The House of Favourite Newspapers

OFM Yabaini Jipu Bima za Afya

0

IMG_0724Waziri wa afya Ummy Mwalimu.

Na Mwandishi Wetu, Risasi mchanganyiko
BAADHI ya madaktari wasio waaminifu, wanashiriki kuihujumu mifuko ya Bima za Afya na kuisababishia hasara ya mamilioni ya fedha, Oparesheni Fichua Maovu (OFM) imebaini.

Siku kadhaa zilizopita, chanzo cha kuaminika kiliwasiliana na OFM na kuelezea jinsi hujuma nzito zinavyofanyika kwenye mifuko hiyo inayohusika kugharamia matibabu ya wanachama wake.

“Kuna upigaji mpya umeibuka, ni vigumu sana kwa mtu wa kawaida kuushtukia lakini ukifuatilia utagundua. Madaktari wanakula njama na wagonjwa feki kuihujumu, nyie fuatilieni mtagundua ukweli,” kilisema chanzo chetu.

MMGL0348Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Rehani Athuman.

OFM KAZINI
Baada ya kupokea taarifa hizo, kama kawaida, OFM waliingia kazini. Kwa nyakati tofauti, walifanya oparesheni za kimyakimya katika hospitali, vituo vya afya na maduka ya madawa yanayowahudumia wagonjwa wanaotibiwa kwa kadi za bima za afya.

KILICHOBAINIKA
Baadhi ya madaktari wasio waaminifu, wanashirikiana na wagonjwa feki kuihujumu mifuko ya bima za afya kwa kuwaandikia dawa zinazouzwa bei mbaya au wakati mwingine kuandikiwa huduma ghali kama upasuaji wakati katika hali halisi, hawapatiwi huduma hiyo.

“Unajua mgonjwa akiwa na kadi, hakuna kikomo cha gharama anazotakiwa kutumia. Hata kama ataandikiwa dawa za shilingi milioni moja, atapewa tu halafu mfuko husika ndiyo utakaomlipia,” alisema nesi mmoja kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa kuwa si msemaji.

MCHEZO UNAVYOKUWA
Kachero aliyepandikizwa na OFM kama mgonjwa, alienda kwenye hospitali moja maarufu jijini Dar es Salaam na zamu yake ya kumuona daktari ilipofika, aliingia na kujaribu kumshawishi daktari huyo ili amuandikie dawa za bei mbaya, akishazichukua kwa kutumia kadi yake halali ya bima ya afya, akaziuze kisha wagawane fedha.

Bila kujua kwamba ameingizwa mtegoni, daktari huyo alikubali na kufunguka kwamba kama shida yake ni kuuza, hata yeye (daktari) analo duka la madawa kwa hiyo yupo tayari kumkatia ‘cha juu’ ili akachukue dawa hizo na kumkabidhi kwa ajili ya kuzipeleka kwenye duka lake.

Baada ya makubaliano hayo, daktari huyo alimuandikia kamanda wetu orodha ya dawa kibao anayotakiwa kuchukua kwenye maduka yaliyoidhinishwa kupokea kadi za bima ya afya. Kwa hesabu za harakaharaka, dawa hizo ziligharimu shilingi 620,000 (laki sita na elfu ishirini).

Kamanda wetu alitoka na kwenda kwenye duka kubwa la madawa akiwa na kadi yake ya bima ya afya ambapo alipewa dawa zote kisha akapewa fomu ya kuweka saini kama ulivyo utaratibu wa wagonjwa wanaotibiwa kwa kadi za bima ya afya.

Baada ya kufanikisha zoezi hilo, kachero wetu aliwasiliana na daktari aliyemuandikia dawa hizo, wakakubaliana kukutana nje ya kituo chake cha kazi ili ampe mzigo wake. Dakika kadhaa baadaye, kachero wetu alikutana na daktari huyo, akamkabidhi furushi la dawa ambapo daktari huyo naye alimshikisha chake.

WAHUSIKA WANAJUA MCHEZO HUU?
Baada ya kujiridhisha jinsi ufisadi huo unavyofanyika, OFM haikuishia hapo, iliwatafuta viongozi wa mifuko inayotoa huduma ya bima za afya ili kusikia kwa upande wao wanalizungumziaje suala hilo.

Rehani Athuman, Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), alipotafutwa na mwandishi wetu na kuulizwa kama anaujua mchezo unaofanywa na madaktari wasio waaminifu kwa kushirikiana na wagonjwa feki, alikiri kuujua na kuongeza kuwa tayari watu kadhaa wamechukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

“Kwanza ni kosa kisheria kwa mwanachama wetu kufanya udanganyifu wa aina yoyote na pindi akibainika, hatua kali za kisheria zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupandishwa kizimbani. Mpaka sasa kuna zaidi ya kesi 13 zinazohusiana na hujuma hizo zipo mahakamani. Kati ya hizo, kesi sita zimeshatolewa hukumu. Pia tumeshavifungia vituo 17 kutokana na kubaini kwamba vinafanya udanganyifu kama huo.

“Kwa upande wa madaktari, akikutwa na kesi ya kufanya udanganyifu kupitia mteja wetu kwa lengo la kuchukua dawa, tunawapeleka katika bodi zao kwa hatua zaidi.
“Natoa wito kwa wanachama wetu kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo vya udanganyifu vinataka kufanyika. Pia ni makosa kwa mteja kutumia kadi ambayo siyo yake ili kuepuka kuingia kwenye matatizo.

“Kwa upande wetu NHIF tumejizatiti kubana mianya yoyote ya udanganyifu na tunaomba wananchi watupe ushirikiano,” alisema Rehani.

Leave A Reply