The House of Favourite Newspapers

Nilikula Chakula Kwa Jirani, Nikawa Mchawi! – 01

0

MPENZI msomaji, kabla sijaanza kukuletea mkasa mpya unaomhusu kijana mwenye kisa kipya ninachoanza kukisimulia leo ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam, napenda kuwashukuru wasomaji mlionipigia simu na kunipongeza kwa mkasa ulioisha wiki mbili zilizopita uliomhusu Sabina aliyekuwa akijihusisha na mambo ya kichawi yaliyosababisha kuwatoa kafara ndugu zake wakiwemo wa mumewe kwa ajili ya kupata utajiri.

Jambo la kuhuzunisha ni kwamba, mganga waliyekuwa wakimtegemea aliyekuwa wakala wa Lusifa huko Tabora alipofariki dunia wakakosa kinga ndipo mali zao ziliisha kwa kuteketea kwa moto.

Si mali za Sabina tu, pia rafiki yake aliyemshauri na kumpeleka kwa mganga huyo, naye alifariki ghafla na mali zake kuteketea na mwishoni Sabina alifariki dunia baada ya kufuatwa kimazingira na watu aliowatoa kafara wakiwemo wazazi, ndugu na watu baki waliovaa mashuka meusi waliomuita alipomalizia tu kumsimulia bibi yake mambo ya kichawi aliyokuwa akiyafanya.

Hata hivyo, nawapa pole wasomaji wote walioguswa na msiba wa dada Rosemary aliyesimulia kisa hicho kilichotuachia mafunzo mengi kuhusiana na mambo ya kichawi na utajiri wa kichawi aliyefariki dunia kwa matatizo ya uzazi katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Wasomaji hao ni wengi mno lakini miongoni mwao walionipigia simu na kushindwa kujizuia kulia alikuwa ni mama Mariam wa Ipuli Tabora, dada Debora wa Manyara, Mwalimu Mage wa Mtwara na baba wawili wa Makole Dodoma ambaye alisema mkasa huo umempa funzo kubwa sana.

Wengine ni Amini wa Dodoma aliyesema kisa hicho kimempa mafunzo maishani mwake, dada Esther wa Magereza Ukonga, Dar aliyeguswa mno na kifo cha Rosemary na kusema Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Mwingine ni dada Rinda wa Iringa, ambaye amesema kupitia mkasa huo umempa mafunzo na kutamani kusimulia mkasa wake ili kuelezea mapito ya maisha yake yanayohuzunisha ambapo hivi sasa anajuta.

Rinda aliyenisimulia kwa kifupi sana kisa hicho cha kusisimua, alinieleza kuwa, kutokana na masaibu yaliyompata, kisaikolojia hayupo vizuri labda mpaka atakapoileza jamii.

Jambo la kusikitisha nilitamani sana niwaletee kisa cha Rinda lakini mawasiliano hayakuwa mazuri ila nakuahidi nitamtafuta ili anisimulie kisa chake chote na nitakiandika siku za usoni.

Kwa kuwa ni wengi mno wameguswa na kifo cha dada Rosemary na kisa cha Sabina na kukiri kwamba kimewapa mafunzo, nawasihi kutafuta mafanikio kwa njia halali badala ya kutumia uchawi ambao mwisho wake huwa si mzuri kama ilivyotokea kwa marehemu Sabina aliyepoteza mali na maisha ya watu wengi wasio na hatia wakiwemo wazazi na ndugu zake.

Baada ya kutoa pole na shukurani kwa wote waliofuatilia mkasa wa Sabina uliokuwa na kichwa kisemacho; ‘Uchawi wa Shangazi Ulivyoteketeza Ukoo Wetu,’ nawaletea kisa cha kijana Samweli ambaye hivi sasa ana miaka 20 aliyeingizwa kwenye uchawi na mama mmoja mchawi aliyekuwa jirani yao wakati akiwa na umri wa miaka minne.

Kama ilivyokuwa katika mkasa wa Sabina, naamini kisa cha Samweli kitakuhuzunisha na kukupa funzo kuhusu malezi ya watoto, jinsi watu wabaya wanavyoweza kuyabadilisha maisha ya mtu mwema na kuwa mchawi kwa masilahi yao.

Hebu sasa ungana nami katika sehemu hii ya kwanza hadi nitakapohitimisha kusilimua kisa hiki cha aina yake kilichotokea katika jamii yetu kinachomhusu kijana Samweli ambaye anaanza kwa kusimulia:

Ndugu zangu, katika hii dunia kuna mambo ya kutisha yanayofanyika kwenye ulimwengu wa giza chini ya Lusifa mkuu ambaye ni shetani, shetani anapokuwa kazini hataki mchezo na yupo makini sana.

Shetani ni mjanja mno na kila siku iendayo kwa Mungu amekuwa akiongeza wafuasi wengi, anawaangusha dhambini watu waliosimama imara kwenye imani zao na kuwapeleka kwenye ziwa la moto.

Lusifa nilijiyekuta nikimtumikia kwa kipindi cha miaka 14 baada ya kuingizwa kwenye uchawi na mama mmoja jirani yetu mchawi kisa kikiwa kuchukizwa na wokovu wa wazazi wangu, hana huruma hata kidogo!

Lusifa hachagui mtu wa kumtesa kwa kumfundisha mambo ya kichawi, wizi, uongo, kiburi, uzinzi, dharau, tamaa mbaya na mengineyo mengi maovu, akikunasa kutoka mikononi mwake huwa ni kwa neema ya Mungu pekee.

Ili upate picha kamili ya familia yetu na jinsi nilivyoingizwa kwenye uchawi na kupewa cheo kikubwa kwenye ulimwengu huo wa giza licha ya kuwa mtoto mdogo kwa vile tu wazazi wangu waliookoka waliwasumbua sana wachawi na kuharibu nguvu zao, ngoja nikuelezea historia yangu japo kwa ufupi.

Katika familia yetu, mimi ni mtoto wa kwanza nikifuatiwa na wadogo zangu wawili, wa mwisho wetu ni msichana ambaye hivi sasa anaishi na mama yetu mdogo mkoani Mbeya.

Hapa jijini Dar es Salaam tunaishi Buza wilayani Temeke kwenye nyumba yetu ambayo licha ya kuwa ni ya kisasa lakini bado haijafanyiwa umaliziaji (finishing) kutokana na hali ya kiuchumi ya baba kuwa mbaya kwani hivi sasa hana kazi.

Hata hivyo, tunamshukuru Mungu suala la kodi ya nyumba tumeepukana nalo, kwa sasa mtafutaji mkubwa wa riziki ya familia ni mama anayefanya biashara ndogondogo.

Mama yangu tangu alipoolewa na baba hakuwahi kuajiriwa zaidi ya kujishughulisha na biashara hizo, licha ya kuwa Wakristo lakini hawakuokoka.

Wa kwanza kuokoka alikuwa mama, aliniambia aliokoka Juni mwaka 1997 alipokuwa na ujauzito wangu baada ya kushuhudiwa mambo ya wokovu na rafiki yake aliyetubu dhambi na kuziacha.

Mama aliniambia baada ya kuokoka, baba hakumuelewa kwani aliacha mambo yote yasiyofaa kama kunywa pombe, kusengenya, manung’uniko, kuvaa nguo fupi au za kuacha sehemu kubwa ya mwili ikiwa wazi nk.

Anasema aliacha pia mambo ya kwenda kwa waganga, kusema uongo na mambo mengi yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu.

Kwa kuwa baba hakuokoka na alishirikiana na mama katika baadhi ya mambo, kitendo cha mama kuokoka kilimchukiza akawa adui wa mama.

Je, kiliendelea nini katika familia ya kina Samweli hadi akawa mchawi? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply