The House of Favourite Newspapers

Nyie Yanga Raha Asikwambie Mtu! Watetea Ubingwa Wao wa Ligi – Video

0

NYIE Yanga raha asikwambie mtu! Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobaki kwenye michuano ya kimataifa, unaweza kusema huu ni mwaka wao kutokana na mengi mazuri wanayoyafanya ndani ya uwanja.

Yanga ambao jana walikuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, wamefanikiwa kutetea ubingwa wao wa ligi hiyo na kufanya hadi sasa kuuchukua mara 29, ikiwa ni nyingi zaidi ya timu yoyote.

Katika mchezo wa jana uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar, Yanga ilishinda 4-2 dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao ya Kennedy Musonda (dk 39), Mudathir Yahya (dk 70 na 90) na Farid Mussa (dk 88). Mabao ya Dodoma Jiji yalifungwa na Collins Opare (dk 59) na Seif Karihe (dk 67).

Timu hiyo ambayo Jumatano ijayo ina mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya nusu fainali dhidi ya Marumo Gallants itakayochezwa nchini Afrika Kusini, ikitoka huko ina kibarua kingine nyumbani.

Hadi sasa, Yanga ikiwa na mataji mawili msimu huu, Ngao ya Jamii na Ligi Kuu Bara, inasaka mengine mawili kulinogesha zaidi kabati lao la makombe.

Ikitoka Afrika Kusini kucheza mechi ya nusu fainali ikiwa na mtaji wa mabao 2-0, itacheza nusu fainali nyingine ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Singida Big Stars, ikipenya, itakutana fainali na Azam FC.

Kikosi hicho chini ya Kocha Nasreddine Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze, msimu huu kwao una mafanikio makubwa zaidi kuwazidi watani zao wa jadi, Simba waliomaliza msimu bila ya taji lolote.

Ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu iliobeba Yanga, ni wa 29, ikiwa ni idadi kubwa zaidi na kuwafunika Simba waliobeba mara 22.

ORODHA YA MABINGWA WA TANZANIA TANGU 1965

Sunderland (Simba – 1965), Sunderland (Simba – 1966), Cosmopolitan (1967), Yanga (1968), Yanga (1969), Yanga (1970), Yanga (1971), Yanga (1972), Simba (1973), Yanga (1974), Mseto (1975), Simba (1976), Simba (1977), Simba (1978), Simba (1979), Simba (1980), Yanga (1981), Pan Africans (1982), Yanga (1983), Simba (1984), Yanga (1985), Tukuyu Stars (1986), Yanga (1987), Coastal Union (1988), Yanga (1989), Simba (1990), Yanga (1991), Yanga (1992), Yanga (1993), Simba (1994), Simba (1995).

Yanga (1996), Yanga (1997), Yanga (1998), Mtibwa Sugar (1999) Mtibwa Sugar (2000), Simba (2001), Yanga (2002), Simba (2003), Simba (2004), Yanga (2005), Yanga (2006), Simba (2007), Yanga (2007/08), Yanga (2008/09), Simba (2009/2010), Yanga (2010/2011), Simba (2011/2012), Yanga (2012/2013), Azam (2013/2014), Yanga (2014/2015), Yanga (2015/2016), Yanga (2016/2017), Simba (2017/2018), Simba (2018/2019), Simba (2019/2020), Simba (2020/2021), Yanga (2021/2022) na Yanga (2022/2023).

Leave A Reply