The House of Favourite Newspapers

KAHABA KUTOKA CHINA-06

0

 

Rose alibaki akiwa amepigwa na mshtuko mkubwa, hakuamini kama baba yake ndiye ambaye alisimama mbele ya geti lile. Alikuwa akimwangalia huku akitetemeka kupita kawaida. Hofu kubwa ikaingia moyoni mwake, uso wa baba yake ukaonekana kuwa kwenye hasira kubwa kupita kawaida.

Rose akaihisi miguu yake ikitetemeka sana, alitamanai kurudi kule alipotoka lakini akajikuta akikosa nguvu kabisa za kurudi.

Bwana Shedrack alikuwa akitetemeka kwa hasira, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka kwa wakati huo, macho yake yakaanza kupata wekundu fulani, hakuamini kama kweli Rose alikuwa ametoka nje ya nyumba ile bila ruhusa yake. Kichwani mwake kwa wakati huo, akili yake ikaanza kumwambia kwamba ile ndio ilikuwa tabia yake kwamba kila siku anaondoka nyumbani hapo na kwenda nje ya nyumba ile.

Hata kabla Rose hajajua ni nini cha kufanya, akashtukia akishikwa mkono na kuvutwa ndani. Bwana Shedrack alionekana kuwa mwingi wa hasira, kitendo cha Rose kutoka nje ya nyumba ile kilionekana kumkasirisha kupita kawaida. Huku akimvuta kuelekea ndani, alikuwa akiuvua mkanda wake, alipomfikisha sebuleni, akamtusukumia kwenye kochi.

Kabla ya kuchapwa mikanda, Rose alikuwa akilia kupita kawaida, kwake, tayari aliona kuwa kipindi hicho kilikuwa kipindi cha hatari kwake. Hasira ambazo alikuwa nazo baba yake zilionekana kuwa hasira kubwa ambazo zisingeweza kupoa hata mara moja.

Kabla ya kuanza kumchapa, Bwana Shedrack akalisogelea kochi moja na kukaa, alikuwa akihema kwa nguvu kana kwamba alikuwa ametoka kukimbia mbio ndefu. Hakutaka kumchapa Rose katika hali ya hasira ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho kwa kuona kwamba angeweza kumuua, alisubiria kwanza hasira zake zipungue.

“Naomba unisamehe baba” Rose alimuomba msamaha baba yake huku akianza kutembea kwa magoti na kulia.

“Umetoka wapi?” Lilikuwa swali la kwanza kutoka kinywani mwa Bwana Shedrack.

“Nimetoka kutembea” Rose alijibu huku akitetemeka.

“Wapi?”

“Nje” Rose alijibu.

“Sawa. Nipe simu yako” Bwana Shedrack alimwambia Rose.

Rose akashtuka kupita kawaida, hakutarajia kuambiwa maneno kama yale. Meseji zote ambazo alikuwa akitumiwa na wanaume wengine zilikuwa katika simu yake na wala hakuwa amezifuta. Akazidi kutetemeka, hakujua kama alitakiwa kumpa simu baba yake au la.

“Nipe simu yako” Bwana Shedrack alimwambia Rose kwa mara ya pili.

Rose hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kuchukua simu yake na kisha kumpa baba yake huku akitetemeka kupita kawaida. Bwana Shedrack akaichukua simu ile na kisha kuanza kuangalia angalia. Alifungua kila sehemu, akasoma meseji zote ila meseji za mwisho ambazo zilitumwa siku hiyo kwenda kwa Joshua zikamfanya kufahamu kila kitu.

“Umetoka kufanya mapenzi” Bwana Shedrack alimwambia Rose kwa hasira.

“Sijafanya baba”

“Umetoka kufanya mapenzi mpuuzi wewe. Nilikwishakwambia, nitakuua” Bwana Shedrack alimwambia Rose.

Siku hiyo hakutaka kumwadhibu, alijua fika kwamba kama angemuadhibu basi asingeweza kufanikisha kumshawishi juu ya suala la kuolewa na Peter ambaye alikuwa tayari kwa moyo mmoja kumuoa Rose.

“Naomba utulie Rose. Wewe ni binti yangu ambaye ninakupenda sana, tulia binti yangu. Kila kitu katika dunia hii kinapita. Wanaume wapo na wataendelea kuwepo” Bwana Shedrack alimwambia Rose.

Kwanza Rose hakuamini, hakuamini kama baba yake ndiye ambaye aliongea maneno yale mara baada ya kuonekana kuwa na hasira katika kipindi kichache kilichopita. Bwana Shedrack akasimama na kisha kumuinua Rose na kumkumbatia kitendo ambacho kilimshangaza mpaka John aliyekuwa pembeni.

“Badilika binti yangu. Mapenzi yapo tu” Bwana Shedrack alimwambia Rose.

“Nimebadilika baba. Nisamehe baba” Rose alimwambia baba yake.

Kuanzia siku hiyo Bwana Shedrack akajifanya kuwa na upendo wa dhati kwa Rose, hakutaka kumfokea kwa kitu chochote kile, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuitengeneza akili ya Rose na hatimae mwisho wa siku aje kukubali kuoana na Peter.

Kitu alichokifanya Bwana Shedrack ni kuchukua simu ya Rose na kisha kukaa nayo.Kila simu ambayo ilikuwa ikipigwa, alikuwa akiangalia kioo, alipoona kwamba ilikuwa namba ngeni, alikuwa akiachana nayo.

Maisha yaliendelea zaidi na zaidi mpaka kufikia siku ambayo Bwana Shedrack akaamua kumwambia Rose ukweli juu ya Peter ambaye alikuwa akimpenda sana na alikuwa tayari kumuoa na kuishi kama mume na mke.

“Sitaki kuolewa baba” Rose alimwambia baba yake.

“Kwa nini tena binti yangu mzuri?” Bwana Shedrack aliuliza.

“Nitakutia aibu”

“Kivipi? Una mimba?”

“Hapana”

“Sasa kivipi?”

“Simpendi Peter” Rose alijibu.

“Hapana. Unajua mapenzi si lazima mtu umpende siku hiyo hiyo, wakati mwingine unaweza kupita muda mrefu, halafu baadae ukaja kumpenda kwa dhati” Bwana Shedrack alimwambia Rose.

Kila siku Bwana Shedrack alikuwa mtu wa kubembeleza mpaka pale ambapo Rose akakubaliana nae. Kwanza kitu cha kwanza akawasiliana na Peter na kisha kumueleza kila kitu. Peter hakuonekana kuamini.

“Amekubali?”

“Ndio. Mimi ndiye mzazi, yeye ni mbegu yangu, kwa nini akatae”

“Nashukuru sana mzee. Kwa hiyo lini tuanze mipango ya harusi?”

“Siku yoyote ila kwanza njoo uonane nae” Bwana Shedrack alimwambia Peter.

Siku iliyofuata Peter akafika mahali hapo na kisha kuanza kuongea na Rose. Japokuwa Rose hakuwa akimpenda Peter, hakuwa na jinsi, akauruhusu moyo wake kumuingiza Peter ila wasiwasi wake ulikuwa sehemu moja tu, juu ya ujauzito aliokuwa nao.

“Huyu huyu nitambambikia” Rose alijisemea.

Kwa kuwa aliamini kwamba Peter alikuwa akimpenda, akataka kufanya nae mapenzi, Peter hakuwa na kizuizi, hakujua Rose alikuwa ametega nini. Peter akafanya mapenzi na Rose, mbegu zake zikaingia ila hazikuweza kufanya chochote kile.

“Mbona unahuzunika tena?”

“Leo ni siku yangu ya kupata mimba” Rose alimwambia Peter huku akijifanya kulia.

“Mungu wangu!”

“Ndio hivyo”

“Ila hakuna tatizo. Nitakuoa, tutamlea mtoto wetu pamoja” Peter alimwambia Rose.

Lengo la Rose likaonekana kukubalika, tayari aliona kwamba alikuwa amempatia sana Peter kwa kumuweka tayari kulea mtoto ambaye hakuwa damu yake. Kwa Peter ikaonekana kuwa kawaida, muda wote alikuwa tayari kulea mtoto hasa kwa Rose ambaye alikuwa akimpenda sana.

Mara baada ya kumaliza kila kitu wakatoka chumbani na kisha kuanza kumpeleka Rose nyumbani kwao kwa kutumia usafiri wake. Hawakuchukua muda mrefu, wakafika nyumbani hapo, Rose akateremka na kisha kuanza kuelekea ndani huku akiwa na furaha ya kukamilisha kile alichotaka kukikamilisha. Alipoufikia mlango wa sebuleni, akaufungua, macho yake yakatua usoni mwa baba yake ambaye alionekana kuwa na hasira.

“Kuna nini tena baba?” Rose aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.

“Irene……!” Bwana Shedrack alisema huku akiobnekana kuvimba kwa hasira na kuiweka simu ya Rose mezani kitendo ambacho kilimshtua sana Rose.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa hapahapa.

Leave A Reply