The House of Favourite Newspapers

NDOA SIYO UMEME WA LUKU!

OHH mke wangu kila nikirudi anavimba domo, kunipakulia tu shida nikisema hivi visingizio kibao! Heee heeeiyaaaa, utalalama sana mwaka huu, mwanamke wako mwenyewe shida zako uzilete kwangu, inahu?

Shoga leo nimekuja kivingine, nahisi mdomo wangu kama vile umemwagiwa pilipili mbuzi maana si kwa kuchachuka huku, kila mada natamani niongee tu, acha leo nianze na wale wanaume wanaojifanya wameoa kumbe wameoa umeme wa luku, halooo ehhhh, langu kalio mchana naketi kibarazani usiku feni, upo?

Baada ya kukupa udambwidambwi nianze kushusha pumzi na weeeweee! Dume zima unayejua kuwa ukishaoa na kuweka ndani unafikiri kinachofuata ni shoping na kujaza friji kama siyo kuweka umeme wa luku!

Kwanza nataka utambue mwanamke siyo umeme wa luku, ukishaoa basi unaweka ndani na kumtumia kama vocha za shilingi mia tano, utue babu nikutue ennnh! Tena nachukia wanaoendelea kukomalia kuwa mwanamke ni pambo la nyumba! Zamani sawa ila siku hizi mwanamke kuhangaika, mwanamke kusaidiana na mwanaume, akisomesha watoto basi wewe unalisha na kuvalisha watoto, upo?

Utakuta mzee mzima akishaoa basi anaona amemaliza, kila siku atakuwa akiondoka asubuhi kurudi usiku wa manane tena siku nyingine akija ananuka mipombe kama siyo harufu za pafyumu za wanawake, looo! Unafikiri huyo mwanamke kwao hakuwa anakula na kulala? Wazazi wake walishindwa kumgeuza vocha au umeme wa luku kutwa kukaa ndani na kupiga kelele unapoisha?

Badilikeni bwana nyie wanaume mlio ndani ya ndoa, hata wewe ambaye unafikiria kuoa! Labda nilipapase sikio lako kidogo kama ulikuwa hujui, mwanamke anababaika na vitu vidogo sana! Ukijitengea muda wako wa mapumziko ya kazi jaribu kushinda naye karibu, ongea naye mambo yenu ya familia, jaribu kumtoa hata outing, haloooo eeehh ya kisoda bia nitalewa miye!

Siku hizi, wanawake wengi wanafurahia ndoa zao kwa sababu wanaume wao wanajua jinsi ya kuwapetipeti, pamoja na kuwa wanafanya kazi Jumatatu hadi Ijumaa lakini Jumamosi au Jumapili lazima wataitenga kuwa pamoja siku nzima au nusu siku, hiyo shoping wanafanya pamoja, wanasaidiana usafi wa ndani akimaliza hapo basi anaenda kuonana na marafiki zake na huko wala hakai kwa muda mrefu anakuja kumaliza siku na wewe, upo?

Siyo umekaakaa kama feni ya panga boi iliyochakaa mpaka uilazimishe kuisukuma ndiyo iwake, shuuutuuuu! Mwanaume badilika, rejesha furaha ya nyumba, mpe nafasi mkeo ya kukaa naye, jua matatizo na umshirikishe mipango yako!

Shoga, wiki ijayo bado nitakuwa na wanaume nyienyie mnaopenda kuficha wanawake zenu mishahara, heeee heeeiyaaa kama nakuona unavyoniangalia, niko na weweeee! Tukutane wiki ijayo, ni mimi kungwi la makungwi niliyepigwa mishale mingi hadi kuota sugu, Shangingi Mstaafu Anti Naa.

Comments are closed.