The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti Ili Nitajirike -20

0

ILIPOISHIA

Nikasikia sauti ile ikiniambia niende ndani ya mochwari ile, maelekezo mengine angeniambia, nikafanya hivyo na kuanza kuingia humo ambapo kulikuwa na masanduku mengi yaliyokuwa na maiti nyingi. Nikaambiwa nisubiri. Nakuja kutahamaki, eti ilikuwa saa sita usiku. Nikabaki nikitetemeka tu.

SONGA NAYO
Ulikuwa usiku mkubwa, nakiri kwamba hakukuwa na sehemu iliyokuwa inatisha kama ilivyokuwa mochwari. Ndani ya mochwari ile, kulikuwa na majeneza ya maiti ambazo zililetwa humo ndani na nyingine tayari kwa kuchukuliwa lakini pia kulikuwa na masanduku mengi ambayo ndani yake kulikuwa na maiti, baridi lililokuwa humo ndani, lilikuwa kubwa mno.

Humo kulikuwa na walinzi wawili, walikuwa wakilinda, nilijiuliza walipata wapi ujasiri wa kuwa ndani ya chumba kile, tena usiku mzima huku wakionekana kutokuwa na hofu hata kidogo.
Mimi, sikuwa nikionekana, yaani hata niliposogea karibu yao, hawakuwa wakiniona zaidi ya kufanya vitu vyangu. Humo, ndipo nilipojifunza kwamba kulikuwa na mambo mengi yaliyokuwa yakitokea.

Niliwaona watu wakija usiku huohuo, walikuwa wakizungumza na walinzi hao na kuwaambia shida zao, wengine walifika kwa kuwa walihitaji baadhi ya viungo kutoka kwa maiti ili waende kufanya mambo yao ya kishirikina.
Nilimuona mlinzi mmoja akitoka na kwenda kwenye sanduku moja, akalivuta kisha kuanza kuitoa maiti iliyokuwa ndani. Mwili wangu ulisisimka mno, sikuamini nilichokuwa nikikiona, hofu ilinijaa moyoni mwangu.
Mlinzi yule akaivua nguo maiti ile, sikujua alichokuwa akikihitaji, yale mambo ambayo nilikuwa nikiyasoma kwenye vitabu vya kusisimua, siku hiyo nilikuwa nikiyaona kwa macho yangu.

Akachukua kisu ambacho alikihifadhi sehemu maalum, nyuma ya mlango na kisha kuanza kukata kifundo cha mguu cha maiti ile kwani ndicho kilichokuwa kikihitajika kwa hali na mali.
Ninayoyazungumza hapa, niliyashuhudia kwa macho yangu. Mapigo yangu ya moyo yalikuwa juu mno, japokuwa kile kilikuwa kikifanywa kwa maiti lakini niliogopa na kuionea huruma, niliona kama ilikuwa ikionewa.
Alipomaliza, mlinzi akakichukua kifundo cha mguu ule kisha kumpa mwanaume aliyekuwa amekifuata na kuondoka nacho. Walinzi waligongesheana mikono, kila mmoja alionekana kuwa na furaha.

Wala haukupita muda mrefu, nikaona mlinzi mmoja akitoka nje. Sikutaka kubaki ndani, wakati namsubiria yule mganga, nilitaka kujua ni kitu gani kingine kilichokuwa kikitokea.
Nilimfuata mlinzi, alikwenda moja kwa moja kwenye gari la kifahari, Range SUV nyeusi na kuongea na mtu aliyekuwa humo ndani. Nilisogea kwani nilitaka kuyasikiliza mazungumzo yao.

“Nahitaji maji ya maiti,” alisema mzee aliyekuwa humo ndani ya gari.
“Laki mbili! Hela ipo?” aliuliza mlinzi yule.
“Ipo! Naomba ukaniwekee humu!”
Yule mzee sikuweza kumfahamu kwa kipindi kile lakini sauti yake, hapo baadaye nilimfahamu kwani nilikutana naye mara kwa mara. Baada ya kuzungumza hivyo, akatoa kidumu na kumpa mlinzi yule ambaye akakichukua na kuondoka nacho.
Sikutaka kubaki hapo nje, nikamfuata mlinzi mle mochwari alipokwenda. Nilipoingia, nikakuta akimwambia mwenzake kwamba kulikuwa na dili jingine, kuna mtu alifuata maji ya maiti.

“Hakuna tatizo! Twende kule kwenye maiti za wiki iliyopita!” alisema mlinzi aliyeletewa taarifa.
Wakatoka na kuelekea kwenye moja ya masanduku yaliyokuwa mwisho kabisa ambayo yalikuwa na maiti zilizokuwa na muda mrefu humo mochwari. Wakafungua sanduku moja, wakatoa maiti ya msichana na kuiweka juu ya meza moja kisha kuanza kuiosha huku wakikinga maji na kuyaweka katika sufuria kubwa kabla ya kuyaweka katika kidumu kile.
“Mungu! Kumbe haya ndiyo yanayotokea!” nilijikuta nikisema.

Waliendelea na zoezi lao mpaka walipomaliza na kujaza kile kidumu, yule mlinzi akaelekea nje na kumpa yule mzee, gari likawashwa na kuondoka mahali hapo.

Wakati ikiwa imefika saa nane usiku, hapo ndipo mganga yule akatokea na kunifuata. Kabla ya kuzungumza lolote, akaniangalia machoni, aliiona hofu niliyokuwa nayo.
“Upo sawa?” aliniuliza.
“Ndiyo! Nipo sawa na nipo tayari kwa kazi,” nilimwambia.
Alichokifanya mganga yule ni kuuchukua usinga wake, akaanza kuimba wimbo ambao sikuwa nikiuelewa. Aliimba kwa sauti kubwa iliyonifanya nione kama wale walinzi wangesikia lakini haikuwa hivyo.
Waliendelea kupiga stori huku mganga yule akiendelea na wimbo wake. Alipomaliza, akalifuata sanduku moja, akalitoa pale lilipokuwa. Nilibaki nikiwa nimeduwaa tu, sikuamini kilichokuwa kikiendelea, sanduku lilikuwa zito lakini yeye alivyolishika ilikuwa ni kama mtu aliyeshika kikaratasi.

Akaliweka chini, akalifungua na kisha kuiangalia maiti ile. Niliogopa, hata kusogea kule sikuweza. Wakati nimesimama huku nikiwa nimeduwaa, yule mganga akachukua unga fulani na kuipaka maiti ile kisha kuanza kuzungumza maneno ambayo sikuyaelewa, ghafla katika hali iliyonishtua nikaiona maiti ile ikiinua mkono wake.

“Mungu wangu!” nilisema kwa mshtuko, sikuamini kile nilichokiona. Mganga yule hakunyamaza, aliendelea kuzungumza maneno yale, mbali na mkono, ile maiti ikainuka kisha kukaa kitako mlemle kwenye sanduku. Mpaka kufikia hatua hiyo, nilitamani kukimbia. Jasho lilinitoka.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply