The House of Favourite Newspapers

Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani – 3

0

ILIPOISHIA:

Maisha yaliendelea, nakumbuka siku moja tukiwa tumelala majira ya saa saba usiku nyumba yetu ilivamiwa na maaskari. Emma Mo pamoja na mimi tulichukuliwa juujuu na kupelekwa polisi usiku huo huo. Kwa upande wangu sikujua tumechukuliwa kwa sababu gani.Kabla ya kutuchukua walifanya upekuzi mzito kitu kilichonishangaza na kujiuliza kuna nini.

SASA ENDELEA…

Tulipofika polisi tulitenganishwa kila mmoja aliwekwa sehemu yake, tulilala pale hadi asubuhi. Kesho yake majira ya saa tano tulitolewa kwa dhamana na rafiki zake na Emma Mo, walikuwa ni watu wenye pesa sana.

Mpaka tunarudi nyumbani sikujua jana yake tulichukuliwa na polisi kwa kosa gani, kila nilipomuuliza alinijibu kwa mkato; “Achana nayo.” Pamoja na kukaa kimya bado nilikuwa kwenye maswali mazito juu ya kuvamiwa na askari polisi wenye bunduki nzito na mbwa kama jambazi au haini.
* * *
Jioni ya siku ile Emma Mo alinieleza kuwa tatizo lake ni zito kwa hiyo anatakiwa kuondoka nchini usiku ule. Nilijiuliza ni tatizo gani linalomkimbiza nchi.
“Sasa utarudi lini?” nilimuuliza.

“Kwa kweli haijulikani, ikiwezekana kuonana itakuwa majaliwa.”
“Oooh Mungu wangu na mimi itakuwaje?”
“Sina jinsi itabidi nikuache kwa sababu tatizo lenyewe limetokea ghafla.”
“Mimi nitaishi vipi kwa kuwa wewe ndiye umeniachisha shule?” nilimuuliza nikiwa nimetaharuki.

“Siwezi kukuacha kwenye hali mbaya bali nitakuachia pesa nyingi, nina imani itakutosha kununua nyumba na gari zote nimekuachia.”
“Kiasi gani cha fedha unaniachia?”

“Milioni 70 ila hapa unatakiwa kuanzia kesho uondoke kwani nyumba hii si mali yetu tena, nimeiuza ili kupata nauli na pesa ya kukuachia.”

Nilitamani kulia kwa kujua sasa ndipo wakati wa kuadhirika mtoto wa kike kwa sababu Emma Mo alikuwa amenizoesha vibaya sana. Sikuwa na jinsi nilimuagia palepale kwa sharti hakutaka kusindikizwa na mtu. Baada ya Emma Mo kuondoka nilirudi ndani.

Baada ya kuondoka sikuona sababu ya kulia au kuhuzunika sana kwani Emma Mo alikuwa kishanifungulia maisha hivyo nilitakiwa kuyaendeleza. Nilijikuta nikiwa njia panda nifanye nini na zile pesa. Wazo la awali lilikuwa kurudi nyumbani na kuomba msamaha kwa wazazi wangu.

Lakini nilijiuliza nitawaeleza nini ili wanielewe ikiwa nimewatia hasara kubwa. Niliamua maisha yangu yawe mbele kwa mbele, sikutaka kurudi nyuma. Kama pesa nilikuwa nayo ya kuishi maisha yoyote ninayotaka. Nilisimama mbele ya kioo kuthibitisha uzuri wangu. Uzuri wangu ulikuwa umeongezeka mara dufu.

Nilikuwa nikiona fahari kusimama kwenye kioo kwa muda mrefu kwa kuuangalia uzuri wangu. Baada ya kununua nyumba na kuuza baadhi ya magari nilianza maisha mapya ya kujitegemea, bado niliishi maisha ya kifahari ya kujirusha kila kumbi ya starehe sikukosa mwisho wa wiki .

Siku zote kizuri chajiuza nilichukua muda wa miezi mitatu baada ya Emma Mo kuondoka kupata bwana mwingine. Nilimpata kijana wa Kiarabu ambaye nilimchanganya na kutangaza ndoa.

Kwa kweli ilikuwa harusi kubwa sana ambayo nina imani mpaka Mungu ananichukua haitatokea katika maisha yangu. Bwana huyu pesa alikuwa nayo alikuwa akimiliki magari na vituo zaidi ya kumi vya mafuta jijini.
* * *
Mwanzo ndoa niliifurahia kwa kuona napendwa na ndugu na jamaa wa mume wangu. Lakini ndoa ilinitumbukia nyongo kwa kujiona nipo kizuizini, yaani nilikuwa mimi na ndani ndani na mimi kama utumbo. Kwa kweli ndoa niligundua ni utumwa haina nafasi ya kujitawala.

Nilijifikiria kama pesa ninayo tatizo nini, maisha ya kufungwa yalinishinda na kuamua kuomba talaka, japokuwa mume wangu alinipenda sana. Lakini nilimlazimisha kunipa na kumtishia asiponipa talaka atanipea mahakamani.

Mume wangu hakuwa na jinsi alinipa talaka, baada ya talaka niliapa sitaolewa tena. Niliishi maisha yangu ya kumchagua mwanaume atakayekubali masharti yangu.

Niliyaanza maisha yangu kwa staili nyingine kwa kila jioni kwenda kwenye kumbi za starehe na kurudi nyumbani usiku wa manane. Siku moja nikiwa kwenye moja ya kumbi za starehe nilimuona kijana mmoja ambaye nilivutiwa naye.

Niliamua kumtongoza na yeye alikubali bila kipingamizi, kuanzia hapo nikawa na yule kijana ambaye nilikuwa natanua naye katika kumbi za starehe. Mmh! Kweli usichokijua sawa na usiku wa giza, kumbe yule kijana alikuwa na akili nyingi. Katika maisha niliyoishi naye kwa kuonesha mapenzi mazito na kumhudumia kwa kila kitu kumbe alikuwa na lake moyoni.

Siku moja alinizidi akili na kuniibia kiasi kikubwa cha pesa, ilikuwa ni nusu ya pesa niliyoachiwa na Emma Mo kwa kunidanganya amepata nyumba na mimi mapenzi yaliniziba macho nilimwamini kwa kumpa pesa za kulipia nyumba kumbe ndiyo nilimpa nauli ya kunitoroka.

Sikumuwaza sana kwa kuwa benki nilikuwa na milioni nne niliamua nusu ya pesa kununua vito vya dhahabu, kwa kujua hali mbaya ilikuwa njiani lazima niwe na vitu vya kumvutia mwanaume pale nitakapochemsha maisha.

Japokuwa mwanzo nilikuwa mgumu lakini nilijikuta nakubali ofa za wanaume, lakini nilichagua wanaume wenye pesa kutokana na umbile na uzuri niliokuwa nao, hakuna mwanaume aliyekataa dau nililomwambia.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.

Leave A Reply