The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi Na Maiti 20 Nitajirike – 1

fb

KWA jina ninaitwa Zakia Ramadhani, ni mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto kumi, mama yangu aliyeitwa Zubeda Hassani na baba yetu aliyeitwa Saidi Ramadhani ambaye hapo tulipokuwa tukiishi alijulikana zaidi kwa jina la Mzee Mkude.

Familia yetu ilikuwa miongoni mwa familia masikini zilizokuwa zikiishi katika Kijiji cha Mbingu kilichokuwa katika Wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro. Hatukuwa na fedha, baba alikuwa mkulima mzuri wa mpunga, mara kwa mara aliamka asubuhi sana na kuelekea shambani kulima huku mama akibaki nyumbani akiandaa uji, unapoiva, ninaondoka naye na kuelekea huko shambani.

Maisha yalikuwa magumu, yalituumiza lakini hatukuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kupambana usiku na mchana ili tupate angalau fedha za kufanya mambo yetu mengine. Maisha hayo ya kimasikini, niliyachukia sana, nilitamani kuwa na fedha na kuyabadilisha maisha hayo, baba yangu atembelee gari, awe na nyumba nzuri na kufanya biashara zitakazomuingizia fedha nyingi.

Hizo zilikuwa ndoto nilizoota kila siku, ndoto za utajiri lakini kwenye maisha halisi, bado tulikuwa masikini wa kutupwa. Kula kwetu haikuwa ya uhakika, kidogo maisha yanakuwa na ahueni wakati wa mavuno, hapo, tutakula na kushiba, tutanunuliwa nguo na kufanya mambo mengine lakini kwenye kipindi cha upandaji mpunga, tulikuwa kwenye wakati mgumu sana.

Wazazi wetu hawakujua kitu chochote kuhusu uzazi wa mpango na ndiyo maana walizaa watoto wengi tena waliokuwa na utofauti wa umri mdogo, mimi ambaye ndiye nilikuwa mtoto wa kwanza, nilikuwa na miaka ishirini, aliyenifuata ambaye ni mvulana aliyeitwa Husseni alikuwa na miaka kumi na tisa, yaani watoto wote kumi tulipishana kwa mwaka mmojammoja.

Sikuwa na elimu, sikubahatika kuingia darasani, wazazi wetu hawakuwa wamesoma na hawakuamini kama elimu inaweza kumsaidia mtu kupata mafanikio. Kipindi cha nyuma waliambiwa sana watupeleke shule kujifunza lakini wakakataa kwa kuamini kwamba hata usipokuwa na elimu, ukitafuta fedha, utazipata tu, cha msingi uwe na moyo wa kutafuta.

“Unaweza kwenda shule, ukapoteza fedha kumbe Mungu amekwishakuandikia maisha ya kitajiri hapo baadaye, uje kuolewa na milionea au hata wewe kupata fedha kupitia biashara nyingine,” aliniambia baba, tena kwa ujasiri huku akiniangalia machoni.

Nilichokigundua ni kwamba baba hakuwa na fedha, hakuwa na uwezo wa kutulipia ada na ndiyo maana hata sababu alizozitoa hazikuwa na msingihata kidogo. Sikutaka kuingilia, niliendelea kubaki nyumbani mpaka nilipofikia umri huo, sikuwahi hata kuingia darasani kusoma.

Miaka ishirini lakini bado niliendelea kuishi kwa wazazi. Sijui kama nilirogwa au la lakini ukweli ni kwamba kila mwanaume niliyekuwa naye aliniacha siku chache kabla ya ndoa kisha kumuoa mwanamke mwingine.

Nakumbuka nilikuwa na mwanaume aliyeitwa Hamisi Sultan. Huyu mwanaume alinipenda sana, alikuwa mkulima mzuri, alijituma sana kijijini kiasi cha kumiliki mashamba yake ya mpunga, wazazi wangu walimpenda lakini kitu cha ajabu kabisa kilichotushangaza, wiki mbili kabla ya kufunga ndoa, akaniacha na kumuoa mwanamke mwingine.

Iliniumiza moyoni, sikuwa na jinsi, nililia sana na mwisho wa siku nikasahau na kuendelea na maisha yangu. Mwanaume wa pili aliyefuata aliitwa Abdul Maliki. Alikuwa mzuri wa sura, nilimpenda sana na wiki tatu kabla ya kufunga ndoa, akaniacha na kumuoa mwanamke mwingine.

Hayo yote yaliyotokea, yaliniumiza mno, sikuamini kama mimi ndiye niliyekuwa nikipitia maisha hayo. Hawakuishia wanaume hao tu, walikuja wengine kama watatu lakini matokeo yalikuwa yaleyale, kila aliyetaka kuniona, wiki chache kabla ya kufunga ndoa, aliniacha.

Sikutaka kukubali, nilichokifanya ni kufanya uchunguzi wa kujua tatizo lilikuwa nini, nilichogundua ni kwamba sababu kubwa ilikuwa ni umasikini na pia familia kuwa kubwa ilisababisha. Wanaume waliogopa kunioa kwa kuwa walijua kwamba sisi ni masikini, familia ya watoto kumi ilikuwa kubwa kiasi kwamba wakaona kama wangenioa, basi wangebebeshwa mzigo mkubwa wa kuitunza familia.

Nikakata tamaa ya kuolewa, sikuona kama kuna mwanaume mwingine angekuja na kunioa. Nililia usiku kucha, nilimlaumu Mungu lakini pamoja na kulia kote, lawama zote nilizozitoa, ukweli ukabaki palepale kwamba hakukuwa na mwanaume aliyetaka kunioa.

“Yaani sababu ya umasikini tu? Yaani sababu ya kuwa na familia kubwa tu?” nilijiuliza maswali mawili, majibu yake yalikuwa yenye kuumiza mno.

Maisha yaliendelea, hapo kijijini kulikuwa na familia nyingine zilizokuwa na uwezo kifedha, zilikuwa na nyumba zenye mabati, nyumba zao zilijengwa kwa matofali, hizohizo familia ndizo zilizotuletea dharau sisi masikini.

Kulikuwa na mambo mengi yaliyoniumiza, ila hili, lilikuwa la kwanza. Sikuona sababu ya kudharaulika kwa kuwa hatukuwa na fedha, sikuona sababu ya wazazi wangu kudharaulika kwa kuwa tu kila siku walivaa mavazi yaliyochakaa. Nilitaka na sisi tupewe heshima kama watu wengine, tupendwe na kuthaminiwa kama watu wengine ila hayo yote, yasingewezekana bila kuwa na fedha.

“Baba, hizi dharau zitakwisha lini?” nilimuuliza baba.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia kesho hapa kujua kitakachoendelea katika sehemu ya pili.

MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI

halotel-1

Comments are closed.