NAUNGA MKONO MWAKYEMBE KUPIGA CHINI ‘KIMOMBO’ MISS TANZANIA

MWAKA 1972, Mwanamitindo Julia Morley ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa shirika linaloratibu mashindano ya Miss Dunia alianzisha kitu kinaitwa ‘Beauty With Purpose’, yaani ‘Urembo kwa Malengo’ kwenye mashindano ya mamiss.  Kwa miaka nenda rudi, Urembo kwa Malengo umekuwa ni moyo wa mashindano ya mamiss sehemu tofautitofauti duniani.

Ndiyo maana hata hapa kwetu katika kila mchakato wa mamiss utaona wanajihusisha kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, kama kufanya kazi za kuosha magari ili walipwe pesa na kupeleka kwa watoto yatima, kulima au kuchangisha fedha kwa ajili ya mahitaji tofauti kwenye jamii.

Inatokana tu na malengo wanayokuwa wamejiwekea katika shindano la wakati huo.Hata hivyo Urembo kwa Malengo mbali na kuwa sehemu ya msaada mkubwa kwa jamii, unaweza kutumika kusapoti na kukuza vilivyo vyetu, kama sekta ya utalii, mambo ya uwekezaji na hata lugha ambayo ndiyo nitaizu

ngumzia hapa zaidi. Namaanisha lugha yetu ya Taifa ya Kiswahili. Ninamu unga mkono Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kama alivyoeleza juzi (Jumamosi) kwenye mashindano ya kumtafuta mrembo wa Tanzania anayekwenda kutuwakilisha kwenye mashindano ya Miss World mwaka huu, ambapo mwanadada kutoka Dar es Salaam, Queen Elizabeth alishinda!

Mwakyembe alisema kwamba kwa muda mrefu lugha ya Kingereza ‘Kimombo’ kimekuwa kikitawala kwenye mashindano ya mamiss, umefika wakati tukipige chini na tukitangaze Kiswahili kimataifa kwa sababu kwa sasa Kiswahili ni lugha ya kimataifa na watu wenye wajibu wa kukitangaza zaidi Kiswahili ni Watanzania wenyewe.

KWELI, KIMOMBO KIPIGWE CHINI!

Ukizungumzia lugha 6,000 zinazozungumzwa zaidi duniani, Kiswahili ni miongoni mwa lugha zilizopo kwenye ‘top 10’, kwa hiyo ni lugha ya kimataifa kwelikweli. Mbali na Kiswahili kuwa lugha yetu ya taifa, ni lugha rasmi inayozungumzwa kwa sasa Afrika Mashariki, lakini kama haitoshi ni lugha rasmi inayozu

ngumzwa kwenye Umoja wa Nchi za Afrika (AU). Sasa kwa nini mamiss wanajichosha na Kizungu! Unaweza kushangaa, wakati Mwakyembe yupo kwenye fainali za shindano hilo alizungumza umuhimu wa mamiss kuzungumza Kiswahili kwenye mashindano hayo na hata mshindi kukizungumza kwenye mashindano ya dunia lakini bado Kimombo kilitawala.

ASILIMIA 80 YA LUGHA ILIYOTUMIKA NI KIMOMBO!

Ukianza kwa ‘ma-mc’ wa shughuli yenyewe, Deogratius Kithama na Hamisa Mobeto, muda mwingi wakiwa jukwaani walikuwa wanatumia Kimombo.

Lakini hata washiriki wenyewe wa shindano la mamiss. Ukitazama walioingia ‘Top 5’, kuanzia mshindi Queen Elizabeth hadi mshindi wa tatu wote walijibu maswali yao kwa lugha ya Kingereza. Ni mshindi wa nne na tano tu ndiyo walijibu kwa lugha ya taifa ya Kiswahili. Lakini hata kwa majaji muda mwingi, jaji mkuu, Devotha Mdachi alikuwa akitangaza matokeo yake au kuzungumza lolote lile kwa Kimombo tu, yaani ilifika hatua mtu unaweza kuhisi upo nchi ya ugenini vile.

KIMOMBO KIKATAMBAA MPAKA KWENYE MUZIKI

Ukija kwenye burudani nako, Kimombo hakikuachwa nyuma. Baadhi ya wanamuziki walioalikwa kuburudisha kwenye shindano hili likiwemo Kundi la Work Malina pamoja na mwanamuziki Ruby, waliimba nyimbo za Kimombo. Ruby alifungua kwa wimbo aliotumia lugha ya Kimombo na alifunga na akapela ya Kimombo!

Binafsi sioni kama ni ufahari kutumia lugha hii kwenye mashindano ya Miss Tanzania au huko kwenye shindano la Miss Dunia kama ambavyo Mwakyembe alisema alipopata nafasi ya kuzungumza mawili matatu. Ufahari ni kuzungumza Kiswahili, lugha yetu mama.

Uzuri ni kwamba kwenye mashindano mengi ya kimataifa ma-miss hupata nafasi ya kuulizwa lugha ambayo wanapenda watumie kujibu maswali, kwa hiyo badala ya Kimombo, Kiswahili kichukue nafasi! Mwisho pongezi ziende kwa mratibu wa mashindano haya, Basila Mwanukuzi,ambaye pia ni Miss Tanzania 1998. Amejitahidi kwa kiasi chake mpaka kufanikisha mashindano haya, kikubwa zile changamoto zote zilizoibuka azitumie kuboresha shindano hili mwaka uja

BONIPHACE NGUMIJE

Toa comment