NIMEPATA DAWA YA TRAFIKI WALA RUSHWA; TUITUMIE !

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu

KAZI ya kufanya kila siku bila kuimaliza inachosha. Hata kula nako kusikokuwa na kikomo ni hatari kwa afya; vipi suala la Askari wa Usalama Barabarani Trafiki kujihusisha na vitendo vya rushwa likemewe miaka yote bila kukinai?   

 

Yako mambo mawili duniani ambayo yanaweza kulifanya jambo lolote lisitimie. MOJA ni mhusika kukosa nguvu au uwezo wa kulimaliza na PILI ni kutokuwa na utashi wa kulitimiza.

Kwenye jambo hili hesabu haziongopi; wanasiasa kaeni kando maana nimejiweka sawa kusema kuhusu tatizo la baadhi ya Trafiki kujigeuza wakusanya mapato yanayoingia kwenye matumbo yao.

 

Potelea mbali Trafiki wakichukia; kwangu mimi heri chuki inayolikomboa taifa kuliko upendo unaoliangamiza. Awamu ya Tano ya Serikali imeamua kuleta mageuzi lakini wapo ambao wangali wanashupaza shingo zao. Rais John Pombe Magufuli anafagia lakini wengine kwa makusudi wanachafua.

 

Zaidi ya miaka 57 ya Uhuru wetu mizizi ya rushwa ni ileile; kila utafiti ukifanywa idara ya mahakama, polisi hazikosi kwenye orodha. Huhitaji kushiba sana ili ufanye kazi ya kuwanasa polisi na mahakimu wanaokula rushwa; vipi dhambi hii haikomi kwenye taasisi hizi?

 

Majibu yako mawili, wenye mamlaka hawana nguvu au uwezo wa kuwakomesha wala rushwa hivyo waondolewe au hawataki rushwa ikome kwa sababu wananufaika nayo, budi napo viongozi watumbuliwe ili vita ya rushwa ikome. Miaka mitatu iliyopita tuliwahi kufanya uchuguzi kuhusu Trafiki kujihusisha na rushwa; tukakusanya ushahidi wa kutosha na kuuchapisha kwenye gazeti.

 

Kilichotokea iligeuka vita kati ya baadhi ya Trafiki na magari yanayomilikiwa na kampuni yetu. Ilikuwa kama kisasi cha nyati waliojeruhiwa na majangili. Kamanda wa Usalama Barabarani wakati ule alikuwa Mohamed Mpinga; ikanilazimu kwenda ofisini kwake kumuona na kumwelezea juu ya vita yetu kati ya ufisadi na visasi vya mafisadi; itoshe kusema aliwakomesha na mambo yakaisha.

 

Nimeumbwa kuitetea haki, wanaonifahamu wanaweza kunielezea vizuri! Baada ya vita vyetu na Trafiki kumalizwa na Kamanda Mpinga bado baadhi ya Trafiki waliendelea kufanya mchezo wao mchafu wa kuwakamua madereva fedha za kununulia mboga majumbani mwao. Kitu hicho kiliendelea kunisumbua, tukarejea tena uchunguzi wetu; tukawanasa wengi mno tena kwa njia rahisi kabisa; tukashauriana:

 

Image result for kamanda wa usalama barabarani tanzania

Tuupeleke ushahidi wetu polisi ili wahusika wachukuliwe hatua; tukafanya hivyo! Picha, sauti na video za tuliowanasa tukawabwagia wakubwa wao wahangaike na wapokea kitu kidogo; sisi tukaondoka zetu; kilichoendelea hatukijui hadi leo. Tumekuwa hatufanyi hivyo kwa sababu tunataka kumfukuzisha askari yeyote kazi hapana! Tunaitetea haki isimame mahali pake na hata ninapoandika haya nia yangu ni hiyo.

 

Wiki mbili zilizopita nilipanda daladala kutoka Kariakoo Gerezani kwenda Makumbusho; nikapata kisa kilichoniumiza ambacho ndicho kilinisukuma kuanza kuwafanyia tena Trafiki uchunguzi wa namna wanavyochukua rushwa kutoka kwenye gari hasa daladala.

 

Kisa chenyewe ni hiki: Nikiwa ndani ya daladala tukiwa eneo la Urafiki, Ubungo jijini Dar, dereva alisimamishwa na Trafiki, alikaa dakika kadhaa Trafiki hakuja kwenye gari kukagua.

Ikabidi kondakta ashuke ili kumfuata; kondakta aliporudi dereva alimuuliza kachukua ngapi?

Kondakta akamjibu: “Mbili”. Abiria wengi hawakuelewa, dereva akaanza kulalamika: “Kungekuwa na kazi nyingine ningefanya, huwezi mtu kuamka saa tisa usiku, unarudi saa sita, hujaona watoto wako halafu huna hata hela, kazi unawafanyia wengine.”

 

Nikamuuliza; kuwafanyia kazi wengine maana yake nini? Akasema Trafiki wanawasumbua sana, kila kona wanasimamisha gari wanataka hela, akasema hata aliposimama pale Urafiki, Trafiki kachukua shilingi elfu mbili, aliposimamishwa Magomeni nako alitoa kiasi hicho. Malalamiko ya dereva yule yalikuwa mengi, yaliwachoma wengi na wengi waliwatuhumu vikali baadhi ya Trafiki kuwa ni hodari mno kwa rushwa; hapo ndipo safari yangu ya uchunguzi ilipoanza tena, nashukuru nimefanikiwa mno!

 

Kama binadamu unaweza kujipa uhusika, unaamka usiku wa manane, unalala usiku mnene halafu mtu anakuja kula jasho lako kwa kunyoosha kidole tu bila hata kukagua kosa la gari anataka umpe 2,000; natamani uhusika huu auvae Kamanda wa Trafiki nchini Fortunatus Muslim, auvae kila mkuu wa Trafiki halafu tuone kama rushwa kwa trafiki ni jambo linalotakiwa kufanyiwa mchezomchezo kulishughulikia!

 

Binafsi nimeumizwa, siyo tu na simulizi ya dereva bali namna ninavyofahamu kutafuta kwa jasho na uchungu wa kudhulumiwa unachojikipata kwa jasho, nikisema hivi madereva daladala na makondakta wananielewa zaidi. Rushwa ya Trafiki haina kificho, iko waziwazi, nenda Magomeni mida ya asubuhi utakuta baadhi ya Trafiki wako pale wanakusanya kodi za madereva.

 

Ukifika pale utakuta foleni ya makondakta wakielekea ‘kumuona’ Trafiki. Ukitoka hapo Urafiki wapo, Kimara Bucha nako wapo, kila kona ya jiji utawakuta wanakimbizana na daladala na vigari vidogo vya mizigo kuvikamua rushwa. Najiuliza hivi hawa wakubwa wao hawaoni uovu huu, wangejaribu kuvaa pama siku moja na kupanda daladala wangejionea mambo ya ajabu kwa askari wao.

Image result for kamanda wa usalama barabarani tanzania

Niyazungumza haya sitaki kuamini kama serikali hii ya Magufuli haina nguvu ya kukomesha rushwa barabarani! Nasita pia kukubaliana na sababu ya pili kwamba serikali haina utashi wa kutokomeza rushwa kwa trafiki.  Tatizo kubwa tulilonalo Watanzania wengi ni kuishi kwa kulalamika! Siku ile wakati dereva anakamuliwa fedha wengi waliona; hawakufanya chochote. Dereva alipoanza kulalamika nao wakaanza kulalamika baadaye mambo yakapoa.

 

Hatutakiwi kuishi hivi, MIMI NIMEPATA DAWA YA KUKOMESHA RUSHWA KWA TRAFIKI nayo ni kila mwananchi kuingia vitani. Najua wengi tuna simu za kisasa kuanzia leo ukiona tukio la Trafiki kuchukua rushwa piga picha, chukua video kisha isambaze picha hiyo mitandaoni kwa nguvu, ukiambatanisha na maneno haya:

 

TRAFIKI MAKINI AKIWA KAZINI.

Usiseme anachukua rushwa utachukuliwa hatua! Weka picha yako halafu msifie tu Trafiki huyo kwa kazi nzuri; iache picha iongee yenyewe. Tukifanya hivi kwa wingi wetu naamini wataaibika na kuacha tabia za kuchukua rushwa. Kama hilo halitoshi wenye namba za simu za makamanda wa mikoa, wakipata picha za Trafiki wala rushwa wazitume kwao pia na kuwasifia kwa kazi nzuri.

 

Tukishirikiana kwa pamoja rushwa itakoma, tupaze sauti sote kumsadia vita Rais Magufuli, rais wa wanyonge na rais asiyependa rushwa. Tusikubali kuishiwa nguvu katika vita hii, tusikubali pia kuonekana hatuna utashi wa kukomesha rushwa, safari ya ukombozi imeanza lazima wote tufike kwenye nchi ya haki.

VIVA TANZANIA, VIVA MAGUFULI, VIVA VITA DHIDI YA RUSHWA. 

MAKALA: RICHARD MANYOTA, UWAZI


Loading...

Toa comment