Nisamehe Latifa-44

Waliendelea kuzungumza ndani ya gari, Dominick ambaye naye alipewa heshima kubwa alikuwa ndani ya gari hilo, hakuzungumza chochote kile, alibaki kimya huku masikio yake yakiwa makini kusikiliza na ubongo wake kuwa makini kukariri kwa ajili ya kutengeneza makala yake.

Safari ile iliendelea mpaka walipofika katika Hoteli ya Kilimanjaro, wakateremka kisha kuingia ndani. Hakukuwa na wateja wengi, wale waliokuwepo, walitakiwa kubaki haohao na hata wale waliotaka kupanga hotelini, hawakuruhusiwa mpaka Latifa atakapoondoka.

Ratiba ilikwishapangwa, Latifa alitakiwa kukaa hapo hotelini mpaka kesho yake ambapo angechukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huko, angefanya ziara ya kuzunguka kwa wagonjwa kisha kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala na mwisho kabisa kuitwa katika Kituo cha Televisheni cha Global.

Mawazo juu ya Dominick hayakuisha, picha ya mtu huyo ilikuwa ikimjia kichwani, alimpenda mno, hakutaka kumwambia ukweli kwani alikumbuka maneno aliyomwambia nchini Senegal kwamba asije siku akamwambia kwamba alikuwa akimpenda.

Usiku ulikuwa mrefu, alibaki akiwa amekumbatia mto tu huku mwili wake ukianza kutetemeka, hakuwa na hamu ya kuwa na mwanaume mwingine, aliyekuwa akimtaka kipindi hicho alikuwa Dominick tu.

Baada ya kukaa mpaka saa saba usiku, Latifa akashindwa kuvumilia, alichokifanya ni kuchukua simu yake na kwenda sehemu ya majina, akaanza kulitafuta jina la Dominick.

“Mungu! Naomba anielewe,” alisema Latifa.

Alipoliona jina la Dominick, hapohapo akapiga namba hiyo na simu kuanza kuita. Wakati inaita, mwili wake ukazidi kutetemeka, japokuwa kulikuwa na kiyoyozi kilichokuwa kikifanya kazi lakini kijasho chembemba kikaanza kumtoka.

“Hallo!” aliita Dominick kwenye simu.

“Hallo Dominick, naomba uje chumbani,” alisema Latifa kwa sauti ndogo.

“Kuna nini?”

“Wewe njoo tu!”

“Kuna amani lakini?”

“Ipo, tena nyingi tu, naomba uje,” alisema Latifa.

“Sawa!” alijibu Dominick na kukata simu.

Moyo wake ukapoa, akajisikia amani moyoni mwake, muda huo, usiku huo ulitulia alikuwa akimsubiri mwanaume aliyekuwa na mapenzi naye, Dominick afike chumbani humo.

Baada ya dakika kadhaa kupita, akasikia mlango ukigongwa, akashusha pumzi ndefu, akasimama na kuanza kuufuata, alivalia nguo laini ya kulalia iliyoyafanya maungo yake kuonekana vilivyo, akaufuata mlango na kuufungua, alipomuona Dominick tu, mapigo ya moyo wake yakaanza kuongeza kasi, akahisi kama moyo ungeweza kuchomoka.

“Karibu,” Latifa alimkaribisha Dominick.

“Asante.”

Dominick akaingia ndani, yeye mwenyewe alichanganyikiwa, vazi alilovaa msichana huyo lilimuweka kwenye wakati mgumu, kila kitu maungoni mwake kilionekana wazi, wazimu ukampanda, kila alipojitahidi kujikaza kiume, akashindwa kabisa.

“Umependeza,” alisema Dominick, alishindwa kuvumilia, japokuwa lilikuwa ni vazi la kulalia tu lakini akakosa maneno, akaona bora asifie hivyohivyo tu.

“Na hili vazi?” aliuliza Latifa.

“Ndiyo! Koh koh koh…u mzuri sana Latifa,” alisema Dominick na kujikoholesha, akili yake ilihama, alichokuwa akikifikiria ni mapenzi tu.

“Nashukuru!” alisema Latifa na papo hapo akamvuta Dominick na kumlaza kitandani, wakabaki wakiangaliana kama paka waliotaka kupigana.

Kila mmoja damu ilimchemka kupita maelezo, sekunde kadhaa mbele walijikuta wakiwa wamekumbatiana.

Nini kiliendelea? Usikose kufuatilia wiki  ijayo.


Loading...

Toa comment