The House of Favourite Newspapers

Nilivyoteseka Kwenye Mianzi ya Kichawi – 7

0

ILIPOISHIA
Nilifurahi sana kimoyomoyo kupata nafasi hiyo, nikajiambia “lazima nipange ya kumuambia mfalme ili kujiokoa, hiyo ni last chance yaani nafasi ya mwisho kwangu na jamaa zangu kuweza kujiokoa.
“Vipi, mbona kama unataka kuniambia kitu?”

“Nihakikishie tu kwamba mfalme nitaongea naye?”

“Utaongea naye, ni sheria, kuna wengi sana wanaokoka kwa kusema maneno ya mwisho hayo wakiyapangilia vizuri na kumuingia mfalme, mnaweza kupunguziwa adhabu.”
“Nitashukuru sana kupata nafasi hiyo.”
“Sawa. Nenda kalale usubiri kesho, siku ya kufa na kupona,” alizidi kunishauri.SONGA NAYO…
Tulijitenga na askari huyo na kukaa pembeni huku tukimchungulia kupitia nondo zilizowekwa mlangoni.

Niliingia kwenye sala ya kimoyomoyo kumuomba Mungu atuepushie balaa la kufukiwa tukiwa hai.
Kwa kweli sikupata hata lepe la usingizi na hali ilikuwa hivyohivyo kwa watu wengine ambao walikuwa wamekaa hatua chache kutoka nilipokuwa mimi hasa baada ya kuwaambia tumuombe Mungu kwa pamoja bila kujali dini zetu.

Waswahili wanasema saa hazigandi, hivyo nilianza kusikia majogoo yakianza kuwika. Mawazo yalikuwa mengi na nilikuwa nafikiria jinsi ya kujinasua na kifo pamoja na wenzangu.
Nilijua kuwa mfalme au chifu yule alikuwa hatanii, kweli kesho yake atatutupa shimoni kutuua.
Niliwaza tena lile wazo langu la awali la kujifanya mimi ni mtume wa Mungu. Nilijiuliza kimoyomoyo nitamshawishi nini ili aamini kuwa naweza kuwa mtume wa kweli?

Kwa kuwa nilikuwa mwanamazingaombwe niliwaza kwamba nimuombe kumuonesha maajabu fulani ya kimazingaombwe labda yanaweza kusaidia akasadiki kuwa mimi ni mtu wa Mungu na akaacha kutuua.
Niliwaita wenzangu na kuwaambia wazo langu hilo. Wote waliniunga mkono lakini tukasema ni mchezo gani wa mazingaombwe unaoweza kumteka akili akaogopa kutuua?

Mawazo yalikuwa mengi, kuna waliosemsa nimuoneshe jinsi ya kubadili mchanga na kuwa sukari, wapo waliosema nibadili majani kuwa vitambaa na wapo waliosema nigeuze maji kuwa majivu, kwa kuwa michezo yote hiyo naimudu.

Hata hivyo, kuna jamaa mmoja alisema tumuoneshe mchezo wa kumchinja mtu kisha kumfufua. Hilo wazo nililiafiki.Sasa kivumbi kilikuwa je tutapata nafasi ya kuonana tena na huyo mkuu wa pale na kupata nafasi hiyo kabla ya kwenda kutumbukizwa shimoni ili tufe?

Baada ya majadiliano hayo niliangalia saa yangu mishale ilikuwa inaonesha ni saa 10 alfajiri, wote tulikuwa tumejikunyata sehemu moja mithili ya kuku wa kufugwa wanavyojikusanya kwenye taa wakati wa usiku ili wapate joto.

Wote walijua kuwa mkombozi wao katika sakata hilo la kufukiwa kwenye shimo tukiwa hai ni mimi. Swali lililokuwa likigonga kwenye vichwa vyetu ni je, tutapata nafasi ya kumuomba huyo mfalme ili tumuoneshe manjonjo hayo?

Alfajiri hiyo nilisikiliza kwa makini kama nitasikia adhana, lakini sikusikia, hata ilipofika saa kumi na mbili nilisikiliza kama nitasikia kengele ya kanisani ikigongwa, pia nayo sikuisikia.
Nikajua kuwa watu wa pale hawana dini tunazozijua sisi. Yaani hawaujui Uislamu au Ukristo.
“Ndiyo maana hawana ubinadamu,” nilijishtukia nikisema kwa sauti.

“Unazungumza na nani?” alinihoji kijana mmoja.
“Ahh, nimewaza sana na kujishtukia nikisema hivyo, hawa jamaa wanaotushikilia hawana dini.”
“Kwa nini unasema hivyo?” aliniuliza kijana yule.
Nikamweleza sababu kutokana na mawazo yangu na kuunganisha na kutosikia viashiria vya dini tulizozizoea wakati wa alfajiri au asubuhi kama hiyo.

Yule kijana nilipomwambia hivyo hakunijibu badala yake alijikunyata na kuegemea ukuta uliokuwa na baridi kali kutokana na hali ya hewa ya siku hiyo. Kulikuwa na baridi kali na bahati mbaya sana hatukuwa na shuka za kujifunika.

Walioteseka zaidi kwa baridi ni baadhi ya vijana ambao walivaa mafulana maarufu kama ‘kaawoshi’, niliwasikia baadhi yao wakitetemeka na meno yao kugongana. Niliwahurumia sana lakini nadhani waliingiwa na woga zaidi kwa kujua kuwa bado saa chache uhai wetu ukatishwe.

“Kweli. Sasa kumepambazuka, kifo chetu kinakaribia,” nilisema na kuwaangalia wenzangu walioonekana kukata tamaa.“Kaka saa ngapi?”Mmoja wao aliniuliza. Niliangalia saa nikamwambia kuwa ni saa kumi na mbili na robo na tukiangalia nje tuliona mwanga wa jua ukianza kuchomoza.

Haukupita muda mrefu tangu yule kijana aniulize swali kwani alitokea askari ambaye hakuwa yule wa usiku na akaja moja kwa moja kwenye geti letu na kulifungua.
“Wote tokeni nje,” alisema kwa amri. Alionekana ni mnene na mrefu pia alikuwa akionekana kana kwamba ni mcheza kareti kwa sababu niliangalia mikono yake nikaona ina sugu kwenye vidole na pia misuli yake ya kwenye mikono na kifua ilikuwa mikubwa.

Tulitolewa nje na baada ya kutoka niligundua kuwa kumbe kulikuwa na askari wengi na wote walikuwa wakituangalia, walipangwa mistari miwili na sisi tukawekwa kati.

Upande wetu wa kushoto ndipo kulipokuwa na godauni ambalo wasichana walilazwa, nao walitolewa nje na kuamriwa kusimama msitari mmoja kama tulivyokuwa tumesimama.
Wengi wao walikuwa na macho mekundu bila shaka kutokana na kulia usiku kucha kwa sababu ya hofu ya kifo tulichotangaziwa jana yake.

“Nisikilizeni kwa makini. Mimi naitwa Kamanda Ben Mtwanga,” alisema yule askari mwenye miraba minne ambaye nilihisi alikuwa kamanda wao.“Wote tutawapeleka kwa mfalme ili mkaagane naye kabla ya kupelekwa kwenye shimo la kifo ambako mtatupwa humo.

“Mkifika kwa mfalme kila mmoja wenu atapewa nafasi ya kuzungumza na kumwambia mfalme kile alichonacho moyoni na hasa kuhusu maisha yako huko unakotoka.

“Unatakiwa uwe huru kuzungumza na usiwe na wasiwasi kwa sababu hiyo ni nafasi yako ya pekee.
“Kama unataka kusamehewa utamwambia na utatoa sababu nzito ambayo unafikiria inaweza au zinaweza kukutoa katika janga hili zito ambalo adhabu yake ni kupoteza maisha, ukiwa makini unaweza kupona na adhabu hii, kuna mwenye swali?” aliuliza yule kamanda.
“Ndiyo, tunalo,” nikasema.
“Uliza, wewe si ndiye kiongozi wa wahalifu hawa?”

Leave A Reply