Ndege ya Shirika la Emirate A380 Yatua Kwa Dharura Tanzania
Uwanja wa Ndege wa Julius Kambarage Nyerere uliopo Jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Aprili 16, 2023 umepokea Ndege kubwa aina ya Airbus A380 ya Shirika la Ndege Emirates yenye uwezo wa kuchukua Abiria 550 iliyotua kwa dharura ili kuongeza mafuta kwa ajili ya kuendelea na safari.
Ndege hiyo iliyobeba Abiria 514 imetokea Sao Paulo, Brazil kuelekea Dubai imelazimika kukwepa njia yake ya kawaida ya kupitia kwenye anga ya Sudan ambayo kwa sasa imefungwa. Kutokana na kukwepa njia yake ya kawaida safari ya Ndege huyo imekuwa ndefu hivyo kulazimika kutua Tanzania kwa dharura ili kuongeza mafuta yatakayoisaidia kukamilisha safari yake.
Ikumbukwe mnamo mwaka 2018 tukio kama hili lilitokea pale Ndege nyingine ya Airbus A380 kama hii iliposhindwa kutua nchini Mauritius kutokana na hali mbaya ya hewa na badala yake ikatua Dar es salaam ambapo Abiria walilazimika kulazwa Hotelini na kuondoka kesho yake.