The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nifanikiwe-23

ILIPOISHIA

Nikakifuata kiti kimoja na kutulia, tukaletewa vitabu vidogo kwa lengo la kuimba nyimbo za kumtukuza shetani, mbali na vitabu hivyo vidogo tukaletewa vitabu walivyoviita Biblia lakini kitu cha ajabu Biblia hizi zilikuwa tofauti kabisa.

Pale mbele kabisa yaani kwa juu ziliandikwa LUSIFA…tena kwa herufi kubwa. Nikashangaa!

SONGA NAYO

Leo ninapokaa na kuanza kufikiria maisha yangu niliyoishi ya kumtumikia shetani huwa ninaumia, nimetubu kwa Mungu lakini wakati mwingine nahisi kama Mungu hakuwa amenisamehe kwani niliyoyafanya yalikuwa mengi mno.

Yanayoendelea katika ulimwengu mwingine yanatisha sana, nilibaki nikiiangalia Biblia ile, mwili wangu ulikuwa ukitetemeka sana, sikuamini kama kweli ulimwengu mwingine nao walikuwa na Biblia yao, moja ya vitabu vinavyoheshimika sana duniani.

Bado watu walikuwa wakiendelea kuimba nyimbo za kumtukuza shetani. Japokuwa sikuwa tayari kumwabudu shetani lakini sikuwa na jinsi, kila mmoja alikuwa makini sana ndani ya jumba lile.

Baada ya muda wa kumsifu shetani ulipokwisha, tukaambiwa tunyamaze kwani kulikuwa na ugeni maalumu uliotoka kuzimu ambao ulifika hapo kanisani kwa ajili ya kutusalimia.

Wote tukabaki kimya na baada ya muda kama wa dakika mbili, watu wawili wakatokea, walikuwa ni mwanamke na mwanaume. Wote walikuwa wazuri wa sura, sikujua hao walikuwa wakina nani lakini tukaambiwa kwa sisi tusiowajua, hao walikuwa ni jini mahaba ambaye alijulikana kwa jina la jini Maimuna na jini makata, jini ambaye alikuwa na hasira kali sana.

Hao ndiyo waliokuwa wakiuendesha ulimwengu kwa kipindi hicho, wao ndiyo walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha dunia inapotea. Leo unapowaona watu wanapenda sana ngono, jua kwamba jini Maimuna anafanya kazi yake, anawasahaulisha watu na ufalme wa Mungu hivyo kuanguka katika dhambi.

Mbali na ngono, pia unaweza kushangaa kwa nini watu wanauana sana. Unasikia mahali fulani kuna mauaji makubwa yametokea, kesho unasikia kuna mauaji sehemu fulani, ndugu zangu, hizo ni kazi za huyu Jini Makata ambaye amekuwa akisimamia katika suala zima la mauaji.

Walikuwa hapo kwa ajili ya kuwapongeza, walifanya kazi kubwa sana kiasi kwamba hata shetani mwenyewe alihisi kwamba jina lake linaendelea kutukuzwa kila siku.
Walianza kuongea, hawakuongea Kiswahili wala Kiingereza, walizungumza kwa lugha nyingine kabisa ambayo sidhani kama ilikuwa hapa duniani lakini kitu cha ajabu kabisa, niliielewa vizuri kabisa lugha hiyo.

Walipata dakika ishirini za kuzungumza ndipo wakaondoka na baadaye shetani kuingia. Kama unakumbuka ile picha niliyoiona pale nje kwenye jengo, ndiyo picha halisi ya shetani, alikuwa na umbo la kibinadamu lakini sura yake ilikuwa ni ya mnyama.

Alisimama mbele yetu na kuanza kuzungumza, sauti yake haikuwa ya kawaida, ilikuwa na mikwaruzo mingi, sauti yake ilikuwa tofauti na ile sauti ya kipole iliyokuwa imezungumza nami siku za nyuma, kwa kuisikia sauti yake tu, ilikuwa ni rahisi kujua kwamba huyo hakuwa mtu wa amani hata kidogo.

Huko ndipo nilipopata siri kubwa, ningependa nizungumze japokuwa wengine wanaweza kuhisi vibaya. Katika dini hiyo kumegawanyika, kuna watu ambao kazi yao kubwa inakuwa ni kusimamia wanamuziki wa kike ambao wanatakiwa kuitumia miili yao kuvutia kazi zao.

Angalia video za muziki nchini Marekani, wanamuziki wengi wa kike wanacheza huku wakiwa wamevalia mavazi nusu utupu, hawafanyi hivyo kwa kupenda bali wamepewa maagizo kutoka katika dini hiyo ambayo imekusanya watu wengi sana duniani.

Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kupewa maagizo ya kufanya na vilevile kufahamiana na watu wengine huku wageni tukikaribishwa. Tulikaa huko kanisani kwa saa mbili ndipo tukatawanyika na kurudi.

“Mungu! Nitawezaje kutoka humu?” nilibaki nikiuliza kana kwamba Mungu alikuwa mbele yangu.

“Sipendi kukaa humu ila napo dunia imenikamata Mungu, nitatokaje?” niliendelea kuuliza huku nikiamini kwamba Mungu angenisikia na kunipa jibu.

Njiani wakati naelekea hotelini nilikuwa na mawazo tele, kiukweli hakukuwa na kitu kilichokuwa kikiniumiza kama kuwa katika dini hii, nilishindwa kujitoa kwa sababu nilitamani ule utajiri waliokuwa wamenipa.

Sikuchukua muda mrefu njiani nikafika hotelini, nikateremka na kupanda lifti kisha kuelekea chumbani kwangu huku ikiwa ni saa tisa usiku. Niliposhuka kwenye lifti, nikateremka na kuanza kuufuata mlango, nilipoufungua, nikaingia ndani na kuwasha taa.

Nilishtuka sana baada ya taa kuwaka, nilimuona Majeed akiwa mbele yangu, alikuwa kwenye kiti, alionekana kuwa mwingi wa hasira sana, alikuwa akiniangalia huku akiuma meno yake kwa hasira.

Niliogopa sana, nikabaki nikitetemeka, kwanza nikajiuliza aliingiaje ndani, hakuwa na ufunguo, funguo zote nilikuwa nazo mimi na pia nyingine iliyokuwa mapokezini, haikuchukuliwa kwani kama ingechukuliwa ningejua tu.

Wakati nikijiuliza aliingia vipi ndani ya chumba hicho, Majeed akasimama na kuanza kunisogelea, alionekana kuwa katika hali isiyo ya kawaida, niliona sura yake ikibadilika rangi na kuwa nyekundu, niliogopa, sikujua alitaka kufanya nini, lakini kingine nilichojiuliza, ni binadamu gani alikuwa na uwezo wa kubadilika rangi na kuwa mwekundu? Sikupata jibu, kila alivyokuwa akinisogelea, nilitamani kukimbia.

****

Kwa kweli niliogopa sana, sikuwahi kumuona Majeed akiwa kwenye hali ile tangu nilipofahamiana naye, alionekana kukasirika sana na sikujua sababu ya yeye kuwa vile ilikuwa ni nini. Nilibaki nikitetemeka huku nikimsogelea.

Nilipomfikia, nikamshika mkononi, mwili wake ulikuwa joto kali sana, si kama watu waliokuwa wakiumwa miili yao ilivyokuwa bali ulikuwa na joto kali kiasi kwamba mpaka nikahisi naungua mimi hivyo kuutoa mkono wangu haraka sana katika mwili wake.

“Kuna nini?” nilimuuliza huku nikionekana kuogopa.

“Umetoka wapi?” aliniuliza huku akiniangalia usoni.

“Kutembea…”
“Niambie umetoka wapi,” aliniambia huku akisimama.

“Kwa nini unaniuliza hivyo?” na mimi nilimuuliza.

“Ninataka kujua, umetoka wapi?” aliniuliza tena.

Kwa kweli alinikera sana, ndiyo nilikuwa nampenda lakini hakutakiwa kuwa mkali kama alivyokuwa. Mimi ni mwanamke, ninahitaji mwanaume atakayekuwa tayari kukaa chini na mimi na kuzungumza, pale ninapokosea, basi aniambie kwa sauti ambayo itanifanya nijue kweli nimekosea.

Yeye alikuwa mpenzi wangu, lakini hakupafahamu nyumbani kwangu, tulikutana tu ndani ya ndege, baada ya hapo, hakukuwa na kingine kilichoendelea, sasa kwa nini alijifanya kuwa mkali kwangu?

“Unaniuliza hivyo kama nani?” nilimuuliza, na mimi nikajifanya kumletea ukali kwani kama ningekaa kimya, angenipanda kichwani.

Nilivyomuuliza hivyo, nikamuona akianza kunyong’onyea na kukaa chini. Alikubaliana na swali langu, hakuwa mtu wa kunipelekesha ni lazima ajue kwamba mimi kama mwanamke nilikuwa na nafasi yangu katika mahusiano na si kufanya kila alichotaka nikifanye.

Hakunijibu zaidi ya kusimama tena na kuondoka zake, wala sikutaka kujali kwani hakuwa akinibabaisha kwa kitu chochote kile, kama yeye alikuwa mtu mwenye pesa, hata mimi mwenyewe nilikuwa hivyohivyo.

Usiku sikutaka kupoteza muda kumfikiria, nilifanya mambo yangu mengine na maisha kuendelea kama kawaida, sikutaka kumpigia simu wala nini kwani kama ni kuishi, nilikuwa na uwezo wa kuishi bila yeye. Asubuhi ilipofika, nikaondoka na kwenda katika ofisi za KLM na kujiandaa na safari ya kurudi Tanzania siku inayofuata.

Siku hiyo sikutaka kuwasiliana na Majeed kabisa, na ninadhani hata yeye alilifahamu hilo na ndiyo maana hata kunitumia meseji, hakunitumia. Asubuhi ilipofika, nikajiandaa na kwenda uwanja wa ndege ambapo nikapanda ndege na kurudi Tanzania.

Ndani ya ndege nilikuwa nikifikiria mambo mengi sana, nilitaka kuwa bilionea zaidi ya nilivyokuwa, nilitakiwa kupambana usiku na mchana, sikutaka kufikiria sana mapenzi kwani niliona yasingeniongezea kitu chochote kile katika maisha yangu.

Nikiwa katika mawazo hayo, mara mhudumu mmoja aliyekuwa amebana nywele zake kwa nyuma akaja pale nilipokuwa na kunipa kipande cha karatasi na kuniambia kwamba alikuwa amepewa na mtu aliyekuwa katika viti vya nyuma.

“Nani?” nilimuuliza.

“Sijui! Amesema nikupe tu,” alinijibu huku akiniangalia.

“Mh!” nilibaki kuguna tu.

Nilichokifanya ni kukichukua na kisha kufungua. Maneno niliyokutana nayo hayakuwa mengi, yalikuwa machache tu yaliyoandikwa ‘Nisamehe mpenzi, tutazungumza zaidi tukifika Tanzania.’

Baada ya kuandika ujumbe huo, kwa chini aliambatanisha na jina lake, alikuwa Majeed, kwa kweli nilishtuka, sikuamini kile nilichokiona, ilikuwaje Majeed awe ndani ya ndege hiyo? Sikuwa nimemwambia kwamba siku hiyo nilikuwa nikiondoka kurudi nyumbani, sasa alijuaje kama ningekuwa humo?

Nilichokifanya ni kusimama na kuangalia viti vya nyuma kama ningebahatika kumuona, nilipotazama, hakuwepo kitu kilichonifanya niwe na hofu moyoni mwangu.

“Mh! Huyo Majeed yupo wapi?” nilijiuliza huku nikiangalia huku na kule.

Kwa kweli hakuwepo, nilichanganyikiwa na wakati mwingine niliona kama nikiwa kwenye ndoto fulani hivi. Nilichokifanya ni kuanza kumtafuta mhudumu aliyekuwa amenipa kile kikaratasi ili niweze kuzungumza naye. Kitu cha ajabu, naye sikumuona.

“Jamani! Mbona hali inachanganya hivi? Mhudumu mwenyewe yupo wapi?” nilijiuliza.

Nilibahatika kuwaangalia wahudumu wote, yule mhudumu ambaye alibana nywele zake kwa nyuma sikumuona kabisa. Nilichanganyikiwa zaidi na kuhisi kwamba inawezekana nilikuwa katika ulimwengu mwingine kabisa.

Nikatulia kwenye kiti lakini sikuwa na amani hata kidogo. Nikaagiza juisi, ilipokuja, nikachukua na kuanza kunywa taratibu. Wakati juisi ikiwa nusu kabisa, nikasikia kama mtu ananiita, sauti yake niliijua vilivyo, ilikuwa ni ya Majeed, nikageuka nyuma ili nimwangalie, kitu cha ajabu sasa, katika kiti cha nyuma yangu, ndipo alipokuwa ametulia, nikashtuka kwani nilikumbuka vilivyo kwamba mwanzo nilipokuwa namtafuta, pale hakuwa yeye, sasa alifikaje hapo? Na kama alikuwa amekaa hapo tangu mwanzo, yule mwanaume aliyekuwa katika kiti hicho alikuwa wapi? Kila nilichojiuliza, nikakosa jibu, tukabaki tukiangaliana tu.

 

Je, nini kitaendelea?
Tuukutane Jumatatu hapahapa.

Comments are closed.