The House of Favourite Newspapers

Njia ya kutafuta na kupata mafanikio

0

Kila mmoja ana hofu maishani mwake lakini kinachotutofautisha ni kiwango cha hofu alichonacho kila mmoja. Bila shaka hata wewe msomaji wangu nikikuuliza ni kitu gani unachokiogopa zaidi, utanitajia. Kinaweza kuwa kimoja, viwili au vingi lakini kimsingi, wengi wetu kuna mambo tunayoyaogopa.

Wapo ambao wanahofia mambo machache kama kifo, maradhi, kupoteza kazi na kufilisika.Wapo wengine ambao kwao kila kitu wanakiogopa. Wanaogopa kutengwa na jamii, kukataliwa na watu wanaowapenda, kusemwa vibaya, kufeli, kukosea, kufokewa na mabosi zao na kadhalika.

Hata wakitaka kuvuka barabara, badala ya kutanguliza umakini wa kutazama huku na kule ili kama hakuna magari ndiyo wavuke, wao hutanguliza hofu ya kugongwa na magari na kufa kifo kibaya, matokeo yake wanavuka hata sehemu zisizostahili kwa sababu hofu ina kawaida ya kuupumbaza ufahamu.

Kila kitu katika maisha yao kimejawa na hofu, hawajiamini tena, wanaishi zaidi kuwafurahisha watu wengine kuliko kujifurahisha wao na nafsi zao, kila wanachofanya wanahofia wengine watasema nini! Ni watumwa wa hofu zao wenyewe.

Ni ukweli ulio wazi kwamba, hofu ni kama wingu ambalo watu wengi hujitengenezea maishani mwao na kusababisha washindwe kuuona mwanga wa jua ambao kwa kawaida huzibwa na mawingu. Kama nilivyosema, hofu huupumbaza ufahamu, kadiri unavyozidi kuwa na hofu maishani mwako, ndivyo unavyozidi kujiweka mbali na mafanikio.

Chukulia mfano, wewe ni mfanyabiashara mwenye mtaji mdogo, anakuja mtu na kukupa ushauri kwamba kuna biashara fulani ambayo ukiwekeza mtaji wako ulionao na kuongeza juhudi, ndani ya muda mfupi utapata mafanikio yatakayokufanya upige hatua kubwa.

Kwa sababu umetanguliza hofu mbele, utahisi anayekupa wazo hilo anataka kukutapeli, anataka kuona unaanguka kimtaji. Badala ya kuthubutu, ule mtaji wako mdogo ulionao, utaendelea kuukumbatia kama umebeba yai au glasi na matokeo yake, hutakuwa na ujasiri wa kuziendea fursa kubwa, hata zile ambazo ni za wazi kabisa kwa sababu ya hofu ya kushindwa.

Unafikiri utaweza kupiga hatua kwa mtazamo huo? Haiwezekani, utabaki palepale miaka nenda rudi, utafanya kitu kilekile kwa kiwango kilekile mpaka unazeeka. Utakuwa unahisi wenzako wanaofanikiwa labda wanatumia ‘ndumba’ lakini kumbe mchawi wako ni wewe mwenyewe kwa kutanguliza hofu.

Chukulia mfano mwingine kwamba wewe ni muajiriwa. Unajituma sana katika kazi lakini kipato chako ni kidogo ukilinganisha na mahitaji yako. Unahitaji kula, kulipa kodi na karo, unahitaji kupata mahitaji yako ya msingi lakini mshahara unaopata haukidhi kabisa mahitaji yako.

Kwanza huwezi kuwa na ujasiri wa kumvaa mwajiri wako na kumueleza hali halisi kwa sababu tayari umetanguliza hofu; unamuona bosi wako kama ‘mungu mtu’. Hata ikitokea umejikakamua na kumueleza lakini akakataa kukusikiliza, huna ubavu wa kuanza kutafuta kazi sehemu nyingine kwa sababu tu unahisi ukienda kufanya kazi sehemu nyingine, utaharibu na kufukuzwa.

Unaogopa mazingira mapya, unaogopa kufanya vitu vipya, kila kitu kwako unatanguliza hofu. Matokeo yake utaendelea kufanyakazi ileile, kupata mshahara uleule na kukumbana na shida zilezile maisha yako yote.

Kumbe kama ungekuwa na ujasiri wa kuishinda hofu yako, hata kama utapitia matatizo kwa kipindi fulani lazima mwisho wa siku mapambazuko yataonekana maishani mwako na shida zote ulizopitia zitabaki kuwa historia.

Leave A Reply