The House of Favourite Newspapers

Waheshimiwa, ‘sinema’ mjengoni hazitusaidii!

0

KWENU Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Niwasalimu kwa umoja wenu kwa vile siwezi kumsalimu mmojammoja.Poleni na kazi za kujenga taifa letu ambalo limetafunwa na wajanja wachache kwa muda mrefu. Mkitaka kujua hali yangu, mimi ni mzima wa afya. Nashuhudia utukufu wa Mungu kila siku, kwa pamoja tuseme, Amina.

Nimewakumbuka leo kwa barua maana nami nina jambo nataka kuwaambia. La kwanza, nataka kuwaambia, Bunge la 11 kila mtu alikuwa akilisubiri kwa hamu.

Kila Mtanzania anataka kuona mabadiliko ya kweli kimaisha. Wamechoka maisha ya mateso. Wamechoka kuishi katika hali ngumu. Huduma mbaya hospitalini, watu wanapoteza maisha kwa kukosa huduma. Imani kubwa wananchi wameiweka kwa rais wao wa awamu ya tano, Dk. John Pombe Magufuli.

Dk. Magufuli anasaidiwa na nyinyi katika kutimiza ndoto za Watanzania. Ameonesha mfano wa kutumbua majipu. Ameonesha jinsi gani anachukizwa na rushwa na ubadhirifu. Kazi imebaki kwenu nyinyi ambao mnatunga sheria na kupitisha bajeti ya serikali.

Waheshimiwa wabunge, imekuwa ni kama desturi yenu kila bunge linapowadia, baadhi yenu badala ya kujadili vitu vya msingi, mnakazana kuleta porojo ambazo hazina kichwa wala miguu. Mnasababisha vurugu ambazo si za lazima.

Sisemi kwamba wapinzani kila wanaposababisha vurugu wanakuwa hawana hoja lakini kuna wakati unaona wanafanya mambo kishabiki. Nikiwa kama mwananchi wa kawaida, kuna vitu ambavyo wakati mwingine vinakuwa havina tija.

Mbunge anaomba mwongozo kwamba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepotosha kuhusu suala la elimu bure, kuna baadhi ya shule bado zinachangisha wazazi mahitaji mbalimbali.
Naibu Spika, Tulia Ackson alitoa ufafanuzi kwamba waziri alieleza wazi kwamba mfumo wa elimu bure ni mpya na waziri ameeleza wanazikusanya changamoto zote ili wazifanyie kazi, baadhi yenu mkafanya vurugu, mkatoka bungeni.

Kabla ya hapo, wabunge wa upinzani walifanya vurugu kwa sababu ya kung’ang’ania msimamo wa kutojadili hotuba ya rais hadi pale muafaka wa suala la TBC1 kuruhusiwa kuonesha ‘live’ matangazo ya Bunge.

Sitaki kusema katika hilo waliotoka walikuwa na hoja au la lakini hapa nataka mnielewe kwamba zile sinema za kurushiana matusi, kejeli za kipuuzi kwetu sisi wananchi wa kawaida hazitusaidii. Tunataka mbishane kwa hoja na mwisho wa siku mkubaliane kwa hoja.

Tukiona mnatupiana maneno ya vijembe au baadhi ya wabunge wanabisha vitu bila sababu ya msingi na kusababisha vurugu, tunawahesabu kwamba hamna uchungu na maumivu wanayoyapata wananchi waliowachagua.

Tunawaona kama ni watu wanaotaka kuchelewesha mambo, kupiga soga kisha mpate posho ziwasaidie na matumbo yenu. Ndugu zangu, tumieni muda wenu vizuri hapo mjengoni. Jengeni hoja zenye masilahi makubwa kwa taifa na si vitu vidogovidogo viwapotezee muda na kuleta vurugu. Mnapojadili mambo yenu, acheni ushabiki wa kivyama. Wekeni masilahi ya taifa mbele. Bishaneni kwa hoja na wale watakaoshindwa, wakubali bila kufanya vurugu, kejeli wala maneno ya vijembe.
Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa, wenu katika ujenzi wa taifa;
Erick Evarist

Leave A Reply