The House of Favourite Newspapers

Ndugu Waitenga Familia ya Mzee Small

mzee-small2Na Gladness Mallya | Risasi Mchanganyiko, Toleo la Desemba 21, 2016

DAR ES SALAAM: Miaka miwili tangu kufariki kwa msanii mahiri wa vichekesho nchini, marehemu Said Ngamba ‘Mzee Small’, ndugu wa familia yake wanadaiwa kuwa katika mgogoro mkubwa, uliosababisha waitenge, kwani hivi sasa kila mmoja anaishi kivyake.

Chanzo cha karibu na familia hiyo kililiambia Risasi Mchanganyiko kuwa mara tu baada ya kufariki, baadhi ya ndugu zake walitaka mke wa marehemu, Fatuma Said aondoke ili asiwe miongoni mwa wasimamizi wa mirathi, jambo lililosababisha watoto wake kukimbilia mahakamani.

“Yaani ulikuwa ni mgogoro mzito kwani kuna baadhi ya ndugu walitaka mke wa Mzee Small aondoke, lakini kwa kushirikiana na mtoto wake mkubwa wakaenda mahakamani na mpaka sasa hawako vizuri na hao ndugu zao, hawazungumzi, kila mtu na maisha yake,” kilisema chanzo hicho.

Baada ya kupata habari hizo, Risasi Mchanganyiko lilitia ‘maguu’ nyumbani kwa Mzee Small, Tabata-Mawenzi, Dar na kufanikiwa kukutana na mtoto wake aliyejitambulisha kwa jina la  Mahamudu Said Ngamba aliyekiri kuwepo kwa mgogoro huo.

“Hatuko vizuri kabisa na ndugu zetu wa upande ule, maana walitaka baada ya mzee kufariki mama naye aondoke, tulienda mahakamani na mimi na mama yangu tukashinda na kuchaguliwa kuwa wasimamizi rasmi wa mirathi, kwani mzee aliacha nyumba tano na miradi ya maji ambapo fedha tunazozipata huko tunawalipia wadogo zangu ada ya shule kwani bado wanasoma.

“Wao hawana habari na sisi na hakuna mtu anayeenda nyumbani kwa mwenzake, jambo ambalo linaniumiza na ninawaomba waachane na mambo hayo, yamepita kama tuliwakosea watusamehe, kwani kuna wakati tunatamani kwenda kuwasalimia lakini tunashindwa kutokana na tofauti zilizopo,” alisema Mahamudu.

Ili kuleta usawa, gazeti hili lilimtafuta mmoja wa wanandugu wanaodaiwa kuwasusa, (jina linahifadhiwa) na kumuuliza kuhusu mgogoro huo, lakini alikana kuwepo kwa tatizo, akisema wao ni watu wazima wenye akili timamu, hawawezi kuingilia mali za Mzee Small kwani alikuwa na mke na watoto.

“Sisi ni watu wenye akili timamu na tunajiheshimu hivyo hatuwezi kuingilia mali za Mzee Small maana ameacha mke na watoto, huyo aliyesema tuligombana kisa mali maneno hayo siyo ya kweli hata kidogo,” alisema ndugu huyo.

Darassa Anusurika Kifo kwa Ajali Hii Mbaya ya Gari Huko Kahama Shinyaga

Comments are closed.