The House of Favourite Newspapers

Nchemba Afafanua Tozo ya Laini za Simu

0

WAZIRI wa Fedha na Mipango,  Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa ufafanuzi wa baadhi ya tozo alizowasilisha bungeni wakati wa mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22 na kuleta mkanganyiko kwa wananchi ikiwemo makato ya miamala ya simu, kodi ya majengo kwa njia ya Luku na Makato yanayopendekezwa ya mafuta kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

 

Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kupitia Jukwaa la Wahariri (TEF), katika kikao kilichoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

 

Alisema kuwa kodi hizo zimetafsiriwa kinyume na lengo la Serikali, ambapo kwenye kodi ya kuongeza salio mtu akiweka kuanzia Sh. 1000 hadi Sh. 2500, atatozwa shilingi 10, shilingi 2500 hadi 5000 atatozwa Sh. 21, shilingi 50,000 hadi 100,000 atatozwa shilingi 186 na shilingi 100,000 kwenda juu anatozwa shilingi 200 na sio kila siku ni pale anapoweka mudawa maongezi.

 

“Hatujaweka kodi kwenye laini za simu kama ambavyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakichanganya, hata kule Bungeni wanachanganya wanasema sasa kila siku itakuwa inakatwa shilingi 10 mpaka 200 kwa hiyo kama ni 200 kwa siku 30 ni shilingi 6000, halafu hata kama hukuweka fedha, siku ukiweka inakatwa kama nipige tafu, hatukuweka hivyo”, alieleza Dkt. Nchemba.

 

Alibainisha kuwa haimaanishi kwamba shilingi 10 sio mzigo lakini Serikali iliangalia matatizo yaliyopo na kugundua kuwa yanagharimu zaidi, kuliko thamani ya shilingi 10 itakayotozwa kama kodi.

 

Alifafanua kuwa miradi mikubwa inayotekelezwa nchi ukiwemo wa mradi wa Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere ambao unahitaji zaidi ya shilingi trililioni nne na ujenzi wa Reli ya Kisasa unaohitaji zaidi ya shilingi trilioni 20 ili kukamilika, iwapo fedha zote zitategemea mikopo nchi itapitiliza uwezo wa kukopa na kutokukopesheka hivyo ushiriki wa wananchi ni muhimu.

Leave A Reply