The House of Favourite Newspapers

OFM Kazini… Chimbo la Unga, Bangi Laibuliwa

0

 

Chimbo lenyewe hili hapa

 

LICHA ya juhudi kubwa zinazofanywa na vyombo vya dola katika kutokomeza uhalifu wa aina zote, ikiwemo biashara na matumizi ya madawa ya kulevya, chimbo la uuzwaji na utumikaji wa vileo kama gongo, bangi na madawa ya kulevya, limeibuliwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi Dar es Salaam, karibu na sehemu ya kupakia meli za abiria waendao Zanzibar.

Kitengo Maalum cha Kufichua Maovu (OFM) cha Global Publishers, mwishoni mwa wiki kilitonywa na msamaria mwema juu ya kufanyika kwa biashara ya madawa ya kulevya yakiwemo bangi na ‘unga’ sambamba na unywaji wa pombe haramu ya gongo.

“Pale utafikiri hamna serikali, yaani kuanzia asubuhi hadi jioni, watu wanavuta, wanakunywa na usiku wanafanya mambo ya kifuska, lakini cha ajabu haya yanafanyika umbali wa mita zisizozidi mia tatu tu kutoka kilipo Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.

 

 

“Hali hii inasababisha usalama kuwa mdogo kwa watu wanaopita maeneo haya kwa sababu watu wanakuwa wameshalewa asubuhiasubuhi na mara nyingi watu wanakabwa hadharani na hakuna anayechukua hatua zozote,” kilisema chanzo hicho kilichosema ni mfanyabiashara ndogondogo, ambao nao ni waathirika wa kuporwa.

 

OFM waliingia kazini na kulifikia eneo hilo, ambako walishuhudia vibanda vingi vya maboksi vimejengwa na ndani yake, watu wakiendelea na shughuli za biashara za unga, bangi na gongo kama kawaida.

 

 

Katika mojawapo ya vibanda hivyo, mama mmoja alionwa akiuza gongo huku vijana wa kiume na kike, wakivuta madawa hayo ya kulevya bila hofu yoyote. Wakati shughuli hiyo ikiendelea, baadhi ya wananchi walikuwa wakipita kuyaelekea magenge ambayo yamejengwa
 eneo hilo, huku wakikumbana na harufu kali ya bangi.

 

Hata hivyo, zoezi la kupiga picha eneo hilo lilikuwa gumu, kwani vijana waliokuwa hapo walikuwa makini kutazama mtu yeyote waliye na mashaka naye na wakati mmoja nusura kamanda wa OFM ashtukiwe.
Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Salum Hamduni ambaye baada ya kuelezwa kuhusu kinachoendelea eneo hilo, alikiri kulifahamu na kueleza kuwa kume-kuwepo na oparesheni za mara kwa mara zinazoendeshwa na polisi ili kuwakabili wahalifu hao.

 

“Tumekuwa tukifanya doria mara kwa mara kwa sababu tunafahamu uwepo wa makundi ya kihalifu pale, wengi tumewakamata na tumewafikisha mahakamani, wengine wako katika vituo vya polisi na wengine walihukumiwa,” alisema Kamanda Hamduni.

Alisema hata hivyo, zoezi la kukamata wahalifu katika eneo hilo ni endelevu na kulishukuru Risasi Mchanganyiko kwa taarifa hizo, alizosema zitaendeleza harakati zao kuhakikisha vitendo vyote vya kihalifu vinatoweka katika eneo hilo.

 

MWANDISHI WETU, RISASI MCHANGANYIKO

Leave A Reply