The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike-17

ILIPOISHIA..

Kila niliyemwangalia, alionekana kuwa na hamu ya kufahamu, utajiri mkubwa namna hiyo niliutoa wapi? Kwani hata gari nililokuwa nalo, lilikuwa gumzo sana kijiji kizima na hata vijiji vya jirani . Eti yule Zakia aliyekataliwa kuolewa na wanaume kibao, leo alikuwa tajiri! Haikuwaingia akilini.

ENDELEA NAYO…

Niliendelea kuwa gumzo kila kona ndani ya kijiji hicho na hata vijiji vya jirani, wale wanaume waliokuwa wamenikataa, walishangaa, nilijua kwamba walijuta kwani waliamini kama wangekubali kunioa, inawezekana katika maisha hayo tungekuwa pamoja, kutanua pamoja na kufanya mambo mengine pamoja, hata huo utajiri ungekuwa wao pia.

Sikutaka kujali, niliamua kusahau kila kilichotokea na katika kipindi hicho nilikuwa bize kufanya mambo yangu. Nilifika kijijini, familia yangu haikuwa hata na fedha za kutosha, hivyo haikuweza hata kuandaa chakula kwa ajili ya watu wengine lakini kwa sababu nilikuwa kijijini hapo, nilihakikisha hakuna kitu kinachoharibika.

Nilikanunua magunia ya mchele na maharage, wanawake waliokuwa hapo, huku nikisaidiana nao tukaanza kupika chakula kwa ajili ya watu waliokuwa msibani hapo.

Maisha yaliendelea, sikutaka kurudi, niliendelea kukaa kijijini hapo huku nikisubiri arobaini ya baba na ndipo nirudi nyumbani. Biashara zangu hazikusimama, kila siku fedha ziliingia kwani watu niliowaweka katika biashara hizo, hawakuweza kunizunguka au kunidhulumu kwani fedha zenyewe zilikuwa na ulinzi mkubwa.

Niliendelea kuwa gumzo, ilikuwa vigumu sana watu kugundua mahali nilipoupata utajiri huo. Wengine waliulizana maswali, majibu yao yalikuwa ni hisia kwamba inawezekana nilijishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya mjini, wengine wakahisi kwamba inawezekana nilikuwa changudoa, kilichowashangaza ni kwamba japokuwa nilikuwa hapo kijijini, bado niliendelea kuingiza fedha kama kawaida.

Sikutaka mama na ndugu zangu wengine waendelee kuishi kwenye nyumba hiyo, nilichokifanya ni kuirekebisha huku nikinunua nyumba nyingine na kuzikarabati, zikaonekana kisasa, kulikuwa na mabati, zilipakwa rangi na kuonekana kama nyumba za mjini.

Wanaume waliniogopa, hawakujiamini, nilipata taarifa zao kwamba walikuwa wakinizungumzia sana, hasa uzuri wangu lakini hakukuwa na aliyekuwa tayari kunifuata, waliniogopa sana, sikutaka kujali kwani kijijini hakukuwa makazi yangu tena, nilikuwa nakaa kwa muda kabla ya kurudi Dar es Salaam.

Baada ya wiki mbili kukaa kijijini hapo ndipo nilipoanza kuona mambo ya ajabu ambayo yalinishangaza sana. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuota ndoto mbaya na za kutisha zilizonisisimua usiku mzima.

Haikuwa kawaida, kipindi hicho hali ilikuwa mbaya kabisa. Kuna siku niliota nikiwa kwenye mlima mmoja mkubwa, nilisimama kileleni kabisa, mlimani kule kulikuwa na makaburi ishirini na moja, nilijiuliza yale makaburi yalikuwa ni ya nini, majibu niliyopata ni kwamba yale ishirini yalikuwa ni ya zile maiti nilizofanya nazo mapenzi na lile moja lilikuwa ni kaburi la baba yangu.

Niliogopa sana, nilitamani kuondoka mahali hapo, kila niliponyanyua mguu, nilishindwa kukimbia. Wakati nawaza ni kitu gani nilitakiwa kufanya, ghafla nikaanza kusikia sauti za paka wengi, nilishangaa, iweje nisikie sauti za paka wengi na wakati nilipopiga macho huku na kule hakukuwa na paka? Nilijiuliza lakini hata kabla sijapata jibu, kwa mbele yangu nilimuona paka mkubwa, ukubwa wake ni mithili ya mbuzi.

Nilibaki nikimshangaa paka yule, sikuwahi kumuona kabla, alikuwa mweusi tii na macho yake yalikuwa yaking’ara sana usiku ule, mwendo wake ulikuwa ni wa madoido, na kila alipokuwa akipiga hatua, alikuwa akilia.

Paka yule alinisogelea, nilibaki nikitetemeka tu, nilitamani kukimbia ila nikashindwa, paka yule akanisogelea na kuanza kuniangalia machoni, kilichonishangaza, macho yake hayakuwa ya paka bali yalikuwa ni ya binadamu.

“Kwa nini umefanya hivi Zakia?” aliniuliza paka yule.

Hapo ndipo nikashangaa zaidi, paka kuongea, tena alitoa sauti iliyofanana kabisa na ya baba yangu. Paka yule akaanza kutokwa na machozi ya damu, niliogopa na kuhisi kwamba kulikuwa na kitu mahali hapo, huku nikiwa namshangaa, paka yule akabadilika na kuwa katika umbo la binadamu. Alikuwa baba yangu.

“Baba…” nilianza kuita huku nikibubujikwa na machozi.

“Kwa nini umeniua binti yangu?” aliniuliza, nilibaki nikitetemeka, sikumjibu, nilibaki kimya huku nikimwangalia.

“Umeniua kwa sababu ya pesa! Pesa kitu gani Zakia, utakufa, utaziacha na hutoweza kuzikwa nazo, yaani umeniua kwa sababu ya tamaa ya pesa!” alisema baba huku akitia huruma sana, hata mimi mwenyewe nilibaki nikimshangaa.

Wakati akizungumza maneno hayo, ghafla nikawaona paka wengine wakija kutoka katika upande aliokuwa baba, nilibaki nikijiuliza wale paka walikuwa wakina nani. Walikuwa ishirini kwani niliwahesabu kwa haraka sana, walipofika karibu yangu, wakabadilika na kuwa zile maiti ambazo nilifanya nazo mapenzi.

“Umefanya mapenzi na sisi kwa sababu ya utajiri!” alisema maiti moja huku wote wakiniangalia.

Sikujibu kitu chochote kile, mwili mzima ulikuwa ukitoka jasho, nilitetemeka kana kwamba nilikuwa katika sehemu iliyokuwa na baridi kali. Hofu ilinijaa moyoni mwangu, nilipoziangalia maiti zile, zilitisha, zilikuwa na damu, hazikuoshwa, yaani kama zilikuwa zimetoka kupata ajali muda si mrefu.

“Kwa nini uliniua?” aliniuliza baba kwa sauti kubwa iliyozitetemesha ngoma za masikio yangu. Hapohapo nikaanza kupiga kelele na kukurupuka kitandani pale huku nikihema kwa nguvu kama mtu aliyenusurika kufa.

“Kuna nini Zakia?” aliniuliza mama baada ya kuniona nikiwa nimeshtuka kutoka usingizini huku nikitetemeka.

“Mama! Baba! Nimemuona baba…” nilimwambia mama huku nikimsogelea, nilikuwa na hofu kubwa.

“Ni ndoto Zakia, ni ndoto tu!” mama aliniambia huku akinivuta nisogee karibu yake.

“Nimemuona baba!’

Wakati nazungumza hayo, ghafla katika hali iliyonishtua, mbele yangu kukatokea kundi kubwa la watu, walivalia sanda, nilipowaangalia vizuri wale watu, zilikuwa zile maiti, mbele yao kabisa waliongozwa na baba ambaye alikuwa na damu mwili mzima. Kuona hivyo tu, nikaanza kupiga kelele, cha kushangaza, mama hakuziona maiti hizo.

“Mama…mama…maiti…maiti mama…” nilipiga kelele huku nimwambia mama aziangalie zile maiti zilizokuwa zimesimama mbele yetu lakini mama hakuona kitu zaidi ya giza ambalo lilitawala chumbani mule.

“Maiti?”
“Ndiyo mama! Hizo hapo zimesimama, zimevaa sanda, mama, naogopa wataniua,” nilimwambia mama.

Wakati nazungumza hayo, mwili wote ulikuwa umelowa jasho, mauzauza yaliyokuwa yakitokea yaliniogopesha mno, kuna kipindi niliona bora kufa kuliko kuendelea kuyaona yale niliyokuwa nikiyaona mbele yangu.

Usiku wa siku hiyo sikulala tena, niliendelea kubaki macho, maiti zile hazikuzungumza kitu chochote kile, zilibaki zikiwa zimesimama mahali pale. Maiti ya baba ilikuwa mbele kabisa, ilivalia sanda nyeupe zaidi ya sanda zilizovalishwa kwa zile maiti nyingine.

Mpaka inafika alfajiri, saa kumi, maiti zile ndipo zilipoanza kupotea chumbani mule. Bado nilikuwa nikiweweseka sana na niliona njia sahihi ya kuepukana na hayo yote ilikuwa ni kuondoka tu.
Sikutaka kukaa tena kijijini kwa kuamini kwamba mauzauza kama yale hutokea vijijini tu kwani nilipokuwa Dar, hakukuwa na mauzauza hayo, hivyo nikapanga kuondoka hata kabla ya arobaini ya baba.

“Mama! Nataka kuondoka,” nilimwambia mama, akaonekana kushtuka.

“Unasemaje?”
“Siwezi kukaa hapa, kuna uchawi sana, naogopa kufa, siwezi kukaa hapa,” nilimwambia mama huku nikimaanisha kile nilichokuwa nikikizungumza mbele yake.

“Lakini arobaini ya baba yako bado.”
“Najua mama, ila si kukaa kwa hofu namna hii, kila siku maiti, ninaweweseka mama, kuna watu wananiroga hapa,” nilimwambia mama.

“Basi tutakwenda kwa mganga,” aliniambia.

“Kwa mganga? Siwezi mama, siwezi kwenda kwa mganga,” nilimwambia.

Nilijua kile ambacho kingetokea huko, najua kwamba mganga ambaye tungemwendea angeweza kusema kila kitu kilichotokea kwamba maiti hizo zilinitokea kwa kuwa ni lifanya nazo mapenzi.

Sikutaka mama au mtu mwingine yeyote ajue kilichokuwa kimeendelea na ndiyo maana nikakataa kwenda kwa mganga. Hakukuwa na mtu aliyezungumza lolote lile, kwa kuwa nilikuwa na fedha, walifanya kila kitu nilichowaambia.

Wanakijiji wengi walinishangaa, hawakuamini kama hayo ndiyo yalikuwa maamuzi yangu, kuondoka kijijini hata kabla ya robaini ya baba. Hakukutakiwa mtu yeyote aniambie kitu chochote kile ili nibadilishe msimamo wangu, niliendelea kuwaambia kwamba ni lazima niondoke kijijini na kurudi mjini.

Siku hiyo, nikaanza safari ya kurudi Dar huku nikiwa nimewaachia kiasi kikubwa cha fedha na kuahidi kuendelea kuwatumia fedha zaidi. Ndani ya gari, nilikuwa na mawazo tele, sikuamini kama kweli kile kilichokuwa kikitokea, kilinitokea kipindi hicho.

“Kwa nini mimi? Kwa nini hili linatokea?” nilijiuliza, wakati nikijiuliza hilo, hapohapo nikasikia sauti ya mganga ikinijibu.

“Kwa sababu kuna mengi tumeandaa kwa ajili yako,” niliisikia vema.

“Yapi?”
“Tunataka kukufanya zaidi ya ulivyokuwa. Uwe mwanamke mwenye heshima kuanzia Tanzania mpaka Afrika kwa ujumla,” niliisikia sauti hiyo.

“Mimi?”
“Ndiyo!”

Sikushangaa, niliamini kwamba hilo linawezekana kutokana na maisha niliyoamua kuishi kipindi hicho. Kama ni kumtumikia shetani, niliamua kufanya hivyo kwa asilimia zote, sikutaka kuacha kumtumikia kwani niliweza kuyaona mafanikio makubwa mbele yangu.

Niliendesha gari kwa mwendo wa kasi mpaka nilipofika Ifakara, sikutaka kumtafuta Mudi, nilikuwa na mawazo yangu, nikachukua nyumba ya wageni na kulala humo.

Wakati nikiwa kwenye usingizi mzito, ghafla nikaanza kuota ndoto moja hivi, ndoto iliyousisimua mwili wangu, sikuamini kile nilichokuwa nikikiona kwenye ndoto ile kingekuja kutokea siku moja katika maisha yangu, nilibaki nikiweweseka kitandani pale huku nikijiuliza swali moja la msingi, je ni kweli nilichokiona kingetokea? Sikuwa na jibu hata kidogo. Ndoto yenyewe ilikuwa hivi…

Je, nini kitaendelea?
Je, ndoto hiyo ni ipi?

Tukutane Jumatano hapahapa.12966416_1315897695093303_1213372974_n

Comments are closed.