenye studio yangu na ndiyo inanisaidia kuendesha maisha yangu

Risasi: Kuhusu muziki, una ndoto zozote pengine kama ilivyokuwa awali, au ndiyo zilikwisha futika na umebaki ukifanya kama hobi?

Nas: Ndoto zipo. Lakini ndoto huja pia kutokana na hali halisi inavyokuwa inakwenda, kwa hiyo kwa sasa ndoto zangu ni kuendeleza kwanza studio yangu ili niweze kupata studio kubwa ambayo itakuwa na nafasi ya kufanya kazi zaidi na wanamuziki wengi wa ndani na nje ya nchi.

Kisha baada ya hapo ndipo nitarudi kuangazia muziki kwa kiasi kikubwa kama ambavyo ilikuwa hapo nyuma.

Risasi: Ukiwa haupo kwenye ‘mainstream’, nini hasa unajifunza kutoka kwa wanamuziki wanaofanya vizuri?

Nas: Naona kuna ushindani. Ushindani ambao unaleta chachu ya watu kuzidisha juhudi na kukomaa zaidi ili waweze kufika kule ambako wanahitaji kufika kimuziki.

Risasi: Mwanamuziki gani ambaye unavutiwa naye kufanya naye kazi kwa sasa?

Nas: Kiukweli wapo wengi, sijaweza kumfikiria mwanamuziki mmoja kwa sasa kwa sababu sina kazi ambayo inamhusu mwanamuziki fulani. Bila shaka unafahamu kwamba si kila mwanamuziki anahitaji kumshirikisha mtu fulani, wimbo ndiyo unahitaji kumshirikisha mwanamuziki fulani.

Risasi: Una kipi cha kuwashauri wanamuziki ambao wamepotea na wanajaribu kupambana ili warudi kule walikokuwa?

Nas: Wasikate tamaa. Waendelee kupambana ili kuhakikisha wanafikia malengo yao. Kwa sababu muziki una kupanda na kushuka kama zilivyo biashara nyingine.

Risasi: Umefanya kazi kadhaa na 20 Percent, wewe umepotea na yeye amepotea, nini unafikiri nini sababu ya kupotea kwake?

Nas: Sijui kiukweli kuhusu 20 Percent na sihitaji kumzungumzia.

Risasi: Basi sawa ninakushukuru sana kaka, kila la kheri kwenye muziki wako.

Nas: Asante.

Makala: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.