The House of Favourite Newspapers

Pointi 21 zashikilia ubingwa Yanga

0

YANGA (2)

Mwadishi Wetu

Dar es Salaam

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kumalizika Mei 7, mwaka huu, lakini vinara wa ligi hiyo, Yanga, wanaonekana kuwa kwenye hali ngumu zaidi.

Katika mzunguko huu ambao unaonekana kuwa mkali zaidi, Yanga wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo, kwa kuwa sasa wapo kileleni wakiwa na pointi 39, wakiwa sawa na Azam, lakini ratiba inaonekana kuwabana zaidi kwenye ubingwa, huku Simba ambao wapo nafasi ya tatu baada ya kukusanya pointi 33, wakiwa na nafasi nzuri.

YANGA (5)

Yanga wanaonekana kuwa na hatari zaidi kwa kuwa watazitafuta pointi 27 ngumu huku 21 zikiwa ni za mikoani, wakati Azam ambao wapo nafasi ya pili wakitafuta pointi 24 ngumu, 21 zikiwa ni za mikoani pia lakini Simba itakuwa na wepesi kwa kuwa itavuka ‘boda’ mara tano tu, mechi nyingi ikicheza jijini Dar es Salaam.

Yanga watalazimika kuzifuata pointi tatu Mkwakwani, Tanga dhidi ya Coastal Union, halafu watatafuta nyingine kwenye uwanja mgumu wa Sokoine dhidi ya Prisons na Mbeya City, kisha watakwenda sehemu nyingine ngumu, Mwanza kuivaa Toto, halafu watalazimika tena kusaka pointi nyingine tatu dhidi ya Stand kule Shinyanga, baadaye watakwenda Mtwara kuwavaa Ndanda kabla ya kumaliza mechi za ugenini dhidi ya Majimaji kule Songea.

Hizo zitakuwa pointi 21 za kuvuja jasho kwelikweli ugenini lakini watakuwa na pointi nyingine sita za kutafuta jijini Dar es Salaam dhidi ya Simba na Azam FC, kwa hiyo jumla watakuwa na kazi ya kusaka pointi 27 ngumu.

Hali inaonekana kuwa mbaya mkoani kwa kuwa Yanga mpaka sasa wametoka sare mara tatu, moja kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mara mbili mkoani, ambapo ni dhidi ya Mgambo jijini Tanga na Mwadui, Shinyanga.

Kwa upande wa wapinzani wao Azam FC, wao watakuwa na pointi 24 za kuvuja jasho jingi ili kuzipata. Pointi 21, Azam watalazimika kukomaa kuzipata mikoani dhidi ya Prisons (Sokoine, Mbeya), Coastal (Mkwakwani, Tanga), Mbeya City (Sokoine, Mbeya), Mtibwa (Manungu, Morogoro), Toto (Kirumba, Mwanza), Kagera (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na African Sports (Mkwakwani, Tanga).

Lakini Azam watakuwa na mechi nyingine ngumu dhidi ya Yanga, hivyo kuwa na pointi 24 za kupigania.

Simba ambao wanamchekea zaidi, kama wakipanga hesabu zao vizuri, lolote linaweza kutokea, kwani ‘watapanda ndege’ mara tano tu kwenda kuwavaa Kagera (Tabora), Stand (Shinyanga), Coastal (Tanga), Majimaji (Songea) na Mtibwa (Morogoro). Mechi nyingine ngumu watakazokutana nazo ni dhidi ya Yanga na Azam jijini Dar es Salaam.

Mambo manne hatari kwa Yanga:

Pamoja na kwamba Yanga wanaweza kupata ushindi kwenye baadhi ya michezo hiyo, lakini inaonekana kuwa na hali ngumu kwa kuwa wachezaji wake watakumbana na uchovu wa kusafiri mara kwa mara.

Pili, viwanja vingi vya mikoani vinajulikana kuwa ni vibovu hivyo itakuwa ni muda wa Yanga kucheza kandanda bovu na nje ya makubaliano na kocha wao hali ambayo inaweza kuwafanya kudondosha pointi, hilo halina ubishi.

Uzalendo, pamoja na kuwa na mashabiki wengi mikoani, lakini uzalendo utakuwepo hali ambayo inaweza kuwasumbua Yanga kuondoka na pointi, uzalendo unaweza kuufanya mkoa mzima ukapambana ili timu yao isipoteze pointi kwa njia yoyote.

Kampeni za kujiokoa, hili ni jambo la kawaida sana kwa timu kufanya kampeni ili kuhakikisha kuwa inajiokoa, zinaweza kufanyika kwa njia nyingi, lakini hapa hofu ni kwamba Yanga wanakwenda kuvaana na timu nyingi ambazo kipindi hicho zitakuwa zinapambana ili kujiokoa zisishuke daraja.

Mfano Majimaji, Ndanda, pamoja na Toto, pamoja na kwamba wanaitwa Watoto wa Yanga lakini wakati huo habari itakuwa nyingine.

Timu kubwa zimekuwa na kawaida sana ya kuchezeana rafu kwenye michezo ya mikoani, hili halina ubishi na hii itakuwa nafasi kwa timu nyingine zinazowania ubingwa kuweka fitina ili kuhakikisha Yanga wanadondosha pointi na kuwapa wenyewe nafasi ya kushaini.

Leave A Reply